TAARIFA YA MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI ILIYOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU
Tumefarijika kuona takwimu za
wiki iliyopita kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei 2016 zinazoonyesha kuwa,
kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua kwa asilimia 49 (karibu nusu
ya wagonjwa), ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 108, na
hakuna aliyepoteza maisha, ikilinganishwa na wagonjwa wapya 212
walioripotiwa wiki iliyotangulia ya Mei 9 hadi 15.
Mikoa ambayo imeripoti wagonjwa
wiki hii ni Morogoro (47), Manyara(16), Lindi (14), Mara (11) Dar es
Salaam (9), Pwani (6), Kagera (2), Kilimanjaro (2) na Iringa (1).
Halmashauri zilizoongoza kutoa
wagonjwa wengi ni Kilosa (27), Mvomero (15), Kilwa (14), Tarime Mjini
(11), Babati Vijijini (10), Kinondoni (9), Babati Mjini (5), Morogoro
Mjini (5), Kibaha Mjini (4), Bukoba Mjini (2), Chalinze (2), Same (2),
Iringa Mjini (1) na Mbulu (1).
Katika wiki iliyopita, mikoa
ambayo haikuwa na wagonjwa wa kipindupindu ni Kigoma, Dodoma, Mwanza,
Geita, Singida, Shinyanga, Arusha, Tanga, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya,
Simiyu na Mtwara. Na mikoa ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa wa
kipindupindu tangu mlipuko uanze ni Ruvuma na Njombe
Kupungua kwa idadi ya wagonjwa
kusirudishe nyuma juhudi za kuuzuia ugonjwa huu, bali tunatakiwa
kuzidisha jitihada ili tuweze kuuondoa, tusiwe na wagonjwa kabisa. Ni
vema kuchukua tahadhari zaidi, hasa katika msimu wa masika, ambapo kuna
uwezekano mkubwa wa maji ya mvua kusambaza vimelea vya ugonjwa huu.
Tuendelee kuzuia maambukizi, na pia kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa
kila siku, hata kama hakuna wagonjwa, na kusimamia kikamilifu hatua
mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo
Wizara inaendelea kutoa rai kwa
wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira.
Aidha Wizara inatoa elimu ya afya kwa njia ya kupiga simu kupitia namba
117 na kwa njia ya kutuma ujumbe wenye neno KIPINDUPINDU kwenda 15774.
Huduma hizi zinatolewa bila malipo kupitia mitandao yote.
Napenda kusisitiza tena kwamba
ni marufuku kwa watu kutitirisha maji taka ovyo, hasa
katika kipindi hiki cha mvua na mamlaka husika zinatakiwa kuchukua
hatua za kisheria kwa wale wote watakaokiuka agizo hili. Aidha
tunawasihi viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, kata
na tarafa kusimamia kikamilifu suala hili. Wizara inasisitiza kwamba
kila jitihada zifanyike kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii yote ya
Watanzania inatumia maji safi na salama. Hii ni pamoja na kuzingatia
taratibu za kutibu maji ya kunywa katika ngazi ya kaya.
Tunaendelea kuisihi jamii
kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia
yafuatayo:
- Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.
- Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
- Mamlaka za maji zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
- Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
- Kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa au kutibiwa kwa dawa. Na hapa napenda kusisitiza kwa wananchi wanaokaa kandokando ya Mto Pangani, kuwa maji ya mto huo si salama, yameingia vimelea vya kipindupindu na kumetokea wagonjwa wengi katika eneo hilo. Ni muhimu sana kuyachemsha au kuyatibu kwa dawa maji hayo kabla ya kuyatumia nyumbani.
- Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
- Kuzingatia matumizi sahihi ya ORS kwa wagonjwa walioanza kuonesha dalili ili kupunguza athari za ugonjwa.
- Watumishi wa afya kutoa takwimu sahihi na kamili za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa
wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika juhudi za
kutokomeza kipindupindu. Aidha, inawapongeza na kuwashukuru wadau wote
kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na katika kusimamia
kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara ili kuutokomeza ugonjwa huu,
wakiwemo wataalamu wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa,
Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na
wananchi kwa ujumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni