TAMASHA LA MAJIMAJI SELEBUKA KILA KITU KWENYE MSTARI, WAANDAAJI WAZUNGUMZIA MAANDALIZI
Maandalizi
ya tamasha la Majimaji Selebuka ambalo kawaida hufanyika mjini Songea
kila mwaka yamepamba moto na waandaaji wamesema kila kitu kinakwenda
kwenye msitari.
Tamasha
la Majimaji Selebuka linatarajia kuanza kutimua vumbi Mei 28 mpaka Juni
4, mwaka huu mkoani Ruvuma kwa kushirikisha michezo mbalimbali na
maonyesho ya biashara za wajasiriamali.
Tamasha
hilo linaandaliwa na kampuni binafsi ya Tanzania ya Mwandi
ikishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Songea Mississippi
(So-Mi) ambalo linahusika na mambo ya maendeleo ya jamii kwa wanasongea
kwa ushirikiano kati ya Songea Tanzania na Jimbo la Mississippi,
Marekani. Tamasha hilo lilianzishwa 2008.
Mratibu
wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura, amesema kuwa hii ni mara ya pili
kufanyika kwa tamasha hilo ambapo kwa mwaka huu litahusisha zaidi mambo
sita kwa muda wa siku saba huku lengo kubwa likiwa ni kuinua vipaji na
fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.
Rwezaura
alisema kuwa tamasha hilo ambalo litafunguliwa kwa mashindano ya mbio
za nyika (marathon) katika siku ya ufunguzi huku siku ya mwisho
likihitimishwa kwa mchezo wa mbio za baiskeli ambapo washindi wake
watapata nafasi ya kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mafunzo ya mbio za
kimataifa.
“Tunafanya
tamasha hili kwa mwaka wa pili malengo yakiwa ni kuibua vipaji na
kuviendeleza kupitia michezo ya mbio za nyika, kuanzia Kilomita 24, 21,
10, 5 mbio za kujifurahisha, pia mbio za mchezo wa baiskeli ambazo
tunaamini kwa mwaka huu ni za aina yake kwa sababu tunategemea kupata
washiriki kutoka nje ya nchi kama Rwanda.
“Lakini
lengo lingine ni kuibua na kutambua fursa za kiuchumi hasa kwa
wajasiriamali wa Mkoa wa Ruvuma kupitia maonyesho ya shughuli za
wajasiriamali pamoja na biashara katika viwanja vya makumbusho ya Vita
vya Majimaji.
"Pia
tamasha linalenga kuendeleza elimu kwa kufanya mdahalo wa shule za
sekondari kupitia wanafunzi wa shule mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa
wa Ruvuma na kuibua fursa za kitalii,” alisema Rwezaura.
Ada
ya ushiriki wa tamasha hilo, kwa mbio za nyika kilomita 42 ni Sh
10,000, kilomita 21 Sh 5,000, kilomita 10 Sh 3,000, kilomita 5 ni bure.
Kwa
upande wa mbio za baiskeli kilomita 50 Sh 10,000, ngoma za asili kwa
kila kikundi ni Sh 10,000 huku maonyesho ya ujasiriamali kwa kila
kikundi ni Sh 50,000 na kwa mtu mmoja ni Sh 10,000.
Picha kwa msaada wa SalehJembe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni