DAWASCO kugharamia gharama za uunganishwaji wa maji kwa wateja wake.
Maji ni rasilimali muhimu
kwa maisha ya viumbe vyote pamoja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote, ubora wa afya na mazingira kwa
ujumla vinategemea kuwepo kwa maji yakutosha na yenye ubora unaotakiwa.
Maji yana mchango mkubwa
sana katika maendeleo ya jamii kwa kuwa hutumika kwa matumizi mbalimbali
kama vile kuzalisha umeme,kupika, kuoga na kufua nguo, katika ujenzi na
kusaidia maisha ya viumbe hai, matumizi ya viwandani pamoja na kilimo
hivyo usimamizi na utunzaji wake lazima uzingatiwe.
Serikali ina malengo ya
kuwapatia maji wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani, Kibaha
pamoja na Bagamoyo kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.
Hakika aja ya mja hunena,
muungwana ni vitendo. Hii imethibitika kuwa kweli Serikali ya Awamu ya
Tano inajali watu wake hasa wa hali ya chini kama Rais John Pombe
Magufuli ambavyo hupenda kuwaita wanyonge. Watu wengi wanahitaji kuwa na
maji ya bomba lakini uwezo wa kuunganisha ulikuwa mgumu kwani gharama
wengi waliiona kuwa ni kubwa sana.
Kwa kulitambua hilo
Serikali imeamua kuingia gharama za kuwaunganishia maji wateja wake na
wenyewe watalipia kidogo kidogo gharama hizo. Hili ni jambo la kuungwa
mkono sana.
Hapa tunamsikia mkazi wa
Mbweni, Jijini Dar es Salaam, Bi Fatuma Iddi akisema,“Kwa kweli serikali
hii imetukumbuka, mimi nilishapoteza matumaini ya kupata maji kwangu
kwani sikuwa na uwezo wa kulipa malaki hayo kwa ajili ya kuunganishiwa.
Lakini kwa kulipia kwa awamu hilo nitalimudu. Heko Mhe. Rais Magufuli
kwa kutujali hasa sisi wanyonge.”
Takwimu zilizotolewa na
Ofisi ya Mkoa wa Dar es Saalam zinaeleza kuwa Mkoa unapata maji kutoka
katika mito na visima ambapo eneo kubwa la Mji huo linahudumiwa na
Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ambayo imepewa mkataba na
Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASA) na kwa maeneo
yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka kwenye visima
vinavyoendeshwa na vyombo vya watu binafsi.
Aidha, vyanzo vikuu vya maji
yanayopatikana katika Mji wa Dar es Salaam ni mitambo ya Ruvu Juu ambao
kwa siku unazalisha jumla ya lita milioni 82, Ruvu Chini unazalisha
lita milioni 270, Mtoni unazalisha lita milioni 9 na visima virefu 106
ambavyo vinazalisha jumla ya lita milioni 106 kwa siku.
Vyanzo vyote hivi huzalisha
wastani wa jumla ya lita milioni 371 kwa siku zinazotosheleza asilimia
75 ya mahitaji ya wananchi.Mahitaji ya maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam
yamefikia Lita milioni 450 kwa siku yakijumuisha matumizi ya nyumbani,
matumizi ya Viwanda, Kilimo, Mifugo, na usafi wa Jiji kwa siku.
Hata hivyo mtandao wa DAWASA
unapoteza takribani Lita 128,000 sawa na asilimia 48 kwa siku kutokana
na ubovu wa mitambo, uchakavu wa mabomba na matumizi yasiyo halali
lakini hali hii inaendelea kudhibitiwa na DAWASA kwa kukarabati
miundombinu yake, kuwawekea wateja mita za kupima kiasi cha maji
wanayotumia, kuelimisha wananchi na kuchukua hatua za kisheria kwa wale
wanaopatikana na makosa ya uharibifu wa miundombinu au wizi wa maji,
kuongeza matanki ya kuhifadhia maji na kufunga mabomba mapya kwenda
maeneo yasiyokuwa na huduma na kuchimba visima virefu.
Hii inaonyesha dhahiri kuwa
maji yanayozalishwa bado hayatoshelezi wakazi wa Mji huu lakini Serikali
inajitahidi kwa hali na mali kuwasaidia wananchi wake kuondokana na
adha hii ya ukosefu wa maji safi na salama.
Katika kutekeleza kauli mbiu
ya “Hapa kazi tu” ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt.
John Pombe Magufuli aliagiza kuwa ifikapo Juni mwaka huu wateja 400,000
wa Mkoani Dar es Salaam wawe wamepatiwa huduma ya maji safi na salama.
Ili kutekeleza agizo hilo,
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam imeamua kugharamia
uunganishaji wa huduma hiyo kwa wakazi wake ambapo gharama hiyo ilikua
ikilipwa na mteja mwenyewe.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema
kuwa zoezi hili la kugharamia uunganishaji wa huduma ya maji kwa wateja
ni kwa kipindi maalumu cha miezi miwili ambayo ni Mei na Juni ambapo
mteja atawajibika kurudisha gharama za uunganishaji kidogo kidogo kila
mwezi kwa muda wa miezi kumi na mbili.
“Fursa hii itasaidia hata
kwa wananchi wenye kipato cha chini kuweza kuunganishiwa huduma ya maji
hivyo nawasihi wananchi wa sehemu husika kujitokeza kwa wingi kupatiwa
huduma hii,”alisema Mhandisi Luhemeja.
Naye Mkurugenzi wa Biashara
wa Kampuni hiyo Bi. Everada Balati ametoa rai kwa wananchi kutopuuzia
fursa hii kama walivyopuuzia fursa zingine zilizopita kwa kuwa hii ni ya
tofauti na anaamini kuwa watu wengi wataweza kuimudu.
“Huduma hii ni ya haraka
kwakua haichukui zaidi ya wiki kukamilika,mteja wetu atalipia kulingana
na urefu wa sehemu ambayo atafikishiwa huduma hiyo”,alisema Bi. Balati.
Bi. Balati amesisitiza kuwa
malipo haya hayatakuwa na riba bali mteja atahitajika kulipia gharama za
uvutaji wa bomba kama zilivyoainishwa na utaratibu wa malipo
utaunganishwa pamoja na bili ya kawaida ya maji inayopelekwa kwa mteja
kila mwezi.
Wakazi wa Dar wanashauriwa
kuitumia fursa hii nzuri iliyotolewa na DAWASCO ili kuweza kupata huduma
ya maji safi kwa urahisi kwa kuwa gharama za uunganishwaji zilikua
zikiwashinda wananchi wengi sasa unaunganishiwa na kulipia gharama hizo
kidogo kidogo kwa muda wa miezi 12.
Kusema ukweli hii ni fursa
kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani na imekuja kipindi muafaka ambapo
mtambo mkubwa wa maji wa Bagamoyo unakaribia kuanza rasmi. Hii itaondoa
adha ya wakazi wa jiji ambao walilazimika kuamka usiku wa manane ili
kupata maji pindi yanapotolewa kwa mgao. Pia itaondoa kero ya kuuziwa
maji yasiyo salama ambayo watu wengi wamekuwa wakinunua bila kujua maji
hayo yanapatikana wapi na yako safi na salama kiasi gani.
Falsafa au kauli mbiu ya
Hapa Kazi Tu imetafsiriwa kwa vitendo. Hii inajibu kauli mbiu jingine
iliyokuwa inasema Maisha Bora kwa kila mtanzania. Haya kwa hakika
yatakuwa maisha bora kwa kila mtanzania kwani hakuna ambaye siku hupia
bila kutumia maji, iwe mtoto, mkubwa na hata kikongwe anahitaji maji.
Ndio maana watu husema ya kuwa Maji ni Uhai.
DAWASCO zoezi hili
mlikamilishe kwa wakati kama mnavyosema kuwa litadumu kwa miezi miwili
yaani Mei na Juni. Uondoaji wa kero ya maji utasaidia nguvu nyingine na
muda uliokuwa unatumika kwa ajili ya kutafuta maji, kutumika kwa
shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni