MAKALA KUHUSU FALSAFA, DHANA NA UMUHIMU WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVUFalsafa ya Mwenge wa Uhuru
Historia
ya nchi yetu ni pana na ya kuvutia kwa namna ya pekee ukilinganisha na
nchi nyingi za Afrika na Duniani kote. Upekee huu unatokana na uwezo wa
kujenga hoja na uadilifu wa viongozi wetu, hasa mwasisi wa Taifa letu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipochaguliwa kuwa mjumbe kwenye
Baraza la kikoloni la kutunga Sheria (Tanganyika Legislative Council)
mwaka 1958.
Kwa
kuwa Mwalimu alikuwa na ndoto ya kuiona Tanganyika na Afrika iliyo huru,
mwaka 1958 katika hotuba yake ya kwanza alitamka maneno ya kifalsafa
kwa wajumbe na Spika wa Baraza la kikoloni la kutunga Sheria kwa kusema
“Sisi tunataka Uhuru wa Tanganyika, Mkitupatia tutauwasha Mwenge wa
Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje na
mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali
palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”.
Falsafa
hiyo ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni kiashiria kikubwa
kwa Waingereza kwamba watu wa Tanganyika wamechoka kutawaliwa. Siku
Tanganyika ilipopata Uhuru tarehe 09 Desemba, 1961. Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere aliuwasha Mwenge wa Uhuru na akamkabidhi Luteni
Alexander Ngwebe Nyirenda na kikosi cha Vijana wenzake wakaupeleka
Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro.
Mwalimu
wakati akitoa hotuba ya siku ya Uhuru; aliwatangazia Watanganyika,
Afrika na Dunia kwa ujumla kwa kusema
“Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na
kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu,
ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye
chuki na heshima mahali palipo jaa dharau”
Baada
ya Uhuru wa Tanganyika na kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza
walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi
imara ya kulijenga taifa huru la Tanganyika; kudumisha amani, upendo,
umoja, mshikamano na kuweka sera za kukabili maadui ujinga, umaskini na
maradhi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni