TFF YATOA ONYO KALI
Wakati
pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara likitarajiwa kufungwa
Jumapili Mei 22, 2016 kwa michezo minane, Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), limetoa onyo kali kwa timu zote kutojiingiza kwenye mtego wa aina
yoyote wa kupanga matokeo.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi
ameziasa timu zote za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kucheza mechi
hizo kwa kufuata taratibu, kanuni za Ligi Kuu kadhalika sheria 17
zinazoongoza mchezo huo ambao unapendwa na mamilioni ya watu Tanzania na
dunia nzima.
“Nimefanya tathmini yangu na
kubaini kwamba, inawezekana kukawa na mipango ya kupanga matokeo.
Nichukue nafasi hii kuzionya timu zote kutojiingiza hulo. TFF iko
makini, tena makini sana na ina watu wake kila mkoa ambako michezo hiyo
itafanyika, sasa basi naziasa timu kufuata taratibu, kanuni na sheria,”
alisema Malinzi.
Mbali ya Malinzi, pia Bod ya Ligi
nayo imetoa onyo ikisema michezo yote haina budi kuanza saa 10.00 jioni
hata kama kutakuwa na hali ya mvua katika viwanja husika lengo likiwa ni
kukabiliana na upangaji wa matokeo.
Baada ya michezo 29 kwa kila timu,
tayari Coastal Union ya Tanga ikiwa imeaga rasmi Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania 2015/16 na kwamba kuna timu tano ambazo baadhi yake (timu
mbili) zikipata matokeo mabaya zitaungana na Wagosi wa Kaya kushuka
daraja msimu wa 2015/16. Coastal Union yenye pointi 22 na hata ikishinda
mchezo wa mwisho, haiwezi kuzifikia timu zilizo juu yake.
Timu ambazo ziko kwenye hatari ya
kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15);
Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera
Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani
iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye
pointi 30 (nafasi ya 11).
Kwa hali ya mambo ilivyo, licha ya
kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu ikilinganishwa na timu
nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye pointi 27 hadi 29 zinaweza
kuishusha kama Wanakishamapanda hao watapoteza mchezo wa mwisho au
kupata sare huku wapinzani wao wakishinda.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara, Toto Africans itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha Stand United, wakati JKT Ruvu
mgeni wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wenyewe Kagera Sugar watamaliza na
Mwadui FC watakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga wakati Mgambo
wataalikwa Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi-Mbagala,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ilihali African Sports
‘Wanakimanumanu’ wataifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu,
Mvomero mkoani Morogoro.
Mechi nyingine ya kukunja jamvi
kwenye Ligi Kuu ya Vodacom zitakuwa kati ya Mabingwa wa Ligi Kuu msimu
huu, Yanga itakayokuwa mgeni wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa
Majimaji wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo mwingine wenye presha
utakuwa ni kwa Tanzania Prisons yenye pointi 48 ambayo licha ya kucheza
na Coastal Union ambayo imeshuka daraja kwenye Uwanja wa Mkwakwani,
itakuwa inafukuziwa na Mtibwa Sugar kuwa na nafasi ya nne. Mtibwa Sugar
ina pointi 47.
Tanzania Prisons itacheza na timu
ambayo haina nafasi katika Ligi Kuu msimu huu. Presha kubwa ni kwa Simba
na Azam ambazo zina tofauti ya pointi moja katika msimamo wa ligi hiyo
iliyoshirikisha timu 16.
Azam FC ina pointi 63 ikishika
nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga huku Simba inayoshika nafasi ya
tatu ina pointi 62. Mvutano wa Tanzania Prisons, Mtibwa ni wa nafasi ya
tatu na nne hasa ukirejea kwenye zawadi za Vodacom ka timu vinara kama
ilivyo kwa Azam na Simba.
Yanga ambayo imetwaa ubingwa,
tayari imepewa taji na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi
la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji Jumamosi iliyopita na
inachusubiri ni fedha Sh 81,345,723 wakati Azam na Simba zinawania
zawadi ya mshindi wa Pili Sh 40,672,861 na Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044
huku Prisons na Mtibwa Sugar zikichuana kupata zawadi ya Mshindi wa Nne
ambayo ni Sh 23,241,635.
Pia timu zote zinawania zawadi ya
Mchezaji Bora ambayo ni Sh 5,742,940 kiwango kinachofanana na
atakachopewa Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa Bora wa michuano hiyo
inayodhaminiwa na Vodacom wakati Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610
kiwango kinachofanana atakachopewa Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu
itavuna Sh 17,228,820.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni