SIKU YA VIPIMO DUNIANI: VIJANA WA KITANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA MAFUNZO KATIKA FANI YA VIPIMO
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel
Mjema (kulia) akiangalia moja ya mashine ya kisasa inayotumika
kufundishia wanafunzi wa Fani ya Mizani na Vipimo ndani ya karakana ya
chuo hicho leo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Vipimo Duniani yaliyoongozwa na kauli mbiu isemayo Vipimo katika dunia
inayobadilika.\
Mkufunzi
wa Mizani na Vipimo wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi Dar es salaam
Ishigita Shunashu akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza
wanaosomea fani hiyo leo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya
Siku ya Vipimo duniani.
Baadhi
ya wanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza katika Fani ya Mizani na Vipimo
katika Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE). wakiangalia moja
mashine ya kujifunzia masomo hayo iliyofungwa ndani ya Karakana ya
Idara ya Vipimo na Mizani.
Mkufunzi
katika Idara ya Mizani na Vipimo ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es
salaam (CBE) Bi. Rabia Katula akitoa ufafanuzi kuhusu namna
wanavyowajengea wanafunzi wa kuhakiki ubora wa mizani na kushughulikia
matatizo mbalimbali ya mizani.
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel
Mjema (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakufunzi
wa chuo hicho, Idara ya Vipimo na Mizani.
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel
Mjema (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi
wa mwaka wa kwanza wanaosomea shahada ya mizani na Vipimo.
Vijana wa kitanzania wametakiwa
kuchangamkia fursa za mafunzo katika fani ya vipimo na uendeshaji wa
mitambo mbalimbali ili Tanzania mpya ya viwanda iweze kujengwa na
wataalam wazawa kutoka ndani ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof.
Emanuel Mjema alipotembelea maonesho ya vitendo yaliyoandaliwa na walimu
na wanafunzi wa chuo hicho yaliyohusisha matumizi ya vifaa na
teknolojia ya kisasa ya Mizani na Vipimo.
Amesema Tanzania inahitaji
wataalamu wengi wa vipimo kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo kuanzia
ngazi ya kijiji hadi taifa katika sekta ya Mafuta kwenye makampuni
yanayouza mafuta, mafundi wa pampu za mafuta pia kwenye mitambo ya Gesi
na kuongeza kuwa mahitaji wa wataalam hao kwa sasa ni makubwa kuliko
idadi ya wataalam wanaozalishwa kwa mwaka.
Ameeleza kuwa sekta ya vipimo
duniani kote ni sekta mtambuka kwa kuwa inagusa maeneo mbalimbali ya
maisha ya mwanadamu na huchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa maendeleo
katika maeneo mbalimbali ikiwemo mazingira,teknoloji, Gesi, ubunifu
ambayo yote yana vipimo vyake.
Amesema kuwa CBE kama chuo
kinachofundisha fani ya Mizani na Vipimo nchini kimeungana na taasisi
nyingine za elimu duniani kuadhimisha Siku ya Vipimo duniani ambayo
mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu isemayo Vipimo katika ulimwengu
unaobadilika kuweka msisitizo katika ufundishaji unaokwenda sambamba na
mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayotokea duniani ili kukidhi
mahitaji ya soko.
Amesema Siku hiyo iliasisiwa
mwaka 1870 kwa lengo la kuweka viwango kwenye upimaji wa kutumia Mita na
kuongeza kuwa kuanzia wakati huo siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa
duniani kote.
Amefafanua kuwa chuo cha CBE
kimedhimisha siku hiyo kwa kuwa ni chuo pekee kinachotoa taaluma ya
elimu na watalaam wa Vipimo Afrika Mashariki, Kati na Kusini na
kubainisha kuwa nchini Tanzania taasisi za Serikali ikiwemo Wakala ya
Vipimo ambayo watalaam wake wengi wamefunzwa katika chuo hicho.
Prof. Mjema amesisitiza kuwa
suala la vipimo linagusa maisha ya kila siku ya wananchi kutokana na
umuhimu na kuzitaja sekta kama vile viwanda, madini na uchimbaji wa
Mafuta na Gesi haziwezi kufanikiwa bila kuwa na watalaam vipimo.
Ili kuhakikisha sekta ya vipimo
na Mizani katika chuo hicho inakwenda na mabadiliko yanayotokea duniani
chuo hicho kimekuwa kikibadilisha mbinu za kufundishia wanafunzi na
kuandaa mitaala mipya ili kukidhi mabadiliko hayo.
Aidha, amesema wao kama watalaam
wa vipimo wanasimamia na kutoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo
kupiga vita ufungashaji wa mazao kwa kutumia vifungashio vilivyozidi
maarufu kama Lumbesa ambayo vinamnyonya mkulima na kusababisha apate
kiwango kisichoendana fedha na wingi wa mazao yake.
Amefafanua kuwa katika
kukabiliana na changamoto ya mabadiliko inayotokana na uvumbuzi wa Gesi
na Mafuta nchini Tanzania CBE ilianzisha mitaala ya ufundishaji wa
nishati hizo kuwajengea uwezo wanafunzi wanaodahiliwa ili waweze
kumiliki uchumi na kusimamia rasilimali za taifa kwa manufaa ya
watanzania.
Prof. Mjema ameeleza kuwa licha
ya vifaa vya kisasa vya kufundishia kupatikana gharama kubwa,chuo hicho
imeendelea kufanya maboresho ya ndani kununua teknolojia mpya za kisasa
zinazotumia mfumo wa digitali ili kuwawezesha wanafunzi kutumia mitambo
mipya.
Amesisitiza kuwa CBE imeendelea
na program mbalimbali za kuwajengea uwezo wakufunzi wake kwa kuwasomesha
ndani na nje ya nchi ili waweze kutoa elimu yenye ubora na viwango
vinavyokubalika.
“Ni kweli dunia imebadilika na
teknolojia imebadilika sana tofauti na miaka ya nyuma, ili kuendana na
mabadiliko haya tumebaresha mbinu zetu za ufundishaji ili wahitimu wetu
waweze kumudu mahitaji ya soko kwa kukidhi viwango vya ndani na nje ya
nchi kwa kuwa suala la vipimo halina mipaka” Amesisitiza Prof. Mjema.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Chuo
hicho Bw. Boniface Nyamweru amesema kuwa mafunzo anayoyatoa kwa
wanafunzi wake yanalenga kuwajengea ujuzi na uwezo wa kubuni na
kuanzisha vifaa vyao wenyewe vinavyoweza kutumika kwenye masuala ya
Mizani na Vipimo.
Amesema kuwa yeye kama mtalaam wa
masuala ya Mizani na Vipimo anawafundisha wanafunzi wake namna ya
kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusiana na ufundi kwenye Mizani,
kufanya ukaguzi wa Mizani na Mita za kupimia vimiminika mbalimbali kama
mafuta ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mizani na vipimo nchini inapata
wataalam wa kutosha wenye ujuzi.
“Mpaka sasa tunao wataalam wa
ndani wazawa ambao tumewajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto
mbalimbali za kiufundi , wengi wao tumewafundisha sisi hapa chuoni na
wana uwezo wa kufanya ukaguzi na uhakiki wa Mizani na vifaa mbalimbali
vya Vipimo katika viwango na ubora unaotakiwa” Amesisitiza.
Kuhusu matumizi ya huduma ya
Mizani na vipimo nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria huku
akifafanua kuwa vipimo vinavyofanyika nchini ikiwemo matumizi ya mita ya
kupimia mafuta (Flow Meter) eneo la bandari ya Dar es salaam
vimeruhusiwa kisheria.
Faudhia Nchila mmoja wa wanafunzi
wa mwaka wa kwanza wanaosomea fani ya Mizani na Vipimo katika chuo
hicho amesema kuwa sekta ya Vipimo na Mizani ina mchango mkubwa katika
maendeleo ya nchi kwa kuwa inagusa shughuli za kila siku za maisha ya
wananchi.
Amesema vipimo vinagusa sekta ya
ujenzi, maji, vifaa, teknolojia na shughuli mbalimbali za ufundi katika
maeneo mbalimbali nchini huku akisisitiza kuwa mahitaji ya wataalam wa
vipimo nchini kwa sasa ni makubwa kutokana na mchango wake katika
maendeleo ya nchi na kutoa wito kwa vijana wengi zaidi kujiunga na
masomo hayo.
Naye Dunstan Binamu mwanafunzi wa
mwaka wa kwanza anayesomea masuala ya sheria katika fani ya Mizani na
Vipimo akieleza mchango wa fani anayoisomea katika maendelea ya nchi
amesema kuwa inalenga kulinda Haki ya mlaji katika kwa kuhakikisha
masuala vipimo na mizani yanafanyika katika viwango vilivyowekwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni