Wadaiwa 21,721 wajitokeza HESLB kurejesha mikopo
Baadhi wa waandishi wa habari wakifuatiliaa mkutano huo.
Jumla ya wadaiwa wapya 21,721 wa 
mikopo ya elimu ya juu wamejitokeza ili kuanza kulipa madeni yao 
kufuatia agizo la siku 60 lililotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
 Elimu ya Juu (HESLB) mnamo Machi 14 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa 
Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu 
(HESLB) Bw. Robert Kibona wakati akizungumza na waandishi wa habari leo 
jijini Dar es Salaam kuhusu tathmini ya agizo lililotolewa  na bodi hiyo
 kwa wanufaika wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.
Bw. Kibona alifafanua kuwa jumla 
ya Shilingi bilioni 151.5 zinatarajiwa kurejeshwa na wadaiwa hao ambao 
walikopeshwa ili kuwawezesha kupata elimu yao ya juu katika vyuo 
mbalimbali ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 1994.
“Lengo la agizo lilikuwa ni 
kuhahakisha madeni yote yaliyoiva yanakusanywa ili kuongeza uwezo wa 
kukopesha watanzania wengi zaidi na agizo hili limeisha Mei 13 mwaka 
huu.” alisema Bw. Kibona
Kwa mujibu wa Bw. Kibona, kati ya
 wadaiwa waliopatikana, wadaiwa 19,528 walipatikana baada ya Bodi 
kuchambua taarifa za waajiriwa zilizowasilishwa na waajiiri na wadaiwa 
wengine wapatao 2,007 walijitokeza kwa hiari.
“Waajiri wana wajibu wa kisheria 
wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao, baadhi yao walifanya hivyo 
katika siku hizo sitini na tukawabaini wadaiwa hao, tunawapongeza 
waajiri kwa ushirikiano walioutoa na wanufaika wote waliojitokeza kwa 
hiari” alisema Bw. Kibona.
 Aidha Bw. Kibona aliongeza kuwa 
Bodi imeongeza siku 30 za ziada kuanzia Mei 20, 2016 kwa wadaiwa 
waliobaki kujitokeza na uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha 
kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri na wanufaika wanaoendelea kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi 
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas 
Mwaisobwa alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji wa madeni kwa mwezi 
kinatarajiwa kuongezeka kutoka shilingi bilioni 2.7 zinazokusanywa hivi 
sasa na kufikia shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni 2016.
Katika kipindi cha mwaka 
1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kimetolewa kwa 
wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hivi 
sasa ambao kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale watakapomaliza au 
kusitisha masomo yao.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni