NECTA SASA KUFUNGA MITIHANI KWA KUTUMIA MASHINE.
Baraza la Mitihani la Tanzania
(NECTA) limejipanga kuanza kufunga bahasha zenye karatasi za mitihani
kwa kutumia mashine maalum ili kuondokana na hatari ya kuvuja kwa
mitihani hiyo na gharama za ufungaji wa mitihani kwa kutumia mikono.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako wakati
akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka
2016/2017, jana Bungeni Mjini Dodoma.
Prof. Ndalichako alisema kuwa
katika kuimarisha utendaji kazi wake NECTA itanunua mashine mbili za
kufunga mitihani (Auto Poly Wrapping and Packing Machine) ili kuimarisha
usalama wa mitihani kwa kupunguza watu wanaoshiriki kwenye maandalizi
ya mitihani hiyo.
“Katika mwaka 2016/2017 Baraza
litasimika mashine mbili za kufunga bahasha za mitihani hivyo kuondoa
hatari zinazoweza kujitokeza kwa kuwa idadi ya watu wanaofanya kazi hiyo
itapungua.” alisema Prof. Ndalichako.
Aidha, Prof. Ndalichako aliongeza
kuwa Baraza litaboresha mfumo wake wa ukusanyaji na uchakati takwimu na
kuweka Mfumo wa Kielektroniki wa kumtambua mwanafunzi kwa namba maalum
tangu anapoandikishwa shuleni hadi atakapomaliza mzunguko wa masomo
yake.
Alisema kuwa mfumo huo wa
utambuzi utaunganishwa nchi nzima ili kuwezesha kufuatilia maendeleo ya
mwanafunzi kwenye shule yoyote atakayoenda kusoma ndani ya nchi kwa kuwa
namba hiyo atakayopewa na Baraza ataitumia hata kwenye shule nyingine
atakazohamia.
“Wizara itaweka Mfumo wa
Kielektroniki wa ukusanyaji taarifa za wanafunzi chini ya Baraza la
Mitihani ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo wakati wa mitihani
na utaratibu huu utapunguza matumizi makubwa ya fedha kupitia mfumo wa
TSM9.” alisema Prof. Ndalichako.
Pia alieleza kuwa katika
kufanikisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), mwaka wa fedha
uliopita Mamlaka ya Elimu Tanzania imechapisha vitabu 558,720 vya jinsi
ya kujibu mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha Nne ili kuwawezesha
wanafunzi watahiniwa kujibu maswali vizuri katika mitihani yao hatimaye
kuongeza ufaulu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni