SERIKALI YAANDAA MPANGO KABAMBE WA MIPANGO MIJI (MASTER PLANS) ILI KUONDOA MIGOGORO YA ARDHI
By Newsroom on May 26, 2016
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaandaa Mpango Kabambe wa Mipango Miji
(Master Plan) utakaoainisha matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro
ya ardhi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni
Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Mhe. Angelina Mabula wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mpango wa
Serikali kumaliza migogoro ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Mabula alieleza kuwa Wizara
yake inashirikiana na Halmashauri za Wilaya na Miji 18 kwenye program
ya Urban Local Government Supporting Programme (ULGSP) katika kuandaa
Mipango Miji hiyo.
Pia Mhe. Mabula alibainisha kuwa
Wizara inaandaa na kukamilisha programu ya kupanga, kupima na
kumilikisha kila kipande cha ardhi Tanzania itakayotekelezwa kwa kipindi
cha miaka kumi kuanzia 2015 hadi 2025.
“Serikali imekuwa ikiziagiza
Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji kwa
kuwa inatambua umuhimu wa kupima viwanja na mashamba ili kuwa na
matumizi bora ya ardhi yetu” alisema Mabula.
Aidha, Mabula aliongeza kuwa
Serikali kupitia Mradi wa Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kununua
vifaa vya upimaji ambavyo vitasambazwa katika kanda 8 za Wizara ya Ardhi
ili Halmashauri zote zilizopo ndani ya kanda hizo ziweze kunufaika.
Alieleza kuwa makadirio ya awali
ya gharama za mradi huo ni Dola za Kimarekani Milioni 4 ambapo Dola
Milioni 2 zitatumika kwenye upimaji na Dola Milioni 2 zitatumika kwa
ajili ya ununuzi wa Vifaa.
Katika kupunguza na kutatua
migogoro ya ardhi iliyopo sasa, Mabula alisema kuwa Wizara ya Ardhi
imeandaa kitabu cha orodha ya migogoro nchi nzima kinachoainisha vyanzo
vya migogoro hiyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Hali kadhalika, Mabula alisema
kuwa Wizara imesambaza Sera na Sheria za Ardhi hasa kwenye maeneo yenye
migogoro, wameimairisha mfumo wa kielektroniki katika kutunza
kumbukumbu, na kuboresha ofisi za Kanda ili kusogeza huduma za ardhi
karibu na wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni