SERIKALI YAFAFANUA KUHUSU NDEGE NDOGO ZINAZOENDESHWA NA RUBANI MMOJA
SERIKALI imesema kuwa, hakuna 
kiwango kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 
kumi au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili.
Kauli hiyo imetolewa 
leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na 
Mawasiliano, Mhe. Eng. Edwin Ngonyani wakati akijibu swali la Mbunge wa 
Jimbo la Tambwe, Mhe. Khalifa Issa aliyetaka kujua kuhusu Sheria za nchi
 na za Kimataifa zisemavyo kuhusu ndege za namna hiyo kurushwa na rubani
 mmoja.
Eng. Ngonyani amesema
 kwamba, taratibu zinazoongoza fani ya kuendesha ndege nchini huongozwa 
na miongozo inayokubalika Kimataifa na ambayo imeridhiwa hapa nchini na 
Bunge.
Amefafanua kuwa, 
Katika taratibu hizo, kuna matakwa ya kisheria na kiufundi ambayo 
yakifuatwa yanawezesha kuwa na uwezekano mdogo sana wa kukumbwa na 
athari ya kiafya na kushindwa kumudu kuendesha ndege.
Ameeleza kuwa, 
Marubani hupimwa afya zao na madaktari bingwa kila muda maalum kulingana
 na umri kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 140 mpaka 177 ya The Civil
 Aviation (Personnel Licensing) Regulations, 2012.
“Serikali inaruhusu 
ndege kuendeshwa na rubani mmoja kwa kuzingatia taratibu hizo, Aidha, 
Kanuni 32(5) inasema kwamba ndege iliyoandikishwa katika Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania na kuruka kwa shughuli za kibiashara yenye uzito 
unaozidi kilo 5,700 itakuwa na marubani wasiopungua wawili”, alisema 
Eng. Ngonyani.
Pia amefafanua kuwa, 
shughuli za Usalama wa Anga nchini zinaongozwa na Sheria Namba 80 “Cvil 
Aviation Act. 80” na Kanuni zilizotengenezwa chini yake, ambapo urushaji
 wa ndege yenye abiria tisa au zaidi unaongozwa na Kanuni ziitwazo “The 
Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations, 2012” ambapo ndege 
inayotimiza vigezo vilivyowekwa kwenye vifungu (2), (3) na (4) vya 
Kanuni ya 32 kuwa na uzito wa chini ya kilo 5,700 inaruhusu kuendeshwa 
na rubani mmoja.
Ameongeza kuwa, 
katika viwango vinavyotolewa na Shirika la Kimataiaf la Usafiri wa Anga 
(ICAO) kwenye kiambatanisho namba 19, chini ya Mkataba wa Kimataifa wa 
Usafiri wa Anga (Chicago Convention) hakuna kiwango chochote 
kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 10 au zaidi
 ni sharti iendeshwe na marubani wawili.
“Pia hakuna hata 
mapendekezo ya kiutekelezaji kwenye suala hilo, na hata katika 
Kiambatanisho cha 6 chenye sehemu tatu kianchohusiana na uendeshaji wa 
ndege ambacho ndicho kinachozungumzia idadi ya marubani katika 
uendeshaji wa ndege hakina katazo hilo”, alisisitiza Eng. Ngonyani.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni