RC aitaka NHIF kuwa wabunifu ili kuongeza wanachama
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Saidi
 Meck Sadik ametoa rai kwa watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya 
(NHIF) kubuni mbinu mpya za kuwahudumia wanachama wao ili kuhamasisha 
watanzania wengi kujiunga na mfuko huo.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa 
Wilaya wa Siha Dkt. Charles Mlingwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa alipokuwa 
akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa mfuko huo uliofanyika 
Mkoani humo.
Mhe. Meck Sadik amesema kuwa 
Baraza la wafanyakazi ndiyo chombo sahihi cha uwakilishi wa sauti za 
watumishi katika kupanga malengo ya Taasisi pia ni chombo cha kutatua 
migogoro ya kikazi na hivyo kumaliza mapema tofauti zinazojitokeza 
katika sehemu za kazi kabla hazijaathiri utendaji. 
“Kutokana na umuhimu wa huduma 
zenu kwa umma, Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wenu linatakiwa lichukue 
sura mpya na kuwa ni mahali pa ubunifu na kisima cha kuibua mbinu mpya 
za kuwahudumia vizuri wanachama wenu na kujua namna gani mtaendelea 
kuwavutia Watanzania wengi zaidi kujiunga na Mfuko”,alisema Meck Sadik. 
Mhe. Meck Sadik ameongeza kuwa 
anawapongeza kwa ubunifu wao wa kubuni mipango mbalimbali ya uchangiaji 
inayolenga kuwafikia watanzania wa makundi mbalimbali kulingana na hali 
zao za vipato na uwezo wao wa kuchangia.
“Hali halisi ya uchumi wa 
watanzania mnaifahamu, siyo watu wengi wenye uwezo wa kugharamia 
matibabu kwa fedha taslimu hivyo, huduma za matibabu kupitia Mfuko huu 
ni ukombozi mkubwa kwa kundi kubwa la watanzania”, alisema Meck Sadik.
Aidha, Mhe. Meck Sadik 
amewakumbusha  wajumbe wa Baraza hilo kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya 
wafanyakazi na uongozi wa Mfuko kwa hiyo, wana wajibu wa kuyaelewa 
malengo ya Taisisi yao kiutendaji na kuyawasilisha kwa wafanyazi wenzao 
wakiwa kama wamiliki wa kile walichokubaliana na uongozi kuwa ndiyo dira
 na mwelekeo wa taasisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi
 Mkuu wa NHIF, Bernald Konga amesema kuwa mfuko huo utaendelea 
kushirikiana na Serikali, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, 
Jinsia, Wazee na Watoto ili kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la 
upungufu wa dawa nchini.
“Tunajua kuwa upungufu wa dawa 
katika vituo vya matibabu umekuwa ni mojawapo ya kero kubwa katika sekta
 ya afya. Ili kuondokana na kero hiyo, Mfuko umeanza kuchukua hatua 
mbalimbali za kukabiliana na upungufu huo kwa kuanzisha mpango maalumu 
wa kutoa mikopo ya dawa kwa watoa huduma waliosajiliwa ili kuhakikisha 
kuwa wanachama wetu na watanzania kwa ujumla wanapata dawa kila 
wanapokwenda kupata huduma za matibabu”,alisema Konga.
Chimbuko la Mabaraza ya 
Wafanyakazi linatokana na Agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 lililoagiza 
kuwa mahali popote penye wafanyakazi wa kudumu kumi na kuendelea 
panatakiwa pawe na chombo cha kuwawakilisha.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni