MKUU WA WILAYA WETE PEMBA ALAANI VITENDO VYA HUJUMA MALI ZA WANANCHI KWA MISINGI YA KISIASA
SERIKALI ya Wilaya ya Wete Mkoa
wa Kaskazini Pemba imelaani vikali vitendo vya hujuma vinavyofanywa
na baadhi ya wananchi kwa kuhujumu mali za wengine kwa misingi ya
kisiasa .
Akizungumza kwa nyakati tofauti
baada ya kutembelea maeneo yaliyohujumiwa , Mkuu wa Wilaya ya Wete
Rashid Hadid Rashid amevitaka vyombo vya ulinzi kuhakikisha wanaohusika
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria .
Amesema serikali haitavifumbia
macho vitendo hivyo ambavyo vinaweza kusababisha kutoweka kwa amani na
utulivu uliopo hapa nchini .
Maeneo ambayo yamehujumiwa ni
pamoja na bonde la Chwangayo na Mburani Shehia ya Mtambwe kaskazini
pamoja na Shehia ya Pembani ambapo wakulima wamepata hasara kubwa
kutokana na hujuma hizo.
“Serikali ya Wilaya inakilaani
vikali kitendo hichi cha kuhujumu mali za wananchi kutokana na misingi
ya kisiasa , tunaahidi kuwasaka wahusika wote na tutawafikisha
mahakamani ”alieza Mkuu wa Wilaya .
Katika bonde hilo jumla ya
mikarafuu 16 ya daraja la pili ambayo ilikuwa tayari kuzaa pamopja na
nusu ya shamba la muhogo limehujumiwa na watu wasiojulikana.
Mmoja wa wakulima katika bonde
hilo Bakar Mwitani Sheha amesema kuwa uharibifu katika shamba lake
ameubaini baada ya kufika katika aneo hilo kwa ajili ya kupata mahitaji
ya chakula.
Alisema baada ya kubaini hali
hiyo , alitoa taarifa Ofisi ya sheha , Ofisi ya Wilaya pamoja na kutoa
taarifa katika vyombo vya ulinzi kwa hatua zaidi .
Maeneo mengine ni shamba la
mwakilishi wa jimbo la Mtambwe Bi Khadija Omar Kibano na Saleh Khamis
Ahmed ambao mashamba yao ya mpunga yamefyekwa pamoja na Said Khamis
Mohammed na Mariam Suleiman Makame walioharibiwa vipando vya mihogo ,
migomba , viazi , kubomolea nyumba yake pamoja na kuibwa mali ghafi
katika kiwanda cha uchongaji huko Pembeni
Naye Said Khamis Mohamed wa
Shehia ya Pembeni anayemiliki kiwanda cha kuchonga ambaye amebomolewa
baadhi ya kuta za nyumba yake , kung’olewa vipando katika Shamba lake
pamoja na kuchukuliwa samani (funiture) zake alisema vitendo hivyo
vimeathiri biashara yake .
Alisema kwamba tukio hilo
lilitokea juzi majira ya saa nane za usiku baada ya kutoka tangazo
kupitia mskitini lililowataka wananchi wote wa Shehia hiyo kukutana , na
baada ya hapo kundi la watu walivamia na kutekeleza hujuma hizo .
“Nikiwa nyumbani nilisikia tangazo likiwataka wananhi wote wa
Shehia kukutana sokoni , na baada ya muda nilivamiwa na kundi la watu na
kuanza kuchuma machungwa na kisha kuutaka mchungwa , kuvunja baadhi ya
kuta katika nyumba yangu pamoja na kung’owa vipando katika shamba langu
”alifahamisha.
Akitoa tathmini ya hasara iliyotokea katika maeneo hayo , Afisa
maendeleo ya Kilimo Wilaya ya Wete Makame Hamas Said alisema ni
shilingi milioni 7,439,500 /= .
Hadi sasa hakuna mwananchi
aliyekamatwa na vyombo vya ulinzi akihusishwa na vitendo hivyo ambapo
jeshi la Polisi limeahidi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya mikono ya
sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni