Umoja wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania wapinga maandamano ya kuvunja amani
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), Cecilia Augustino
akifafanua jambo wakati alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam leo, kupinga maandamano ya UKUTA. Kulia ni Katibu wa umoja huo
Mwajuma Naty na Makamu Mwenyekiti Zaitun Hokororo.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), Zaitun Hokororo
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.Kulia ni
Mwenyekiti Cecilia Augustino, Katibu Mwajuma Naty na Mjumbe Ziada
Athumani.
……………………………………………………………………………..
Hussein Makame-MAELEZO
Umoja wa Wanawake Viongozi wa
Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), umepinga maandamano yasiyo na ukomo
yaliyotanganzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa
hayana tija kwa wananchi na Tifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa umoja huo Cecilia Augustino,
alisema maandamano hayo yanaashiria uvunjifu wa amani ambayo ni urithi
wa Taifa la Tanzania.
Alisema wamefikisha tamko lao kwa
Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi na kumtaka msajili
kutoacha chokochocko hizo ziendelee kwani zitasababisha kutoweka kwa
amani nchini.
“Sisi wanawake viongozi wa vyama
vya Siasa Tanzania tunapinga azimio la maandamano yasiyo na kikomo
yanayoandaliwa na chama cha Chadema, hakika maandamano hayo hayana tija
kwa wananchi na Taifa kwa ujumla” alisema Hokororo na kuongeza:
“Mheshimiwa Msajili, chokochocko
hizi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa zikiachwa tu bila ya
kukemewa tunaamini tunu yetu ya amani ambayo ni urithi wetu tulioachiwa
na waasisi wetu itatoweka”
Aliongeza kuwa hatma ya maandamano
hayo ni kuingia kwenye machafuko na hatimaye mauaji na mateso kwa
wanawake, watoto na walemavu, mambo ambayo hawatakubali yatokee.
Alibainisha kuwa wanawake viongozi
wa vyama vya siasa wanaamini kuwa siasa ni kushindana kwa hoja na si
uvunjifu wa sheria kwa njia ya maandamano yasiyo na tija kwa wananchi na
Taifa.
Aliliomba Baraza la Vyama vya
Siasa kuhakikisha linawajibika katika kulinda demokrasia, amani na
ustawi wa jamii nzima ya Watanzania.
Katika hatua nyingine, umoja huo
unaojumuisha wanawake viongozi wa vyama 22 vya siasa nchini, umeomba
kufanya kongamano la amani lenye lengo la kuhamasisha amani na utulivu
nchini.
Hivyo, Hokororo aliwaomba viongozi
wakuu wa nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu
wa Rais, Waziri Mkuu, wadau wa amani na mashirika binafsi kushirikiana
na umoja huo kufanikisha kongamano hilo.
“Hakika tunaumia wanasiasa
wanapokuwa chanzo cha migogoro na vurugu kwa Taifa letu.Hivyo tunamuomba
Rais wetu tunajua ni msikivu aweze kuona namna nzuri ya kutafuta
suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa” alisema Mwenyekiti Cecilia Hokororo.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi, tayari ameitisha Baraza la Vyama vya Siasa Agost 31,
mwaka huu ili kutoa fursa kwa pande vyama husika kukaa meza moja na
kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja
huo Ziada Athumani alisema wanaunga mkono hatua hiyo kwani ndio njia
muwafaka ya pande husika ili kufikia muwafaka kwa njia ya amani.
Katika mkutano huo na waandishi wa
habari, wanawake viongozi wa vyama vya siasa waliwakilishwa na wenzao
kutoka vyama vya Demokrasi Makini, ADA TADEA na Chama cha Umoja wa
Demokrasi ya Vyama Vingi (UMD).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni