MSEKWA:WATANZANIA WAACHE KUFUATA MKUMBO
| Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa | 
Na Fatma Salum na Sheila Simba, MAELEZO  
Spika
 wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa 
amewaasa watanzania kuacha kufuata mkumbo wa kisiasa badala yake watii 
mamlaka ili kuepuka kuvunja sheria na kuleta madhara kwao binafsi na 
taifa kwa ujumla.
Msekwa
 aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala 
mbalimbali kuhusu mwenendo wa siasa za hapa nchini na utendaji kazi wa 
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe 
Magufuli. Alieleza kuwa watu wengi wana hulka ya kufuata mkumbo kwenye 
mambo fulani bila ya kuchunguza na kufahamu ukweli wake kabla ya 
kushabikia.
“Ni
 hulka ya watanzania kushabikia mambo wasiyoyafahamu ilimradi tu 
yanawafurahisha masikioni   au machoni mwao kwani hata huko mitaani 
wanakimbilia ngoma bila ya kujua inatokea wapi au inaelekea wapi, hivyo 
nawasihi wajaribu kuwa makini na mbinu za siasa zinazotumiwa na baadhi 
ya vyama kwa kuwa nyingine zina madhara ndani yake.” Alisema Msekwa.
Akifafanua
 mwenendo wa siasa za hapa nchini, Mzee Msekwa alisema kuwa bado 
wanasiasa wengi hawafuati kanuni za ushindani wa kisiasa katika kutafuta
 madaraka badala yake wanatumia mbinu ambazo zinavunja sheria za nchi na
 hatimaye wanapambana na mamlaka.
“Ushindani
 wa kisiasa ni jambo la kawaida na linalokubalika ingawa ushindani huo 
ni lazima ufuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kufikia 
lengo, hivyo kubuni vitu ambavyo vinachochea utovu wa nidhamu na 
uvunjifu wa amani sio jambo zuri, ‘ alisisitiza.
Aidha,
 Msekwa alieleza kuwa utendaji wa Mhe. John Magufuli ni wa kuridhisha na
 wa aina yake kwa kuwa amekusudia kuleta mabadiliko chanya kwa 
watanzania na kuondoa mfumo wa utendaji kazi kwa mazoea jambo ambalo 
limesaidia kurudisha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.
Akizungumzia
 uzoefu wake katika masuala ya kuongoza Bunge, alieleza kuwa tofauti ya 
Bunge la zamani ni kwamba lilikuwa na nidhamu kubwa na linaheshimika 
lakini Bunge la sasa halina utii na hicho ndio chanzo cha malumbano 
yanayojitokeza mara kwa mara katika vikao vya Bunge.
Aliongeza
 kuwa tangu awali wapinzani kazi yao ni kuipinga Serikali iliyo 
madarakani lakini kwenye Bunge la uongozi wake walikuwa wakipinga kwa 
kutumia hoja na kufuata kanuni bila ya kudharau mamlaka ya Spika wala 
Serikali iliyoko madarakani.
“Kanuni
 zinatoa nafasi kwa mbunge asiyeridhika na maamuzi ya Spika kushitaki 
kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge, na kamati hiyo itasikiliza na kutoa 
uamuzi kama mahakama inavyosikiliza lakini wabunge wa sasa hawataki 
kutumia utaratibu bali hutumia mbinu za tofauti ili waweze kupata sifa 
ambazo hazina tija kwa wananchi waliowachagua,” alisema.
Msekwa
 pia amewaasa vyama vya upinzani kutumia mbinu nzuri katika kutafuta 
madaraka bila ya kuvunja sheria au kuhatarisha amani ya nchi kwani 
waliowachagua wanategemea zaidi matokeo ya kazi waliyoahidi kuwatumikia 
kuliko malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wao na taifa.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni