Mashindano ya Olimpiki 2016 nchini Brazil, wawakilishi wa Tanzania kupeperusha bendera. DSTV, Bodi ya Utalii wajitokeza kuwapa nguvu.
Zikiwa zimebaki siku chache kabla
kuanza rasmi michezo ya 31 ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro nchini
Brazil inayotarajiwa kuanza Ijumaa ya Agosti 4, 2016 katika mji wa Sao
Paulo na Rio De Jeneiro nchini Brazil wawakilishi wa Tanzania katika
michuano hiyo wamepata baraka zote kutoka kwa Serikali na kukabidhiwa
bendera ya Taifa kabla ya kwenda kuipeperusha nchini Brazil.
Akikabidhi bendera kwa timu hiyo
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia
Wambura aliwataka washiriki wanaokwenda kuiwakilisha nchi kwenye
mashindano ya Olimpiki mwaka huu huko Rio De Jeneiro nchini Brazil
kujituma na kuhakikisha wanafanya vizuri ili warudi na medali.
Mhe. Annastazia Wambura alisema
kuwa wanapokwenda kuiwakilisha waamini kuwa macho na masikio ya
watanzania wote yapo kwao kwahiyo wajitahidi kadri ya uwezo wao kuweza
kuhakikisha watakapokuwa wanarejea basi waje wakiwa wamevaa medali zao.
” Mnakwenda katika mashindano ya
Olimpiki macho yote ya watanzania yapo kwenu tunategemea mkiwa mnarudi
basi tutakuja kuwapokea mkiwa na medali zenu kifuani na hilo
linawezekana kama mtajituma mkiwa na ari ya ushindi”.
Aidha Katibu Mkuu wa Kamati ya
Olimpiki Tanzania , Filbert Bayi alisema kuwa kwa mwaka huu washiriki
wamekaa kambi katika sehemu tofauti nchini na wengine wakiwa nje ya nchi
na hilo limefanikisha kuweza kujifua vyema na kujiandaa ili kuweza
kurejesha ushindi nyumbani.
Akizungumzia mara baada ya
kukabidhiwa bendera Kocha wa timu ya kuogelea Bw. Alexandra Mwaipasi
alisema kuwa wachezaji wake wameiva kwani mwanzoni walikuwa na
changamoto ya kupata mabwawa yenye viwango vinavyoendana na mashindano
hayo ili kwa matayarisho aliyowapatia wachezaji wake anahakika watarudi
na medali.
Moja ya washiriki wa mchezo wa
kuogelea katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 Magdalena Mosha
alisema kuwa amejiandaa vizuri na anaamini kwa miaka aliyoshiriki kwenye
mashindano ya Olimpiki ya Beijing na London yamempa uelewa zaidi wa
nini anatakiwa kufanya na kuyafanyia kazi mazoezi aliyoyapata nchini
Australia ili kurudi na ushindi.
Naye mmoja wa wawakilishi katika
mchezo wa Judo, Adrew Thomas alisema amejiandaa vizuri kwa ajili ya
mashindano hayo na yuko tayari kuiwakilisha Tanzania na kuleta ushindi
na pia kuitangaza Tanzania katika michezo na utalii uliopo kwa
kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini.
Kwa upande wake Sara Ramadhani
ambaye ni mwakilishi mwanamke pekee katika mshindano hayo kwa wakimbiaji
wa Marathon alisema yuko vizuri kuipeperusha bendera ya taifa na
kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kushindana na kushinda medali hivyo
kuiletea sifa nchini.
Mmoja wa wadhamini wa safari
hiyo kampuni ya Multichoice Africa, imewataka washiriki hao kujituma
zaidi kwani watanzania wote watakuwa wanawaangalia kupitia chaneli zao
zinazopatikana kwenye kisimbuzi cha DSTV.
Katika mchango wao kwa
wawakilishi hao Kampuni ya ving’amuzi ya Dstv imetoa mchango wa
kuwakutanisha pamoja kwa kuandaa hafla ya kuwaaga wawakilishi hao ikiwa
ni moja ya kuwatia moyo waende kupambana na kushinda katika michezo
mbalimbali na kuliletea sifa taifa.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni
hiyo Mkurugenzi wa Multichoice Tanzania Maharage Chande alisema mwaka
huu mashindano yote yatakuwa yakioneshwa moja kwa moja kupitia channeli
za Super Sport na itawapa fursa watanzania kuwashuhudia wawakilishi wao
kwenye mashindano hayo makubwa duniani.
Bodi ya Utalii nayo haikuwa nyuma
kuwapa nguvu na morali wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya
Olimpiki kwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo na pia kutangaza
vivutio vilivyopo nchini kwa mataifa mbalimbali yanayoshiriki mashindano
hayo kwa kuwapatia vifurushi kwa ajili ya kusambaza ujumbe kuhusu
utalii wa Tanzania.
Akitoa nasaha zake kwa
wawakilishi hao Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TTB Bw. Godfrey
Tengeneza aliwaasa wawakilishi hao kujituma kwa bidii na kutangaza nchi
kupitia michezo na pia watumie fursa hiyo kutangaza vivutio vilivyopo
Tanzania kwa kueneza habari kuhusu utalii Tanzania.
“Mtakapokuwa huko mbali na
kushiriki katika michezo muitangaze nchi yetu kwa vivutio vilivyopo
nchini ili tuzidi kupata watalii wengi kutoka duniani kote”.
Timu ya Tanzania inayoenda
kushiriki mashindano ya 31 ya Olimpiki nchini Brazil inawakilishwa na
wachezaji saba ambao ni waogeleaji wawili Magdalena Mosha anayeenda kwa
mara ya tatu kwa upande wa wanawake huku Hilal Hilal akienda kwa mara
ya kwanza kwa upande wa wanaume na wote watakuwa ni waogeleaji kwa
umbali wa mita 50.
Wengine ni Fabian Joseph, Said
Juma Makula na Alphonce Felix Simbu watakaokimbia marathon kwa wanaume
na Sara Ramadhani ambaye ni mwanamke pekee anayeiwakilisha Tanzania
katika mbio za marathon.
Na kwa upande wa mchezo wa Judo Tanzania itawakilishwa na Adrew Thomas Mulugu katika uzito wa kilogramu 73.
Katika mashindano ya Olimpiki
mwaka huu takribani M yanatarajiwa kushindana katika michezo mbalimbali
huku Marekani ikiongoza kuwa na wachezaji wengi zaidi katika mashindano
hayo ikiwa na wachezaji 550 ikifuatiwa na Brazil iliyo na wachezaji 450
na China inayowakilishwa na wachezaji 380.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni