Ijumaa, 6 Mei 2016

FAHAMU JINSI WIVU UNAVYOATHIRI AFYA YA MWANADAMU



 Na Tinah Reuben

WIVU umesababisha watu wasiwe na amani sio tu kwenye mahusiano bali na maisha kwa ujumla.Umesababisha watu wawe na hasira, ghadhabu na uchungu wakati mwingi pengine hata kwa mambo yasiyokuwa na faida.
Wapo waliofikia kugombana na watu wasiohusika kwa sababu tu wanahisi kuingiliwa au kuzidiwa katika mambo wanayoyafanya wengi wakichukulia tabia hii ya wivu ni ya kawaida na haina madhara.
Labda neno hili ni la kawaida na kila mtu anaweza kulitafsiri kwa namna yake lakini katika safu hii ya afya wiki hii nitazungumzia maana ya wivu,kitu gani kinasababisha,madhara yake kwa ujumla na jinsi ya kukabiliana nao.
Wivu ni hali ya kuwa na mtazamo hasi juu ya kitu fulani,ni hisia ya kutokuridhika kuhusu fursa anayopata mtu mwingine iwe ni maendeleo,sifa,cheo,upendo au wakati mwingine kutamani kuona anapata matatizo ambayo hiyo kwao ndiyo huwa furaha.
Mtu mwenye wivu anapomuona ndugu,jamaa au mtu mwingine ana maisha mazuri au kuonyesha dalili za mafanikio au vinginevyo husumbuka katika nafsi yake wakati mwingine hushikwa na mawazo mpaka kumfanya ajisikie vibaya na hata kumchukia ukitafuta sababu hakuna ni kwamba amemzidi kwa kitu fulani.
Kwa kawaida hii hutokana na ushindani ambao huwa upo katika akili ya binadamu tangu akiwa mtoto mdogo.Licha ya dini kuelezea mambo hayo lakini pia mzazi ana jukumu la kumjengea mtoto tabia ya kuridhika na alicho nacho ili kumfanya asiwe na tamaa ambazo hupelekea wivu.Ukichunguza utagundua kuwa watu wa aina hii hujenga utengano baina yao na watu wanaowaonea wivu pamoja na kujenga chuki ambazo huzaa ugomvi ambao huanza taratibu na hatimaye kuwa mkubwa.
Utafiti unaonyesha kuwa watu wenye wasiwasi mwingi na mahitaji mengi kutoka kwa wapenzi wao,watoto, pamoja na wale wanaogombana mara kwa mara na jamaa zao, wamo katika hatari kubwa zaidi ya kuugua magonjwa ya moyo na kiharusi.Ingawa watafiti hao kutoka chuo kikuu cha Copenhagen waliweza kupata uhusiano uliopo kati ya vifo vya mapema na kugombana, na kuwa ugomvi uliongeza hatari ya vifo vya mapema mara tatu, hawakuweza kuelezea kikamilifu sababu haswa ya hali hiyo,na kusema vifo hivyo vya mapema hutokana na magonjwa anayopata mtu kisaikolojia.
Wivu ni hisia iliyotawala sana katika jamii zetu na huumiza watu wengi na kuleta athari kutoka maisha ya mtu mmoja mpaka jamii kwa ujumla bila kujali uwezo wao.

SABABU ZA WIVU
Kujiona unastahili zaidi;Unaweza kudhani kuwa kutokana na elimu yako, kazi yako au hata historia yako basi kuna mambo ambayo unastahili kuwa nayo.Tabia hii inaleta wivu pale unapoona mwenzako
amefanikiwa unaumia moyo na kupatwa na hasira kwa kuwa unaamini wewe ndiye unastahili kuliko wengine.
Binadamu wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kufanikiwa kutokana na juhudi zake acha kuendekeza dhana hiyo itakutesa na kujisababishia maradhi bure!.
Kutojiamini;Wivu unaweza kukuingia kama wewe mwenyewe hujiamini, maana kutokana na kutokujiamini hautakuwa tayari kufanya mambo makubwa na mabadiliko kwa hofu na utakapoona wengine wanafanya na kufanikiwa utafikiri labda wao wanapendelewa na ndipo utakapoanza kuwaonea wivu.
Kuishi au kuzungukwa na watu hasi(makundi);Ni kweli kila mtu ana uamuzi wa kuishi maisha anayoyataka au kuyachagua,kuzungukwa na watu hasi ni kuwa na marafiki,jamaa,ndugu au majirani wenye mitazamo duni(mawazo mgando)yaani hao ukiambatana nao kitu pekee wanachozungumzia ni umbea na majungu.Fanya chaguo sahihi.
Watu wa aina hiyo hakusifia hata kama unafanya mambo yanayokuumiza mwenyewe lakini watu makini hukueleza ukweli hata kama unaumiza.
Madhara yanayotokana na hisia za wivu ni pamoja na kudhoofika kiafya wili na akili,msongo wa mawazo,kupata maradhi ya moyo,kuishi maisha ya chuki na upweke,ngozi kujikunja na kuzeeka mapema,kukosa furaha na hata kusababisha kifo.

NAMNA YA KUUKABILI WIVU
Usijilinganishe na mtu mwingine;Jifunze kujikubali mwenyewe pamoja na maisha yako unayoishi.Pale unapoanza kujilinganisha na mtu mwingine na kuona maisha yake ndio mazuri hukujengea tamaa itakayokufanya uwe na mawazo mabaya na hasira na hapo ndipo wivu unapoanza.
Unatamani vitu ambavyo huna uwezo navyo na huenda ukivipata haviwezi kuwa na manufaa yeyote katika maisha yako,hivyo ulivyo ni bora hivyo ishi maisha yako.
Usiwadharau wengine;Hii ni tabia mbaya sana kuwadharau watu wengine kutokana na sababu zako binafsi na kuwaona hawawezi chochote bila kujua pengine hao unaowadharau wana maana zaidi kuliko wewe.
Kila mtu ana ubora na umuhimu wake kulingana na jinsi Mungu alivyoumba.Huna haki ya kumdharau mtu kutokana na maumbile,jinsia,rangi na hata ulemavu wake kwani hiyo hukujengea ubinafsi.
Jipende mwenyewe kwanza,Kama hujikubali na kujipenda mwenyewe itakuwa ngumu kuwapenda wengine na kuwakubali,watu walio makini na watulivu hawaruhusu hali ya wivu iwavamie na kuwatawala kwa kuwa wanaelewa madhara yake.
Kwa hiyo ni muhimu kujitambua na kufahamu nini unataka pamoja na kuweka juhudi zako katika hilo.Tumia muda,uelewa na akili zako kujifunza jinsi ya kukabiliana na kila hali ya maisha unayokutana nayo pamoja na kuishi kulingana na mazingira.
Kuwa na msimamo;Watu wenye msimamo siku zote hawaruhusu kutawaliwa na hisia zao,jifunze kusimamia yale yote unayodhani kuwa yana faida katika maisha yako bila uoga.Jiulize ni faida zipi umewahi kuzipata kutokana na kuendekeza wivu zaidi ya kujiumiza mwenyewe.
Wivu usikufanye ukapambana na watu ambao hawana lengo hilo na kujikuta ukipoteza muda tu huku ukiendelea kuhatarisha afya yako.Achana na hisia hizo za ubinafsi na roho mbaya,jiambie mwenyewe kuwa mimi ni mtu makini hivyo sitaki kuwa na wivu kwanza ni kitu gani usiwe kama mtoto mdogo.
Watoto wa miaka kati ya mwili na sita wanakuwa bado hawajajifunza kupambana na hisia hivyo hushindana kwa kila kitu,watoto wa umri huu huwa ni wepesi kujisikia kutishwa.Kwa mfano mzazi anapomsifia au kumbemba mtoto mwingine mtoto huyu huanza kulia kwa wivu na hasira kwa wenzake na kama na hata kumg'ata au kumkwaruza.
Kila tunachofanya na kuhangaika kwa njia mbalimbali ni kuwa na maisha mazuri ambayo sio nyumba na gari zuri pekee bali na kuwa na afya njema.Ni lazima kuishi vizuri ambayo sio kwa kula chakula bora pekee pia ni pamoja na kuepuka mambo madogomadogo tunayoyatharau na kuona ni ya kawaida bila kujua yanatuathiri afya zetu taratibu na tunapokuja kushtuka tayari tatizo limeshakua kubwa.Furahia maisha mazuri kwa kuwa na afya bora.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni