Ijumaa, 6 Mei 2016

JE,WAJUA UNAWEZA KUPATA NYWELE NDEFU KUPITIA VYAKULA?




Na Tinah Reuben

ULAJI mzuri umekuwa ukihusishwa katika kuboresha afya ya mwili,akili na ngozi pekee lakini pia unaweza kusaidia katika kuboresha afya nywele na kuzikuza.
Baadhi ya vitu vinavyoweza kufanya nywele zako zikakosa afya na mvuto ni pamoja na vumbi, upepo, mvua, jua, maji na dawa tunazoweka kwenye nywele zetu pamoja na vyakula tunavyokula ambavyo ni chanzo kikuu cha nywele zetu kuharibika na kukosa afya na mvuto.
Watu wengi wamekuwa wakihangaika kupata nywele zilizojaa na ndefu kwa kutumia madawa yenye kemikali ambayo ni hatari lakini hawajui hata ulaji wa chakula unaweza kukusaidia kupata nywele nzuri za asili zinazong'aa bila hata kutia madawa,katika safu hii ya afya leo nimeamua kukuletea aina hizo za vyakula.Ulaji wa vyakula vyenye vitamini, madini kama carbohydrates, protini na vyakula vingine vyenye mafuta kwa ujumla husaidia sana katika hili.Ili kupata nywele zenye afya na zenye kungaa zaidi unatakiwa kupata vitamini vyote yaani (A, B, C, D,na E)na pia madini kama(chuma, zinc, phosphorous, potassium, na magnesium).
Pia mbogamboga kama Spinach, broccoli, Swiss chard, pamoja na mboga zote za kijani kama mchicha hukupa vitamini muhimu.
Vitamini A na C ni muhimu sana katika kuzifanya nywele zikue, vitamini hivi husaidia kuzalisha waxy material, inazalisha sebum – vitamini ambayohuzalisha mafuta yanayosababisha nywele kukua.Mafuta haya yanakuwa kama kondishina ya asili ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa nywele kukua.
Vyakula jamii ya karanga pia vina uwezo mkubwa wa kuzalisha mafuta yanayokuza nywele na zina madini mengi kama chuma pamoja na vitamini E yenye uwezo kurefusha nywele zako na kuvutia.Madini ya chuma yana uwezo mkubwa wa kuzalisha damu nyingi pia vitamin E husaidia damu kutembea na kuzunguka vizuri.
Mambo mengine yanayoweza kukusaidia ni pamoja na kukata ncha za nywele zako ili kuondoa seli zilizokufa na kuzifanya zistawi vema kwa kuanza kujaa upya na kuwa na afya japo ni jambo gumu kidogo mtu kukata nywele zako lakini litakusaidia.
Pia ni lazima utambue kuwa nywele nazo zinahitaji nafasi na kupumzika,kuchana nywele kila siku, kuzipaka nywele jelly kila siku, kuzichana mitindo tofauti, kuziwekea gundi na mafuta tofauti tofauti huzifanya nywele zako zichoke na kukosa afya.
Hivyo unatakiwa mara moja moja uwe unazipa nywele zako nafasi,zipumzishe nywele zako kwa kusuka mitindo ya kawaida au rasta za mabutu.
Vilevile ni muhimu kuosha nywele mara kwa mara na ukijua aina ya nywele zako itakusaidia pia kujua ni aina gani ya shampoo inayokufaa.
Epuka kuzichana nywele zikiwa mbichi au tumia chana kubwa ili kuzuia kukatia unaweza pia kutumia vifaa vya kukaushia kama unavyo,zifunge unapolala na uzihifadhi wakati wa kuogelea kwa kuvaa kofia maalumu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni