WAZIRI PROF.MBARAWA ATOA MIEZI MIWILI KUKAMILISHA UJENZI WA barabara ya Mangaka-Nakapanya
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akisalimia
na wananchi wa Tunduru, baada ya kukagua barabara ya Tunduru-Nakapanya
KM 66.5, Mkoani Ruvuma.
………………………………………………………………………………………..
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi
miwili kwa mkandarasi wa kampuni ya M/s Jiangxi Geo-Engineering (Group)
Corporation anayejenga sehemu ya barabara ya Mangaka-Nakapanya yenye
urefu wa Km 70.5 kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha
lami.
Amesema
hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Tunduru-Mangaka-Mtambaswala
inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 202.5 ambayo
kukamilika kwakwe kutafungua fursa za kiuchumi na kuunganisha mikoa ya
Ruvuma, Mtwara na Lindi.
Amebainisha
kuwa Mpango wa Serikali ni kuwajengea watanzania miundombili bora
itakayowafikisha katika uchumi wa kati ifikapo 2025 hivyo haitamvumilia
Mkandarasi anayechelewesha kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali
inayotekelezwa hapa nchini.
“Natoa
miezi miwili mkandarasi uwe umemaliza hii barabara, wananchi wa Mangaka
na Tanzania kwa ujumla wanahitaji kuanza kuitumia kwa ajili ya kuinua
uchumi wa Taifa”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri
Mbarawa ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha kwa Makandarasi
wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini hivyo lazima wajipange kumaliza
kazi kwa wakati na kuzingatia viwango vya ubora kulingana na makubaliano
ya mkataba.
Aidha
amesisitiza kuwa Serikali haitaingia mkataba mwingine kwa mkandarasi
yoyote ambaye hatakamilisha kazi kwa wakati kulingana na makubaliano.
Kwa
upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa
Mtwara Eng. Dotto John amemhakikishia Waziri Mbarawa kusimamia mradi
huo ili ukamilike kwa wakati na kuchochea maendeleleo ya Mikoa ya
kusini.
“Wananchi
wamengojea kwa muda mrefu kukamilika kwa mradi huu ili uwe kichocheo
cha maendeleo hivyo ninakuhakikishia kuwa nitawasimamia kwa umakini
makandarasi ili wazingatie vigezo tulivyokubaliana kwenye mkataba”,
amesisitiza Eng. Dotto.
Waziri
Prof. Mbarawa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya
Tunduru-Mangaka-Mtambaswala yenye urefu wa km 202.5 inayojengwa kwa
kiwango cha lami ambapo kukamilika kwake kutafungua fursa za kiuchumi
mikoa ya Kusini ikiwemo kuiunganisha Tanzania na Msumbiji kwa lami
kupitia daraja la umoja lililoko Mtambaswala.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni