SERIKALI KUJENGA NYUMBA 9500 KWA AJILI YA ASKARI MAGEREZA
Serikali 
kupitia jeshi la Magereza imesaini Mkataba na Kampuni ya Poly 
Technologies ya China kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya 
Magereza nchini.
Hayo yamesemwa 
na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni 
wakati akijibu swali kuhusu kuboresha makazi ya askari lililoulizwa na 
Mhe. Devota Minja (Mb) leo bungeni mjini Dodoma.
Mhe. Masauni 
alibainisha kuwa  kupitia mkataba huo Serikali itapunguza kwa kiasi 
kikubwa changamoto iliyopo ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya askari wa 
jeshi hilo ambapo mahitaji kwa sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni 
nyumba 4,221 hivyo kupelekea upungufu wa nyumba 10,279.
“Serikali 
inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na 
Polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi, hivyo katika 
kukabiliana na tatizo hili Serikali imeendelea kuzifanyia ukarabati 
mkubwa baadhi ya nyumba na pia kujenga nyumba mpya”. Alisema Masauni.
Mhe. Masauni 
alifafanua  kuwa mgawanyo wa ujenzi wa nyumba hizo mpya ni Makao Makuu 
ya Magereza nyumba 472, Arusha nyumba 377, Dar es Salaam nyumba 952, 
Dodoma 356, Kagera 364, Kigoma 272, Kilimanjaro 390, Lindi 233, Manyara 
206, Mara 378, Mbeya 622, Iringa 336, Morogoro 669, Mtwara 215, Mwanza 
398, Pwani 384, Rukwa 358, Ruvuma 320, Shinyanga 337, Singida 299, 
Tabora 408, Tanga 382, KMKGM Dar es Salaam 219, Chuo cha Ukonga 115, 
Chuo cha Kiwira 183, Chuo cha Ruanda 62, Chuo KPF 27, Bohari Kuu 82 na 
Bwawani nyumba 84.
Aidha, Mhe. 
Masauni aliongeza kuwa kwa upande wa Jeshi la Polisi, Serikali 
inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na 
Zanzibar zitakazosaidia kupunguza tatizo la makazi kwa askari wa jeshi 
hilo.
Mhe. Masauni 
alilieleza bunge kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa
 nyumba kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, 
Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri
 hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni