Serikali kuanza kupima utendaji kazi kwa Taasisi za Umma
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO – Dar es Salaam
Serikali imejipanga kuanzisha
mikataba ya utendaji kazi kwa Taasisi za Umma katika mwaka ujao wa fedha
kwa ajili ya kuhakikisha watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea.
Kauli hiyo imetolewa jana Jijini
Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki alipokuwa akifanya mahojiano
kwenye kipindi kinachorushwa na TBC1 cha ‘TUNATEKELEZA’ kinachoelezea
utekelezaji wa mipango na mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika
kipindi cha Uongozi wa Awamu ya Tano.
Mhe. Kairuki amesema kuwa kwa
kawaida Watumishi wa Umma hupimwa utendaji kazi wao kwa kujaza fomu za
wazi zijulikanazo kama ‘OPRAS’ lakini upimwaji huo hauonyeshi utendaji
wa Taasisi nzima, hivyo ili kufahamu mipango na malengo ya Taasisi ni
lazima kuwe na upimaji wa utendaji kazi wa Taasisi nzima.
“Sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi
wa Umma tumeona kuna haja ya kuwa na mikataba ya kupima utendaji kazi
wa Taasisi husika ,tumeshakamilisha maandalizi na kila kitu kikienda
salama mwaka ujao wa fedha tutaanza zoezi hili”, alisema Mhe. Kairuki.
Waziri huyo ameongeza kuwa zoezi
hilo limeshindikana kuanza mwaka huu wa fedha kwa kuwa bado maandalizi
yake hayajakamilika na kuongeza kuwa taasisi zote zinatakiwa kupewa
mafunzo kabla ya kusaini mikataba hiyo.
Amefafanua kuwa Serikali itaingia
makubaliano kwa taasisi husika kwa kufuata ngazi za uongozi kuanzia kwa
Mkuu wa Taasisi hadi kwa kiongozi wa juu kabisa wa Wizara husika.
Aidha, Mhe. Kairuki amewakumbusha
Watumishi wa Umma kuwa kuvujisha nyaraka za Serikali ni kosa la jinai
hivyo kila mtumishi anatakiwa kuzingatia kanuni za kudumu za Utumishi wa
Umma ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu na uwajibikaji wa hali
ya juu.
“Sheria ya Usalama wa Taifa na
Sheria inayosimamia masuala ya kumbukumbu za nyaraka Serikalini inasema
wazi kuwa ni kosa la jinai kuvujisha nyaraka za Serikali kwahiyo natumia
fursa hii kukemea mtu yeyote mwenye tabia hiyo kwa sababu hatua kali
zitachukuliwa dhidi yake”, alimalizia Mhe. Kairuki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni