SERIKALI KUTOA MAFUNZO MAALUM YA ELIMU YA FEDHA KWA WANANCHI
By Newsroom on May 20, 2016
Wizara ya Fedha na Mipango
imesema kuwa iko tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa
wananchi wote wakiwemo wakinamama kuhusu ili kuleta uelewa mpana wa
upatikanaji wa huduma za fedha na taratibu zinazohusu mikopo.
Kauli hiyo imetolewa leo mijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kachwamba Kajaji
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Anna Lupembe
aliyetaka kujua mipango ya Serikali ya kupeleka huduma za kibenki
vijijini ili wanawake waweze kupata mikopo.
Aidha, alisema kuwa Wizara ya
Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imehakikisha kuwa
huduma za kibenki zinawafikia wananchi wengi ili kurahisisha shughuli
zao mbalimbali za kiuchumi katika maeneo ya mjini na vijiji.
Alisema kuwa baadhi ya Benki
zimeanzisha huduma za Kibenki kupitia mawakala, na huduma za kifedha
kupitia simu za mikononi ambazo zimewasaidia wananchi kwenye sehemu
ambako hakuna matawi ya Benki.
Mhe. Dkt.Kajaji aliongeza kuwa
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu inaendelea kuweka
mazingira wezeshi ili kusaidia nguvu za wananchi na sekta binafsi
kuanzisha benki au taasisi za fedha.
Alitoa wito kwa wananchi
kutumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini
kuzishawishi Benki kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo yao.
Mhe. Dkt.Kajaji alisema kuwa
Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushawishi Benki nchini kupanua
shughuli zao ili ziwafikie wananchi wengi hasa wale wa vijijini wakiwemo
akina mama.
Aidha, Naibu Waziri huyo
alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na BOT iko tayari kutoa mafunzo
maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo wakinamama kuhusu
utumiaji wa huduma za kifedha ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa
huduma za fedha na mikopo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni