Wadau wa Sanaa nchini wahamasishwa kudhamini na kufadhili Mashindano ya Urembo bila ubaguzi.
……………………………………………………………………………………………..
Na. Benedict Liwenga-WHUSM.
Wadau
wanaojishughulisha na masuala ya Sanaa nchini wamehamishwa kujitokeza
kwa wingi katika kusaidia maendeleo ya Sanaa kwa kudhamini na kufadhili
mashindano ya urembo bila kubagua.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw.
Francis Songoro wakati alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Naibu Waziri wa
Wizara hiyo, Mhe. Anastazia Wambura ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi
katika Mashindano ya Miss Tanzania Indian Ocean 2016 yaliyofanyika
katika Ukumbi wa MRC uliopo Mikocheni jijini hapa.
Akiwasilisha
hotuba hiyo, Songoro amesema kwamba kazi inayofanywa na wadau wa sanaa
ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utamaduni ambayo inasisitiza
jamii na wakuzaji sanaa kuendeleza ubunifu katika kazi za kiutamaduni.
Ameeleza
kuwa, Serikali kupitia Wizara yake inathamini na kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na wadau hao hasa katika kukuza na kuviendeleza vipaji vya
vijana nchini, hivyo amewapongeza wadau hao kwa moyo wao wa kujitoa na
kuwataka kuendeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997
katika Sura ya 9 kifungu cha 9:5:8 ambacho kinasisitiza na kuhimiza
watu binafsi pamoja na Mashirika kuwekeza rasilimali katika sekta ya
utamaduni.
‘’Maonyesho
haya ni ishara tosha kuwa sanaa ni kazi, ajira, biashara na burudani,
hivyo kipekee nawapongeza sana’’, alisema Songoro.
Aliongeza
kuwa, Warembo ambao wameshiriki katika mashindano hayo wanautangaza
utalii wa ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo wanaiwakilisha vyema
Tanzania Duniani katika mashindano ya Miss World na pia kukuza uchumi
wa nchi.
Aidha,
amewataka warembo ambao hawakubahatika kuibuka washindi katika
mashindano hayo kutokata tamaa, bali waitumie fursa hiyo hususani ya
elimu waliyoipata wakiwa kambini kwa kuisadia jamii inayowazunguka na
kuwa wanawake wa mfano wa kuigwa katika kujitambua na kujiamini.
‘’Mtambue
kwamba, siyo wote mtakaoibuka washindi na kuendelea mbele katika
mashindano haya, niwaombe wale ambao hamtashinda msivunjike moyo, bali
mkaitumie elimu mliyoipata na yale ambayo mmejifunza mkiwa kambini kwa
kuisaidia jamii inayowazunguka na muwe wanawake wa mfano wa kuigwa’’,
alisema Songoro.
Katika
mashindano hayo, Mshindi wa Kwanza aliyeibuka na kunyakua taji hilo ni
Jackline Kimambo ambaye alipatikana kati ya tano bora na kuvikwa taji
la Miss Tanzania Indian Ocean 2016 na Mshindi wa pili ni Regina Ndimbo
huku wengine waliobaki kwenye tano bora wamepata fursa ya kuingia katika
mashindano ya Miss Kinondoni.
Shindano
hilo lilihusisha jumla ya washiriki wapatao 20 ambapo mmoja kati yao
ndiyo aliyeibuka mshindi na lilidhaminiwa na wadau mbalimbali wakiwemo
Mikocheni Resort Centre, Mlimani TV, Channel Ten, Darling, Helmic,
Tanzania Breast Cancer Foundation, Magic FM, Jozi Lounge, Kiss Printers
pamoja na NTS.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni