KALA JEREMIAH, SUPER NYAMWELA KUPAMBA MSIMU MPYA WA JUKWAA LA SANAA LA BASATA
Msimu
mpya wa Jukwaa la Sanaa unatazamiwa kuzinduliwa rasmi Jumatatu ya
tarehe 25/07/2015 kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba
jijini Dar es Salaam kuanzia saa saa 4:00 Asubuhi – 6:30 Mchana.
Wasanii
hawa wanatarajiwa kuupamba uzinduzi huo kwa kutoa burudani mbalimbali
sambamba na kuongea na wasanii wachanga katika kuwahamasisha na
kuwajengea uwezo juu ya namna wanaweza kutumia fursa mbalimbali za
mashindano ya kukuza vipaji katika kujijenga kisanaa.
BASATA
linatambua kwamba kumekuwa na tatizo la wasanii katika kutambua na
kuchangamkia fursa mbalimbali zilizoko katika sekta ya Sanaa hasa zile
zilizomo kwenye mashindano mbalimbali ya kutafuta vipaji ambayo wasanii
Kala Jeremiah na Super Nyamwela wamekuwa wakishiriki kikamilifu.
Ushiriki
wa wasanii hawa katika kuwajengea hamasa na kuwapa changamoto wasanii
wachanga utasadia katika kuwajengea uwezo wa kutumia fursa hizo.
Mbali
na burudani na elimu hiyo, uzinduzi huu wa msimu wa mpya wa Jukwaa la
Sanaa unaotarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya mia moja (100)
utahusisha pia kongamano maalum ambalo litajikita katika kutoa elimu
mbalimbali kuhusu sekta ya Sanaa kwa wadau watakaohudhuria.
Jukwaa
la Sanaa ni programu iliyobuniwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya
Sanaa lakini pia kusaidia waandishi wa habari kupata habari zihusuzo
sekta ya Sanaa kutoka vyanzo mahsusi.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Imetolewa na Kitengo cha Habari
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni