RAIS FIFA GIANNI INFANTINO AIPONGEZA YOUNG AFRICANS
Rais
wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino,
ameipongeza timu ya soka Young Africans ya Dar es Salaam, kutwaa ubingwa
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.
Young Africans imetwaa ubingwa huo
kwa msimu wa pili mfululizo, lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza
kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.
Katika salamu zake, kupitia barua
yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Jamal Emil Malinzi, Infantino ameelezea ubingwa wa Young Africans kwamba
umetokana na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha,
wachezaji pamoja na mashabiki.
“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania.
Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Young Africans na timu nzima
isiyoshindika kwa mafanikio haya makubwa. Taji la Young Africans ni
matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya Young Africans,” amesema Infantino
katika barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosema: Salamu za
Pongezi kwa Young Africans.
Amesema pongezi zake ziende kwa
uongozi wa klabu, makocha na benchi nzima la ufundi, wachezaji,
madaktari pamoja na mashabiki wote wa Young Africans.
“Kwa niaba ya familia ya soka,
napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Young Africans na Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) kwa jinsi mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa
jamii ya michezo,” alisema Infantino katika barua hiyo iliyotua TFF Mei
21, mwaka huu.
Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi
alikwisha kuipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji
24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya
Utendaji na kwa sasa wanasubiri zawadi ya fedha Sh 81,345,723.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni