ZIARA YA MAJALIWA LINDI NA MTWARA
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wazee wa Ruangwa ambao
walimshukuru kwa jitihada kubwa anazofanya za kuboresha maisha ya
Wanachi wa jimbo lake la uchaguzi. Alikuwa katika ziara ya jimbo lake
la uchaguzi Julai 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo tano kati ya tisa alizokuwa
anakatwa mkulima wa zao la korosho uko pale pale na unatarajiwa kuanza
kutumika katika msimu mwaka huu hivyo ameitaka Bodi ya Korosho kusimamia
uamuzi huo.
“Watendaji wa Serikali katika
ngazi mbalimbali mnatakiwa kuhakikisha kwamba maelekezo haya yanafuatwa.
Malengo yetu ni kumpunguzia mkulima mzigo wa tozo nyingi alizokuwa
anakatwa,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
jana jioni (Jumamosi, Julai 16, 2016) wakati akipokea taarifa ya
maendeleo ya mkoa Mtwara pamoja na taarifa ya kuondolewa kwa baadhi ya
tozo katika zao la korosho zilizowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Halima
Dendego.
Alisema Serikali iliamua kuzifuta
tozo hizo baada ya kubainika kuwa zilikuwa zikiwanyonya wakulima hali
iliyosababisha wauchukie mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Kuanzia mwaka huu Serikali
imeamua mfanyabiashara yeyote wa korosho hana budi kuanza kulipa malipo
ya awali kabla ya kuingia kwenye mnada ili tuwe na uhakika wa kununua
korosho hizo na kuwalipa wakulima kwa wakati,” alisema.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya
kushuka kwa uzalishaji wa korosho Waziri Mkuu aliutaka mfuko wa wakfu
wa kuendeleza zao hilo ufanye utafiti wa kubaini sababu ili waweze
kutafuta namna ya kuipatia ufumbuzi.
“Nitakuja kukutana na viongozi wa
mfuko waniambie wanafanya nini na wamefanya nini miaka mitatu iliyopita
na wana mpango gani huko mbele tunakokwenda kama hakuna mpango
tutauangalia mara mbili mbili kwani wana fedha nyingi lakini hata mbegu
hawapeleki kwa wakulima,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
aliitaka Bodi ya Korosho kuhakikisha kila msimu wakulima wanapata
pembejeo bora na zinawafikia kwa wakati ili waweze kupata mazao ya
kutosha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni