Wanafunzi wa Ualimu waliokosa UDOM wapangiwa vyuo vya ualimu vya serikali.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, 
Sayansi na Teknolojia imewapangia vyuo wanafunzi   wa programu maalum ya
 ualimu chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao hawakupata nafasi ya vyuo 
katika awamu ya kwanza, walioagizwa kuomba mafunzo kulingana na sifa zao
 kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE).
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu 
Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo leo, jijini Dar es Salaam 
alipokuwa akitoa taarifa kuhusu wanafunzi wanaosoma stashahada maalum ya
 ualimu wa sayansi chuo kikuu cha Dodoma.
“Mtakumbuka tuliagiza kwamba 
wanafunzi ambao walikosa sifa za kujiunga na ualimu wa sayansi waliombwa
 kuomba mafunzo yanayolingana na ufaulu wao kupitia NACTE,  Lakini baada
 ya taarifa hiyo tulipokea maombi mengi kutoka kwa vijana hawa wakiomba 
kupangiwa vyuo moja kwa moja na Wizara, wizara imetafakari na kuamua nao
 wapangiwe vyuo vya Serikali,” alifafanua Dkt. Akwilapo.
Aliendelea kusema kuwa, wanafunzi 
ambao waliachwa awamu ya kwanza na kupangiwa katika awamu ya pili ni 
wanafunzi 290 ambao walikuwa wakisomea programu ya stashahada ya ualimu 
wa sekondari na wanafunzi 1,181 ambao walikuwa wakisomea stashahada ya 
ualimu wa msingi.
Dkt. Akwilapo amesema kuwa Wizara 
imeamua kuwapangia wanafunzi hao vyuo kutokana na kuonyesha nia ya dhati
 ya kusomea ualimu ambapo wanafunzi hao wamepangiwa vyuo vya ualimu vya 
Marangu na Tabora.
Aidha, Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa
 wanafunzi hao watajigharamia masomo yao kulingana na viwango vya ada 
vilivyowekwa na Serikali. Pia amewataka kutembelea tovuti ya wizara ya 
hiyo ambayo ni www.moe.go.tz ili kuona vyuo walivyopangiwa.
Mnamo tarehe Mei 28, 2016 Serikali
 iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada 
Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma. 
Katika mchujo wa awamu ya kwanza wanafunzi 382 ndio waliokuwa na sifa ya
 kuendelea na masomo chuo kikuu cha UDOM na wengine 4,586 walipangiwa 
vyuo vya ualimu vya Serikali.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni