Maandamano ya UKUTA hayawezi kufanyika
Maandamano ya UKUTA hayawezekani kwani hii ni ndoto ya mchana na hayana msingi wowote wala tija kwa wahusika hata kwa Taifa.
Hayo yalisemwa na Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Benson Bana katika mahojiano maalum.
“Wanaotaka kuandamana
wanajidanganya na kuwalaghai wenzao kwani kufanya operesheni ni suala la
dola na si la mtu au kikundi cha watu, hivyo maandamano hayo
hayawezekani kabisa, alisema Prof. Bana.
Ameongeza kuwa wanaojiita UKUTA ni
kwamba Mhe. Rais John Pombe Magufuli amewanyima ajenda kwani utendaji
wake umezidi fahamu zao na kuwafanya waanze kutapatapa wasijue nini la
kufanya.
Prof. Bana amesema kama viongozi
wa UKUTA ni waungwana inabidi watamke wazi kuwa wametafakari na kuona
kuwa maandamano hayana maana hivyo wameamua kuyasitisha nchi nzima.
Kuhusu utendaji wa Serikali ya
Awamu ya Tano, Prof. Bana alisema ni Serikali yenye maamuzi ya uhakika
na inayowajali watu wote bila kujali itikadi zao za vyama, dini wala
makabila hivyo inabidi watanzania waipende na kuiheshimu.
“Rais Magufuli utendaji wake ni wa
kuigwa na viongozi wengi Duniani kwani anafanya maamuzi ya uhakika
ikiwemo kukuza uchumi kwa kukusanya kodi na kuziba mianya ya ubadhirifu
wa mali ya umma, alisema Prof. Bana.
Pamoja na kuwa Rais Magufuli
amekuwa madarakani kwa kipindi kifupi, viashiria vyote vinaonyesha kuwa
ni kiongozi imara na shupavu kutokana na mambo makubwa ambayo ameyafanya
kwa kipindi hiki kifupi. Katika kipindi hiki kumekuwepo na nidhamu
katika utumishi wa umma, kodi inakusanywa kwa kiwango kikubwa na elimu
ya msingi inatolewa bure kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala
inavyosema, alisema Prof. Bana.
Aidha, Prof Bana amesema kuwa
wanaomlaumu Mhe. Rais ni wale ambao hawajitambui na labda wanaona mianya
ya ubadhirifu anayoendelea kuiziba, wao wanakosa mapato, vinginevyo
Rais anafanya vizuri katika kuliongoza Taifa.
“Rais Magufuli yuko sahihi kwa
jinsi anavyosimamia vipaumbele vya Serikali ikiwemo elimu bure,
kukusanya kodi na kuzuia mianya ya rushwa pia dhamira ya kuifanya
Tanzania kuwa na uchumi wa viwanda, alisema Prof. Bana.
Prof. Bana ameelezwa kusikitishwa
kwake na watu wanaomkosea Rais heshima na kumwita “Dikteta
Uchwara.”Amesema watu hawa inabidi wazalendo wakemee kabisa vitendo vya
namna hii ambavyo ni utovu wa nidhamu kwa kiongozi.
Akizungumzia uamzi wa kuhamia
Dodoma, Prof. Bana alisema kuwa ni uamzi wa busara kutekeleza azma ya
Serikali ya miaka takribani arobaini iliyopita. Hivyo kuhamia Dodoma
kutaufanya mji huo kuendelea zaidi kimiundombinu na kiuchumi.
Aliongeza kuwa mikoa ya jirani
nayo itanufaika kiuchumi kwani itakuwa karibu na makao makuu ya nchi na
pia kuhama huko kutatoa fursa kwa Dar es Salaam kukua zaidi kibiashara.
Prof. Bana ameitofautisha Serikali
ya Awamu ya Tano na awamu nyingine nne zilizopita kwa kutokuwa na
kigugumizi katika kufanya maamuzi yake ikiwemo hii ya kuhamia Dodoma,
kuondoa wabadhirifu katika utumishi wa umma na kupunguza matumizi yasiyo
ya lazima na fedha hizo kutumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama
afya, elimu na miundombinu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni