Wadau wa Maafa wajengewa uwezo kuandaa Kanzi Data ya Athari za Maafa.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
…………………………………………………………………………………………….
Na. MWANDISHI WETU
Shirika la Umoja wa Mataifa la 
Upunguzaji Athari za Maafa (UNISDR) kwa kushirikiana na Idara ya Uratibu
 wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu wameendesha mafunzo ya siku mbili kwa 
wadau wa masuala ya maafa juu ya namna ya kutumia Kanzi Data ya takwimu 
za Athari za Maafa kutoka Wizara na Taasisi za Serikali nchini.
Mafunzo hayo yalifanyika Julai 19 
na 20, mwaka huu katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kushirikisha Wizara na 
Taasisi za Serikali ikiwemo; Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya 
Ulinzi na Usalama wa Taifa, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Jeshi
 la Zima Moto, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Hali ya Hewa, Mamlaka ya 
Usafiri wa Majini na Nchi Kavu, TAMISEMI, Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo 
Kikuu cha Dar es Salaam na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Mafunzo hayo yalijikita katika 
kusaidia wadau wa masuala ya maafa katika kuongeza uwezo wa kuwa na 
Takwimu sahihi za majanga yanayoikabili Nchi ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo
 Mratibu wa Masuala ya Maafa Shirika la Umoja wa Mataifa la Upunguzaji 
Athari za Maafa, Bw. Adam Fysh alieleza kuwa, Mafunzo 
hayo yatasaidia kuongeza uboreshaji wa kumbukumbu za maafa nchini, “kama
 ilivyokusudiwa, mafunzo yatasaidia kuwa na rekodi za kutosha, 
yatasaidia ufuatiliaji, kuwa na tathimini za mara kwa mara, na 
ulinganifu wa kujua nchi zingine zinafanya nini katika kukabiliaana 
na athari za maafa, mafunzo haya pia yatasaidia wahusika kufanya maamuzi
 sahihi na kwa wakati katika maendeleo hususani kwa kupunguza athari za 
maafa hapa nchini”
Bw. Fysh aliongeza kuwa kiu yake 
ni kuona nchi zinajikita katika utoaji wa taarifa zenye uhalisia na 
sahihi ili kuwa na kumbukumbu na takwimu zenye kusaidia Dunia kujua 
maafa yanayotokea, “Natamani kuona tunakuwa na takwimu sahihi na zenye 
mpangilio zinazohusu athari za maafa hususani yanayoikabili nchi’
Kwa upande wake Mkurugenzi wa 
Idaya ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu  Brig. Jenerali, Mbazi 
Msuya alishukuru jitihada za Shirika hilo kwa kuona umuhimu wa 
kuwajengea uwezo wadau wa masuala ya Maafa na kueleza kuwa mafunzo hayo 
yamekuja kwa wakati na yataleta manufaa makubwa kwa Taifa.
“Nawapongeza Shirika kwa kuona ni 
vyema kuifikia Tanzania kwa kuijengea uwezo wa namna ya kuweka taarifa 
muhumu za masuala ya Maafa katika kanzi data. Hii itatusaidia sana 
katika kupanga mipango yetu kwa namna bora zaidi na vile vile itarahisha
 katika kufuatilia kufanya tathmini”, Alisema Brig. Msuya
Naye Mtaalam wa Masuala ya Hali ya
 Hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa, Bi.Hellen Msemo 
alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutoa fursa za kimaendeleo kwakuwa
 takwimu za athari za maafa zitasaidia kuwa na mipango mizuri ya 
maendeleo ya nchi na kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuona umuhimu 
wa kuratibu mafunzo hayo.
Mafunzo ya kutumia Kanzi Data ya 
takwimu za Athari za Maafa tayari yamezifikia nchi 31 duniani huku 
Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi kumi na tatu za Afrika zilizonufaika
 na elimu hiyo.
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni