WAZIRI MBARAWA AFUNGUA KOZI MPYA YA MAFUNZO YA WAKUFUNZI WA MARUBANI
Rubani Focus Mmbaga kutoka Chuo
cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), akitoa maelezo ya namna ndege
inavyoendeshwa kwa kutumia kifaa maalum cha mafunzo ya urubani
(simulator) kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani
uliofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendesha ndege kwa kutumia kifaa
maalum cha kufundishia marubani (simulator) kwenye chumba cha mafunzo
kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Mkuu wa chuo cha Taifa cha
Usafirishaji Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza na wadau wa sekta ya
usafiri wa anga (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi
wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa wadau wa sekta
ya usafiri wa anga (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mafunzo ya
wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.
wadau wa sekta ya usafiri wa anga
wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika
jijini Dar es salaam.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
…………………………………………………………………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amekitaka Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), kuhakikisha kinatoa marubani waliobobea katika
masuala ya usafirishaji wa anga na wenye uadilifu katika taaluma hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa kozi za Urubani Chuoni
hapo, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa Sekta ya anga ina changamoto ya
upungufu wa marubani pamoja na uadilifu kwenye sekta hiyo, hivyo
ameutaka uongozi wa chuo kutoa mafunzo ambayo yatabeba taaluma iliyo
bora na yenye uadilifu.
“Tunataka kuijenga Air Tanzania
mpya ambayo ilijengwa kwa misingi ya uadilifu, na serikali ipo tayari
kukijengea uwezo chuo hiki ili kitowe marubani waadilifu watakaoweza
kufufua shirikia letu la ndege”, amesema Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amefafanua kuwa
suala la uadilifu ni la muhimu, hivyo ameutaka uongozi wa Chuo na
wakufunzi wake kuwa mfano kwa kuonyesha uadilifu ili wanafunzi
watakaofuzu wawe na tija na uzalendo.
Aidha, amesema kuwa Serikali ina
mpango wa kukiongezea uwezo chuo kwani lengo ni kuzalisha wataalamu wa
usafiri wa anga ndani ya nchi na si kutegemea nchi nyingine.
“Tunataka marubani waweze kupata
mafunzo ndani ya Tanzania na ikitokea wameenda nje ya nchi basi iwe
nikwaajili ya mafunzo maalumu tu” amesisitiza Profesa Mbarawa.
Waziri Profesa Mbarawa amesema
kuwa kwa kutambua changamoto zilizopo kwenye sekta ya anga, Serikali
imejipanga kuboresha sekta hiyo kwa kuongeza idadi ya ndege za abiria
ambapo mbili zimekwisha nunuliwa na mbili nyingine zipo kwenye mchakato
wakununuliwa ili kuongeza ufanisi wa shirika la ndege nchini.
Amewataka watanzania kuiamini
Serikali yao kutokana na uamuzi wa ununuzi wa ndege mpya aina ya
Bombadiat Q400 kwani Tanzania si ya kwanza kuzitumia bali kuna nchi
nyingi zinazotumia ndege hizo ikiwemo Afrika ya kusini, Malawi, Rwanda,
Ethiopia na Austria.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho
Profesa Zacharia Mganilwa ameiomba serikali kuangalia jinsi ya kuongeza
mikopo kwa wanafunzi wanaochukua kozi hiyo kutokana na umuhimu wake
kwa jamii na Taifa kwa ujumla ili kuwezesha watanzania wengi kupata
fursa ya mafunzo hayo.
Aidha, uongozi wa chuo hicho
umeishukuru serikali kwa mpango wake wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya
usafiri wa anga ili iweze kukuza na kuleta ushindani wa usafiri huo
nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni