VIJANA JIAJIRINI NA KUJITUMA ILI KUJILETEA MAENDELEO
Na Mwashungi Tahir /Rahma Khamis Maelezo-Zanzibar
………………………………….
Vijana nchini wametakiwa kuongeza bidii ya kujituma na kujiajiri wenyewe ili kujiletea maendeleo endelevu.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu
Wizara ya Vijana Kazi,uwezeshaji Wazee,Vijana wanawake na Watoto Maua
Makame Rajab wakati akifungua Kongamano la vijana ikiwa ni shamra shamra
ya Siku ya Vijana duniani huko katika Ukumbi wa Haileselas mjini
Zanzibar.
Amesema kujiajiri ni njia nzuri ya
kupambana na umaskini katika jamii na kuepukana na tabia ya kutegemea
Serikali pekee kuwaajiri Vijana hao.
Maua amefafanua kwamba ili Vijana
waweze kujiajiri kwa wepesi ni vyema Vijana hao wakashirikiana na wenzao
kujiunga katika vikundi vya ushirika.
Kwa kufanya hivyo kutawasaidia
Vijana hao kujikwamua katika dimbwi la umaskini na kuepukana na vitendo
viovu ambavyo vijana wengi siku hizi hujiingiza katika makundi maovu
ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya na udhalilishaji wa kijinsia.
Aidha Naibu huyo amewatia moyo
Vijana hao na kuwaambia kuwa hakuna lisilowezekana pale watakapojipanga
kupambana na changamoto za uhaba wa ajira kwa ktumia fursa zilizotolewa
na Serikali ikiwemo mikopo ya kujiwezesha kimaisha.
Akitoa mada katika Kongamano hilo
Naibu Waziri wa kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar,Lulu Msham
amesisitiza Vijana hao kukubali kijiunga katika ushirika na kujiendeleza
katika vikundi ili kuepukana na tabia ya ombaomba.
“Vijana tujitambua na tujuwe
wajibu wetu kwa kujijengea maadili mema katika jamii na tujiepushe na
kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa Amani kwani tukifanya hivyo
tutajiondeshea uaminifu Nchini,”alisema naibu waziri .
Aidha ametoa wito kwa vijana
kuzichangamkia fursa za kugombea nafasi za uongozi na kujitokeza kwa
wingi hasa wanawake ambao bado wapo nyuma kiuongozi.
Akifunga Kongamano hilo la siku
moja Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrisa Kitwana Mustafa amewataka
vijana kutafuta elimu na kuwa na maadili mema na kuweka ushirikiano
katika kazi zao za kila siku.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana
kimataifa yanatarajiwa kufanyika kesho katika Uwanja wa Mnara wa Kisonge
ambapo kauli ya mwaka huu kuelekea 2030 Tokomeza Umaskini kwa
Uzalishaji Endelevu na Matumizi yenye Tija.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni