NSSF yamuunga mkono Rais Magufuli, yatoa mkopo wa bil 4/- kwa kiwanda cha viuadudu Kibaha.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kulia) akikabidhi
mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2 na
laki 1 (zaidi ya Tsh bilioni nne) kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC) Dkt Samuel Nyantahe (wa tatu kushoto) ikiwa ni
mkopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwenye kiwanda cha kuzalisha
viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product Ltd
kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani wakati wa hafla fupi ya
makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye
Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati), Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi
Assumpta Mshana, (wa pili kulia) Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki
ya Azania, Bw Geofrey Dimoso (wa pili kushoto) na Kaimu Meneja Mkuu wa
kiwanda hicho Bw Samwel Mziray.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana pamoja na jopo la maofisa
kutoka NSSF, NDC, benki ya Azania na uongozi wa kiwanda cha kuzalisha
viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product kwa
pamoja wakimsiliza mmoja wa wataalam kutoka kiwanda hicho aliekuwa
akifafanua moja ya shughuli za kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
(kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya
jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kushoto) pamoja na viongozi wa NSSF
kwenye ziara hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
(kulia) akimpongeza mmoja wa wataalamu wazalendo waliopo kwenye kiwanda
hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
pamoja na jopo la viongozi kutoka NSSF, NDC, benki ya Azania na uongozi
wa kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha
Tanzania Biotech Product kwa pamoja wakimsiliza Kaimu Meneja Mkuu wa
kiwanda hicho Bw Samwel Mzirayaliekuwa akifafanua uwezo wa viuadudu
vinavyozalishwa na kiwanda hicho.
………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu,
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) limetoa mkopo wa dola za kimarekani mil. 2.1 (zaidi ya sh
bilioni nne) kwa kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi
vya mbu cha Tanzania Biotech Product Ltd kilichopo wilayani Kibaha,
mkoani Pwani ili kukiongezea uzalishaji wake, hatua inayotajwa kuwa ni
kuitikia wito wa Rais Dr John Magufuli wa kuifanyaTanzania kuwa nchi ya
viwanda.
Mbali na mkopo huo unaotolewa
kupitia benki ya Azania itayayosimamia urejeshwaji wake, pia shirika
hilo lipo kwenye mchakato wa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vipya na
vikubwa zaidi vya kutengezeza nguo, matairi pamoja na sukari hapa
nchini.
Akizungumza wilayani Kibaha
mwishoni mwa wiki wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mkopo huo kwa
Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linalomiliki kiwanda hicho,
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara alisema shirika lake lina
dhamira ya dhati katika kuwekeza kwenye viwanda nchini ili kuongeza
fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania.
“Pamoja na kuitikia wito wa Rais
Dr John Magufuli katika kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili
kuiongeza ajira hapa nchini lakini pia tunatarajia kupata faida kupitia
marejesho ya pesa hizi,’’ Alibainisha.
Akiwatoa hofu wanachama wa mfuko
huo na watanzania kwa ujumla kuhusu usalama wa pesa zao, Prof Kahyarara
alisema uamuzi wa shirika kuwekeza kwenye viwanda sio mgeni kwa kuwa
ulianza miaka ya nyuma ambapo shirika hilo liliwezesha viwanda vya
saruji Mbeya, Mkonge Tanga, Sukari Kagera na kiwanda cha nguo 21st Century cha Morogoro.
“Uwekezaji huo ulionyesha
mafanikio makubwa kwa wananchi wengi walipata ajira na shirika lilipata
faida iliyokusudiwa na kuboresha mafao ya wananchama. Tupo makini na
aina za uwekezaji na miongoni mwa kanuni tunazotumia katika uwezaji ni
suala la tija, faida, usalama na malengo ya mradi husika hususani katika
kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla,’’ alisema.
Akizungumza kwenye hafla
hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu
wenye Ulemavu) Mhe, Bi Jenista Mhagama mbali na kulipongeza shirika hilo
kwa kuunga mkono nia ya Rais na serikali kwa ujumla katika kuelekea
uchumi wa viwanda, alisema uwezeshaji wa kiwanda hicho umeongeza kasi
ya vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia tisini (90).
“Kiwanda hiki ni cha kipekee
barani Afrika na ufanisi wake utawanufaisha si tu watanzania bali
Waafrika kwa ujumla na kutuletea fedha za kigeni,’’ alisema.
Alisema uamuzi wa shirika hilo
kutoa mkopo huo kupitia benki ya Azania utaliwezesha shirika hilo kuwa
na msimamizi thabiti wa marejesho ya pesa za wanachama wa mfuko huo.
“Mwanzo kabisa kwenye uamuzi huu
niliomba kupata uhakika fedha za wanachama na nilipohakikishiwa kuwa
kuna benki itasimamia mkopo huu basi nikajua pesa za wanachama zipo
salama. Niendelee tena kuwaomba wahusika wote wawe makini kwenye pesa
hizi,’’ alisisitiza.
Alitoa wito kwa mifuko ya hifadhi
hapa nchini kuhakikisha inawekeza zaidi kwenye viwanda huku akiwataka
viongozi wa mashirika mbalimbali kuhakikisha wanalinda haki na maslahi
ya wafanyakazi wao likiwemo suala la kuwaunganisha wafanyakazi wao na
mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi
ya NDC Dkt Samuel Nyantahe alisema mkopo huo utakiwezesha kiwanda hicho
ambacho kimejengwa kwa kushirikiana na kampuni ya LABIOFAM SA ya nchini
Cuba kupanua uzalishaji wake na kuwa katika nafasi ya kutafuta soko
hadi nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa huduma za
sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso alisema benki yake
imejipanga kuhakikisha inasimamia urejeshwaji wa pesa hizo kwa mfuko wa
NSSF huku akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo kuwa pesa zao zipo
salama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni