WAZIRI MKUU AKAGUA UTENDAJI KAZI MABASI YA DART
…………………………………………………………………………………………………………………
*Ataka watu walipe tiketi rasmi, wafuate taratibu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekagua utendaji kazi kwenye mabasi ya mwendokasi yanayotoa huduma
katika Jiji la Dar es Salaam na kubaini changamoto kadhaa ambazo amesema
zitarekebishwa kadri mradi unavyoendelea.
Waziri Mkuu ambaye alilipa nauli
na kupanda basi namba 23 lenye usajili namba T125 DGW kuanzia kituo cha
Ferry, Kivukoni, ametumia muda wa dakika 50 kufika Kimara mwisho kwa
kutumia usafiri huo.
Waziri Mkuu alipanda basi hilo
saa 3:30 asubuhi na lilianza safari saa 3:33 baada ya kusubiri wengine
wapande. Kwa wastani ililtumia kati ya dakika mbili hadi tatu kutoka
kituo kimoja hadi kingine. Basi hilo liliwasili Kimara Mwisho saa 4:23
asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa
habari akiwa Kimara mwisho mara baada ya kumaliza ziara hiyo fupi ya
ukaguzi leo (Ijumaa, Mei 27, 2016), Waziri Mkuu alisema aliamua kufanya
ziara hiyo ya ghafla ili kuangalia matumizi ya njia za mabasi yakoje na
pia kuona abiria wanaelewa vizuri namna ya kuitumia huduma hiyo.
Amesema ameridhishwa na mradi
unavyofanya kazi ila ameelezwa kuna usumbufu kwenye mageti wakati abiria
wanapotaka kuthibitisha tiketi zao hasa wakati wa asubuhi kunapokuwa na
msongamano wa abiria. Pia alielezwa kwamba kuna baadhi ya abiria
wanakuja na tiketi za jana yake jambo ambalo linaleta usumbufu kwa
sababu hazitambuliki kwenye mfumo wao.
“Nimeridhishwa na uharaka wa njia
kwa sababu na mimi mwenyewe nimetumia dakika 50 kufika hapa ingawa kuna
maeneo nimeona kuna haja ya kuwa na taa maalum za kuzuia magari
(special sensors) wakati mabasi yakipita ili kuepusha ajali,” alisema.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni
kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na mtaa wa Samora, Morogoro na
Jamhuri na makutano ya Morogoro na Kisutu.
Waziri Mkuu aliwataka Watanzania
waende na tiketi rasmi badala ya kutumia tiketi za jana kwa sababu
kufanya hivyo ni makosa na mtu anakuwa amedhamiria. “Hawa watachukuliwa
hatua za kinidhamu. Mtu akija na tiketi ya jana akamatwe na kupelekwa
polisi, huyu atakuwa amedhamiria,” alisema Waziri Mkuu wakati akiongea
na mhudumu mmoja katika kituo cha Kimara Mwisho.
“Ninawasihi wananchi wanaotumia
usafiri huu wajifunze kufuata utaratibu na kuwasisitizia kuwa kila
abiria aje na tiketi ambayo ni rasmi,” alisema na kuongeza: “Haya mabasi
nimebaini yako vizuri. Ninatoa msukumo kwa watumishi wa umma wapande
mabasi haya ili kupunguza msongamnao wa magari barabarani.”
Katika kupiunguza baadhi ya
changamoto, Waziri Mkuu alisema Serikali itasimamia uboreshaji wa
ukataji tiketi ili kuondoa usumbufu kwa abiria. Pia alivionya vyombo vya
moto viache kutumia njia maalum ya mabasi hayo.
Pia aliwataka polisi wanaofanya
doria za usiku kupita kwenye fly-overs na kuwaondoa watu wanaolala
kwenye maeneo kwani wanahatarisha usalama wa watu wanaotumia njia hizo.
“Zile siyo sehemu za kulala, wanaofanya hivyo wanahatarisha usalama wa
watumiaji wa njia hizo, kwa hiyo polisi wakiwakuta watu wa aina hiyo
wawakamate mara moja,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa
Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga ambaye alifuatana
na Waziri Mkuu kaktika ziara hiyo, alisema amepiga marufuku magari na
pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya Serikali.
“Tulishapiga marufuku magari na
pikipiki kutumia njia hiyo hata kama ni magari ya Serikali, ninawasihi
madereva watambue hili na watii,” alisema.
Machi 22, mwaka huu Waziri Mkuu
alitembelea soko la Feri kwa lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi
sokoni hapo (kuzuia moshi) na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha
soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Aprili 15, mwaka huu, Waziri Mkuu
alifanya kikao na kuwaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na
utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili
kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza pindi majaribio yakianza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni