CCM ZANZIBAR YASISITIZA USHIRIKIANO KWA WAJUMBE WA BARAZAM LA WAWAKILISHI.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) 
kimewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  kuendelea 
 kushirikiana ili kuunda nguvu ya pamoja itakayosaidia kuharakisha  
maendeleo ya nchi kwa ufanisi zaidi.
Kimesema utendaji mzuri wa 
viongozi hao ndani ya Baraza hilo ndiyo utakaoweza kukirahisishia kazi 
Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa 2020, hali itakayojenga 
imani kwa wananchi kuirejesha tena CCM madarakati kutokana na utendaji 
mzuri wa viongozi hao.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa 
CCM Zanzibar, Nd. Vuai Ali Vuai  wakati akibadilishana mawazo na Katibu 
Mpya  wa Kamati ya Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Baraza la
 Wawakilishi Zanzibar (Mnadhimu) huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini 
hapa.
Nd. Vuai alimpongeza kiongozi 
huyo kwa kuaminiwa na Wajumbe wa Baraza hilo na kumchagua kuwa Mnadhimu 
wa Wawakilishi wote wa CCM ndani ya Chombo hicho cha kutunga sheria za 
nchi.
Alisema kuchaguliwa kwa Mnadhimu 
huyo pamoja na msadizi wake kutasaidia kuongeza ufanisi wa kusimamia 
vyema shughuli za baraza la wawakilishi ili ziende sambamba na mahitaji 
ya wananchi majimboni.
Alieleza kwamba mbali na viongozi
 hao kuwa na jukumu la kuandaa miswaada, kutunga sheria na kupitisha 
Bajeti za nchi bado wana wajibu wa kusimamia kwa vitendo ilani ya 
Uchaguzi ya CCM ya 2015/2020 pamoja na kulinda maslahi ya Chama hicho.
“Njia pekee ya kuepuka migongano 
na mivutano isiyokuwa ya lazima ndani ya Baraza la Wawakilishi ni lazima
 kila mara mkumbushane kufuata Kanuni na taratibu zilizopo ndani ya 
Chombo chenu.
Pia nyinyi ni kioo cha Wananchi 
waliokuchagueni kwa kura nyingi hivyo ni lazima muwawakilishe vyema  na 
kuwa mifano mizuri ndani ya jamii kwani kufanya hivyo kutaongeza hamasa 
na ari ya watu wengi kuendelea kuiamini CCM.”,  alisisitiza Vuai na 
kuongeza kwamba  Uchaguzi umekwisha na kilichobaki kwa sasa ni kila 
kiongozi kufanya kazi za kuiletea nchi maendeleo endelevu.
Aidha  Aliwataka Wajumbe wa 
Baraza la hilo kuwa na msimamo imara na kutokubali kuondoshwa katika 
Malengo kwani kuna njama na mikakati michafu inayofanywa na Viongozi wa 
CUF Zanzibar wenye nia ya kuharibu Haiba ya Chama na Serikali kwa 
ujumla.
“Juzi nimesoma katika baadhi ya 
 magazeti kwamba CUF wana mipango ya kuishtaki serikali katika Mahakama 
za Kimataifa na wamezindua kitambu cha Ripoti ya Haki za Binadamu, hizo 
zote ni njama za siasa zilizopitwa na wakati za kutaka kukuondosheni 
katika malengo yenu na msikubali kuyumbishwa.”, alisema Vuai na kuwataka
 wawakilishi wasihofu juu ya Propaganda za CUF .
Aliahidi kuendelea kutoa 
ushirikiano kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati wote 
watakapohitaji ushauri na  mawazo katika shughuli mbali mbali za Chama 
na Serikali .
Mapema akizungumza  Katibu wa 
Kamati ya Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Baraza la 
Wawakilishi Zanzibar(Mnadhimu), Ali Salum Haji alisema lengo la kikao 
hicho ni kujitambulisha kwa CCM na kupata nasaha, mawazo na ushauri 
mbali mbali wa kiutendaji kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu huyo ili waweze 
kuufanyia kazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Salum alieleza kwamba wana nia ya
 kuhakikisha ndani ya miaka mitano Bazara hilo linakuwa na mabadiliko 
makubwa yatakayopelekea  wajumbe wake sio tu kufanya kazi za vikao bali 
wafanye utafti na kutembelea majimboni ili kubaini changamoto 
zinazowakabili wananchi kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Naye Katibu Mndhimu Msaidizi, 
Nassor Salim Jazira, aliahidi kuzifanyia kazi nasaha na ushauri 
uliotolewa na Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai ili waweze kupiga hatua 
kubwa ya maendeleo katika majimbo na Baraza hilo.
Alisema changamoto na vikwazo vya
 kisiasa vinavyotengenezwa na CUF toka kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 
Marudio havitoweza kupunguza kasi ya mabadiliko ya kimaendeleo 
yanayofanywa na Wajumbe wa Baraza, viongozi wa  Chama  na serikali kwa 
ujumla.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni