WIZARA YA AFYA YATOA UFAFANUZI UPUNGUFU WA CHANJO YA KICHAA CHA MBWA NA HOMA YA MANJANO.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mohamed Mohamed
akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya hatua iliyochukuliwa na
Serikali kuagiza na kusambaza dozi mbalimbali za chanjo kupitia mpango
Serikali wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chanjo uliojitokeza
nchini.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa
Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi kuhusu Chanjo ya
Homa ya Manjano na vitendo vya baadhi ya watumishi wa afya
wasiowaaminifu ambao hulipwa fedha ili waweze kuwatengenezea wasafiri
kadi za Chanjo ya Homa ya Manjano na kisha kuzitumia nje ya nchi jambo
ambalo kinyume cha sheria na hatari kwa usalama wa Afya zao.
Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo
wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.
Dafrosa Lyimo akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu mpango wa
utoaji wa chanjo zilizokuwa na upungufu zikiwemo za kifua Kikuu, Polio,
Surua na Lubela ambazo MSD wamekwisaha anza kuzisambaza.
Picha/Aron Msigwa – MAELEZO.
……………………………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
11/8/2016. Dar es salaam.
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
inatarajia kupokea dozi 14,000 za chanjo ya homa ya manjano mwanzoni mwa
mwezi Septemba, 2016 ili kutosheleza mahitaji ya wasafiri watakaohitaji
huduma hiyo kwa kipindi cha mwaka mzima.
Aidha, Wizara hiyo imekwisha nunua
dozi za chanjo ya Kifua Kikuu na Polio 739,700 na kuongeza kuwa dozi
zipatazo milioni 7 zimekwishaanza kusambazwa kwenye mikoa ya Morogoro,
Singida, Dodoma, Tabora na Kigoma.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar
es salaam Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mohamed Mohamed amesema kuwa uagizaji na
usambazaji wa dozi hizo ni mpango Serikali wa kukabiliana na changamoto
ya upungufu wa chanjo uliojitokeza nchini.
Akifafanua kuhusu kukosekana kwa
baadhi ya chanjo ikiwemo ya Homa ya Manjano amesema hali hiyo imetokana
na kutokea kwa mlipuko wa homa hiyo katika nchi za jirani ikiwemo Angola
jambo lililosababisha akiba ya chanjo hiyo dunia nzima kupelekwa kwenye
nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo kwa lengo la kuwachanja wananchi wote
ili kuzuia ugonjwa huo kusambaa.
Amesema kutokana na hali hiyo
akiba iliyokuwa imewekwa kwa ajili ya kuzigawia nchi nyingine hasa
matumizi kwa ajili ya wasafiri ilibidi ipelekwe katika maeneo yaliyokuwa
na upungufu wa dozi hizo kutokana na uharaka na uhitaji wa chanjo hizo.
Amesema wizara kwa kushirikiana na
Shirika la Afya Duniani (WHO) inatekeleza mradi wa majaribio wa
kutokomeza kichaa cha mbwa kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro,
Pwani na Dar es salaam ambayo sasa ina chanjo za kichaa cha mbwa.
Amebainisha kuwa jijini Dar es salaam chanjo hizo zinapatikana katika hospitali ya wilaya ya Temeke, Kituo cha Afya Magomeni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Huduma za Kinga wa Wizara hiyo Dk. Neema Rusimabayila akitoa ufafanuzi
kuhusu baadhi ya watoto waliokosa chanjo katika awamu tofauti amesema
kuwa wote waliokosa chanjo kuhakikisha kuwa wanamaliza chanjo zao kwa
mujibu wa idadi ya chanjo walizopangiwa pindi zitakapopatikana.
Ametoa wito kwa wataalam wa afya
wanaohusika na utoaji wa chanjo kuwapatia taarifa wazazi wenye watoto
ambao walihudhuria vituo vya afya kisha kukosa chanjo hizo, kuhakikisha
kuwa wanarudi katika vituo vya afya ili waweze kumalizia idadi ya chanjo
walizotakiwa kupata pindi zitakapofikishwa kwenye vituo vyao.
Kuhusu Mradi wa majaribio wa
kipindi cha miaka 5 wa chanjo ya kichaa cha mbwa wenye lengo la kuondoa
kichaa cha mbwa amesema kuwa unalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na
vifo vya watu vinavyotokana na kichaa cha mbwa.
Naye Meneja Mpango wa Taifa wa
Chanjo wa Wizara hiyo Dk. Dafrosa Lyimo akifafanua kuhusu mpango wa
utoaji wa chanjo zilizokuwa na upungufu hizo amesema kuwa mpaka sasa
utaratibu wa kupokea chanjo zaidi zikiwemo za kifua` Kikuu, Polio,
Surua na Lubela ambapo MSD wamekwisaha anza kuzisambaza.
Ametoa wito kwa wazazi wenye
watoto waliokosa chanjo kuwasiliana na vituo husika ili waweze kupangiwa
ratiba ya kupatiwa chanjo hizo kwenye vituo vya kutolea huduma vya
serikali ndani ya umri wa miaka 5.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni