WAKWEPAKODI WANAIATHIRI SERIKALI-WAZIRI MKUU
Amesema Serikali haina mgogoro na 
wafanyabiashara bali inawataka walipe kodi na kama kuna wanaonewa na 
watendaji wa chini kwa kubambikiziwa kodi watoe taarifa juu ya jambo 
hilo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo 
(Jumanne, 30 Agost, 2016) wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa 
Makampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohamed Dewji,
 ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imedhamiria 
kuwaunga mkono wafanyabiashara katika shughuli zao ili waweze kulipa 
kodi itakayoifanya imudu kuwahudumia wananchi katika huduma mbalimbali 
za jamii.
“Sisi msisitizo wetu ni ulipaji 
kodi, wakwepa kodi wanatuathiri. Sekta nyingine zinashindwa kuendelea 
kwa sababu hazina mtaji na kodi hazipatikani vizuri,” amesema.
Amesema “Ninyi timizeni wajibu 
wenu kwa kulipa kodi stahiki, tutawasaidia katika kufanya biashara zenu.
 Tutawasaidia katika kusimamia mambo yenu ila mjue kwamba nchi hii bila 
viwanda hatuwezi kwenda,”.
Pia amewataka wafanyabiashara 
kwenda kujenga viwanda katika maeneo ambayo malighafi zinazalishwa ili 
kuwahamasisha wakulima kuzalisha zaidi na kuwapunguzia mzigo wa 
kusafirisha malighali hizo.
Kwa upande wake Dewji 
amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wafanyabiashara wanaiunga mkono 
Serikali ya Awamu ya Tano na   hawana mpango wowote wa kuhamishia mitaji
 yao nje ya nchi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
“Huu ni uongo na uzushi tu ambao 
watu wameamua kuusambaza, mfano mimi mwenyewe nimeanza kuongeza mitaji 
katika biashara zangu. Nimefufua kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato. 
Nafungua biashara zingine mpya kubwa ikiwemo ya kufufua kiwanda cha nguo
 cha Musoma ambacho kitakuwa kinatengeneza jeans za kuuza nje ya nchi,” 
amesema.
Amesema yuko tayari kuwekeza 
kwenye ujenzi wa kiwanda cha sukari katika wilaya ya Rufiji mkoani 
Pwani. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kununua miwa tani milioni 1.2 
zitakazozalisha tani 120,000 za sukari kwa mwaka.
Mkurugenzi huyo amesema amepanga 
kuwekeza sh. bilioni 40 kwa ajili ya kukuza uzalishaji katika mashamba 
yake ya mkonge kwenye mikoa ya Pwani, Tanga na Morogoro.
Pia amewekeza sh. bilioni 70 
katika viwanda vya kusaga unga wa ngano na sembe na anatarajia kununua 
tani laki moja za mahindi katika msimu wa mwaka huu.
Mbali na kuwekeza katika viwanda 
hivyo Dewji amesema anatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza 
sabuni ya unga ambacho kitakuwa ni kikubwa kuliko vyote katika nchi za 
Afrika Mashariki na Kati.
“Tumeamua kuongeza uwekezaji 
katika viwanda ili kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuifanya Tanzania
 kuwa nchi ya viwanda. Vile vile nimefanikiwa kuishawishi kampuni kubwa 
na maarufu ya kutengeneza sigara duniani ya Marlboro kuingia nayo ubia 
na sasa tunajenga kiwanda cha sigara hizo mjini Mrogoro,” amesema.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni