Vyombo vya usimamizi wa Sheria vyatakiwa kutoa adhabu mbadala kwa wahanga wa dawa za kulevya nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole 
nchini Dkt. Augustine Mrema (kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa 
habari (hawapo pichani) wakati alipokutana nao mapema hii leo jijini Dar
 es Salaam na kuwaeleza umuhimu vyombo vya usimamizi wa sheria nchini 
kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa wahanga wa matumizi ya dawa 
za kulevya nchini ikiwa ni sehemu ya barua yake kwa Rais John Magufuli.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole 
nchini Dkt. Augustine Mrema (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi 
wa habari (hawapo pichani) wakati alipokutana nao kuwaeleza umuhimu 
vyombo vya usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo 
cha nje kwa wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya nchini ikiwa ni 
sehemu ya barua yake kwa Rais John Magufuli, kulia ni Dkt. Bingwa wa 
Magonjwa ya Akili toka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Cassian 
Nyandindi na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bw. Vincent 
Tiganya.
Baadhi ya waandishi wa habari 
wakimsikiliza  Mwenyekiti wa Bodi ya Parole nchini Dkt. Augustine Mrema 
(hayupo pichani) wakati alipokutana na waandishi hao leo jijini Dar es 
Salaam kuwaeleza umuhimu vyombo vya usimamizi wa sheria nchini kutoa 
adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa wahanga wa matumizi ya dawa za 
kulevya nchini ikiwa ni sehemu ya barua yake kwa Rais John Magufuli.
Picha zote na Eliphace Marwa – Maelezo.
…………………………………………………………………………………….
Na Eliphace Marwa -MAELEZO -Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Bodi ya Taifa ya 
Misamaha kwa Wafungwa (Parole) Dkt. Augustine Mrema amevitaka vyombo vya
 usimamizi wa sheria nchini kutoa adhabu mbadala ya kifungo cha nje kwa 
wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya nchini. 
Hatua hiyo inaeelezwa itawezesha 
kuwapatia huduma bora za matibabu ambazo ni ngumu kuzipata pindi wawapo 
mahabusu au wakitumikia kifungo katika magereza.
Akizungumza na waandishi wa habari
 leo Jijini Dar es Salaam, Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha 
Tanzania Labour Party (TLP) alisema katika siku za hivi karibuni 
kumezuga tabia kwa baadhi ya askari polisi kuwageuza mtaji wahanga wa 
madawa ya kulevya.
“Natoa wito kwa Jeshi la Polisi 
kuacha mara moja tabia ya kuwabambikia kesi wahanga hawa na badala yake 
washughulike na wakubwa wa wauza madawa hayo ambao wapo katika jamii na 
wanafahamika na hata baadhi ya Polisi” alisema Dkt. Mrema
Aidha Mrema alisema idadi ya 
watumiaji wa madawa ya kulevya imekuwa ikiongezeka kila kukicha nchini 
hatua inayoisababisha Serikali kuwa mzigo mkubwa katika kuwahudumia 
ikilinganisha na mahitaji yaliyopo.
Katika barua yake aliyoiwasilisha 
kwa Rais, Dkt Mrema alisema wahanga hao wamekuwa wakikabiliwa na 
changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vituo vya tiba, kutengwa na 
kukamatwa mara kwa mara na polisi.
Kwa mujibu wa Mrema alisema ndani 
ya barua hiyo pia amemshauri Rais John Magufuli kuwasaidia wahanga hao 
kupata maeneo maalum ya mashamba kwa ajili ya kuendesha shughuli za 
kilimo ili makundi hayo yaweze kujiongezea kipato.
Dkt Mrema pia aliishauri Serikali 
kuwapa wahanga hao jukumu la kusafisha Jiji la Dar es Salaam na kuwa 
walinzi wa wachafuzi wa mazingira. Faini iliyopangwa na jiji ni Tsh. 
50,000, kati ya hizo nashauri tsh 20,000 wapewe wahanga hawa ili iwe 
kama motisha kwao” alisema Dkt Mrema.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa 
magonjwa ya akili kutoka hospitali ya taifa muhimbili, Dkt. Cassian 
Nyandindi jamii haina budi kubadili mtizamo kuhusu watumiaji wa madawa 
ya kulevya, kwa kuwa wahanga hao hawakupenda kuwa wategemezi katika 
matumizi ya madawa hayo.
Dkt. Nyandindi alisema hospitali 
hiyo kwa kwa sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kuwahudumia
 wahanga wa matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo uhaba wa watumishi 
pamoja na vituo vya kutolea huduma. 
Dkt. Mrema ameeleza kuwa vijana 
hawa walipokuwa wakituia dawa za kulevya walidhalilika katika jamii na 
kuonekana kama wanyama na kupelekea hata jamiii kuwatenga kutokana na 
vitendo vya uhalifu lakini baada ya kuanza matibabu wamebadilika kitabia
 na hata jamii imeanza kurudisha imani kwao.
Akielezea kero wanazokutana nazo 
Dkt. Mrema amesema kuwa wahanga wengi wamekuwa wakikamatwa na Polisi kwa
 kukutwa na kete moja au mbili na kufunguliwa mashtaka mahakamani.
“Nimetoa ushauri badala ya 
kuwapeleka magerezani wasioanza tiba bali wapelekwe hospitalini na 
waanzishiwe tiba ili kuwarejesha katika utu wao,” alisema Dkt. Mrema.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni