WAZIRI MKUU KUHUDHURIA MKUTANO WA ADB ZAMBIA
WAZIRI
 MKUU Kassim Majaliwa anaondoka nchini leo (Jumatatu, Mei 23, 2016) 
kwenda Lusaka, Zambia kuhudhuria Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya 
Maendeleo ya Afrika (51st Annual Meeting of the Board of Governors of the African Development Bank – AfDB) utakaofanyika kesho (Jumanne, Mei  24, 2016).
Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli.
Mkutano huo ambao utafunguliwa na
 Rais wa Zambia, Edgar Lungu utajadili masuala ya Nishati na Mabadiliko 
ya TabiaNchi. Pia utahudhuriwa na Marais Idriss Deby wa Chad, Paul 
Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya. Nigeria itawakilishwa na 
Makamu wake wa Rais, Yemi Osinbajo huku Msumbiji ikiwazilishwa na Waziri
 wake Mkuu, Carlos Agostinho do Rosário.
Watu maarufu waliothibitisha 
kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Kofi Annan, Ashish Thakkar, John 
Kufuor, Mary Robinson, Mo Ibrahim, Nancy Lee, Ngozi Okonjo-Iweala na 
Tony Elumelu.
Mkutano huo utakaofanyika kwenye 
kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mulungushi (Mulungushi 
International Conference Centre) utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 
5,000 kutoka nchi  54 ambao ni wanachama wa benki hiyo, washiriki kutoka
 nchi 26 ambazo si za bara la Afrika (non-regional member countries), 
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi
 wa asasi za kiraia. Wengine ni Mawaziri wa fedha, biashara na uchumi na
 wataalamu kutoka vyuo vikuu.
Waziri Mkuu amefuatana na Naibu 
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Asantu Kijaji, wachumi kadhaa pamoja na 
wataalamu wa sekta ya fedha.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni