TADB YAJIPANGA KUWAKOMBOA WAKULIMA NCHINI
Kwa miaka kadhaa sasa kilimo
kimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania hasa katika
upatikanaji wa chakula, biashara ya mazao nje ya nchi, kusaidia
upatiakaji wa malighafi za viwanda vya ndani na kutoa ajira kwa
Watanzania.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka
2015 Tanzania iliuza jumla ya tani 125,134 za mazao ya kilimo katika
soko la nje ikiwemo tani 63,237 za mahindi, Ngano tani 42,538, Mpunga
Tani 7,651 na Mihogo Tani 11,708.
Pamoja na kwamba zaidi ya
asilimia 75 ya Watanzania watagemea kilimo na kutoa zaidi ya asilimia 65
ya malighafi kwa ajili ya viwanda nchini, asilimia kubwa ya shughuli za
kilimo zinafanywa na wakulima wadogo.
Hata hivyo pamoja na umuhimu na
sekta ya kilimo kwenye uchumi wa nchi, bado ukuaji wa sekta hiyo umekuwa
ukikabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kiwango kidogo cha
uzalishaji, ukosefu wa mbinu na teknolojia za kisasa, matumizi madogo ya
umwagiliaji, ukosefu wa mtaji na ukosefu wa mikopo kwa wakulima.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
(TADB) ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa ni jitihada za Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kukabiliana
na changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo nchini.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa
benki hiyo Dkt. Jakaya Kikwete alisema kuwa Serikali imekuwa ikisaidia
sekta ya kilimo kupitia ruzuku za pembejeo na mbolea na kwa sasa
imeanzisha benki ili kero mbalimbali za wakulima zitatuliwe kwa wakati.
Pia Dkt. Kikwete aliwataka
wakulima kutambua kuwa kilimo ni shughuli inayoweza kuwaletea kipato
kikubwa, hivyo watutumie fursa zinazotolewa na Benki ya Kilimo katika
kuendeleza sekta hiyo na kujiongezea zaidi kipato kwani ni wakati kwa
wakulima kufanya shughuli hiyo kiutaalamu zaidi badala ya kuendelea na
kilimo cha mazoea.
Mbali na kutekeleza sera ya
Serikali kuhusu upatikanaji wa fedha za kuendeleza kilimo, pia benki ya
kilimo imepanga kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula
utakaokuwa endelevu na kusaidia kuleta mapinduzi ya kilimo ili kuwatoa
watanzania katika kilimo cha mazoea kwenda katika kilimo cha kibiashara.
Katika kutimiza lengo la
kuanzishwa kwake Benki ya kilimo imetoa elimu kwa wakulima ambapo
vikundi 89 vyenye Wakulima 21,526 vilipatiwa elimu mkoani Iringa,
kufanya tafiti mbalimbali kwenye sekta ya kilimo, kuwajengea uwezo
wakulima hasa vijana katika kuanzisha miradi ya kilimo ili pale
watakopewa mikopo waweze kuitumia vizuri na kuwaletea faida katika
shughuli zao.
Benki imejipanga kutoa mikopo ya
mudamfupi, (Hadi Miaka 2); muda wa kati (zaidi ya miaka 2 hadimiaka 5);
na muda mrefu (zaidi ya miaka 5 hadimiaka 15) kwa Wakulima wadogowadogo,
wa kati na wakubwa ili kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwenye
mnyororo wa ongezeko la thamani katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na
mazao ya misitu (ufugajinyuki).
Akiongea na waandishi wa habari
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Bw. Thomas Samkyi
alisema Benki hiyo imejipanga kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na
mrefu kwa riba nafuu (kati ya 7% hadi 12%) kwa kupitia muungano wa
vikundi vya Wakulima wadogo wadogo, benki za maendeleo ya jamii, vyama
vya kuweka na kukopa, taasisi ndogo za fedha, vyama vya ushirika na
taasisi au vyama vya wakulima.
Bw. Semkyi aliongeza kuwa benki
hiyo imetoa mikopo kwa wakulima kwa kwa vikundi 8 vya wakulima wapatao
857 na sasa inashughulikia maombi ya mikopo kwa awamu nyingine yenye
thamani ya Zaidi ya Sh Bilioni 40.
“Napenda kuwashauri wakulima
wajiunge katika vikundi ili kuirahisishia benki kuwatambua na kutoa
mikopo ya riba nafuu ya kati ya asilimia 7 hadi 12 ili waweze kuendesha
shughuli zao za kilimo katika maeneo ya uzalishaji mazao, uvuvi na
ufugaji hali itakayowawezesha kuwatoa katika kufanya kilimo cha mazoea
na kwenda katika kilimo cha kibiashara” Alisema Bw. Semkyi.
Akifafanua kuhusu aina ya
riba hasa kwa vikundi, Mkurugenzi wa Mikopo na Usimamizi wa Biashara wa
Benki ya Kilimo Bw.Robert Paschal alisema kuwa Riba yake ni asilimia
saba hadi nane na wanaokopeshwa ni wakulima wadogo walio kwenye vikundi.
Alisema wakulima hao watapata
mkopo kwa ajili ya ununuzi wa mbegu bora, kulima shamba na mahitaji
mengine ya shamba ambapo marejesho ya mkopo huo ni mara baada ya mkulima
kuvuna mazao.
Bw. Paschal aliongeza kuwa
kama msimu wa mavuno haukuwa mzuri, labda mvua hazikunyesha na mkulima
hawakupata mavuno, wakijiridhisha na ukweli wa hilo, mkopo unasogezwa
msimu unaofuata.
Aidha Bw. Paschal alisema
kuwa aina nyingine ya mkopo ni wa kati, unaotozwa kwa kipindi cha miaka
miwili hadi mitano na riba yake ni asilimia tisa hadi 10, na mkopo huo
ni kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa vifaa vya kilimo na upanuzi wa
mashamba.
Akizungumzia mafanikio
aliyoyapata baada ya kupata mkopo kutoka TADB, kiongozi wa Chama cha
Nzihi Mixed Crops kilichopo Mkoani Iringa Bw. Emmanuel Fungo anasema
benki hiyo imewapatia mkopo wa shilingi Milioni 222 ambao umewasaidia
sana kwa sababu wameupata kwa muda walioutarajia na bila masharti magumu
tofauti na taasisi nyingine zinazolazimu kuhamishia akaunti yako kwenye
taasisi hiyo.
Anasema sanjari na kuwapatia
mkopo huo pia TADB imewatafutia mteja wa mazao (Mahindi) watakayozalisha
hivyo wana uhakika watauza mazao na kuweza kulipa mkopo na kubaki na
mazao ya ziada.
Rai yangu kwa wakulima ambao mara
nyingi wamekuwa wakilalamikia uhaba wa rasilimali fedha katika
kuendeleza shughuli zao za kilimo ni kutumia fursa inayotolewa na Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
Alisema benki hiyo imejiwekea
malengo katika utoaji mikopo ya uongezaji wa thamani katika shughuli za
kilimo na kuwawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika wa mazao wakati
wa mavuno.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni