Misaada huwa haitozwi kodi – TRA
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imetoa ufafanuzi juu ya utozwaji wa kodi za misaada inayotolewa na
wadhamini kusaidia Sekta ya Maendeleo ya Michezo Nchini.
Ufafanuzi huo umetolewa leo na
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo kutokana
na habari iliyochapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu
Serikali kukosa mabilioni ya fedha kwa sababu ya kutokukusanya kodi ya
fedha zinazotolewa na wadhamini kwenda kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
“Fedha zinazotolewa kama msaada
kutoka kwa wadhamini huwa hazikatwi kodi lakini TRA hupata mapato yake
kutokana na matumizi ya fedha hizo hasa pale wahusika wanapozitumia
katika shughuli za kiuchumi”,alisema Kayombo.
Kayombo ametaja baadhi ya shughuli
za kiuchumi zinazoweza kuwaingizia mapato kutoka kwenye misaada hiyo
kuwa ni; kodi za waajiriwa wakiwemo makocha na wachezaji, makusanyo ya
uwanjani ,kupewa huduma za kitaalam pamoja na majengo ya kupangisha au
kupanga.
Amefafanua kuwa kama Shirikisho la
Mpira wa Miguu Nchini (TFF) linakodisha jengo basi fedha wanazopata
lazima walipe kodi ya asilimia 10 kutoka kwenye fedha hizo na kama wao
ndio wamekodi jengo kwa ajili ya matumizi yao wanatakiwa kutoa kodi ya
asilimia 5.
Kwa upande wa kodi kutoka kwa
waajiriwa, Mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa vilabu vya michezo
kuwa michezo ni ajira kama ajira zingine hivyo mishahara yao inatakiwa
kukatwa kodi kulingana na kiasi wanacholipwa.
Zoezi la kuwatoza kodi makocha na wachezaji limeanza rasmi mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni