SIFA ZA MFUNGWA WA PAROLE NA UAMUZI WA BODI ZA PAROLE UNAVYOFANYIKA HAPA NCHINI
SIFA ZA MFUNGWA WA PAROLE
Sheria ya Bodi za Parole Sura 
400 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 1997 inaainisha kuwa mfungwa 
anayetumikia kifungo cha kuanzia miaka minne (4) na kuendelea anastahili
 kunufaika na mpango wa Parole kama atakuwa na sifa zifuatazo:-
i)  Asiwe amehukumiwa kifungo cha maisha;
ii) Asiwe ni mfungwa 
anayetumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, madawa
 ya kulevya na makosa yanayohusiana na kujamiiana;
iii) Asiwe ni mfungwa ambaye kifungo chake kimebatilishwa kutoka kwenye kifungo cha kunyongwa;
iv) Awe anatumikia kifungo kisichopungua miaka minne (4) au zaidi na awe ametumikia 1/3 ya kifungo chake;
v) Awe ameonesha tabia na mwenendo mzuri kwa muda wote aliokaa gerezani na;
vi) Asiwe na pingamizi la 
kimahakama la kukataliwa kunufaika  na utaratibu wa Parole chini ya 
Kifungu cha 67 cha Sheria ya makosa  ya Jinai.
UAMUZI WA BODI ZA PAROLE UNAVYOFANYIKA HAPA NCHINI
Kimsingi mfungwa anapoingia 
gerezani kwa mara ya kwanza hujulishwa kuhusu haki zake ikiwemo haki ya 
kuingizwa kwenye mpango wa Parole kama ana sifa kulingana na kosa lake 
na muda wa kifungo chake gerezani.  
Mfungwa mwenye sifa ya 
kuingizwa kwenye mchakato wa Parole anapotimiza 1/3 ya kifungo chake, 
Afisa Parole hukusanya taarifa mbalimbali zinazomuwezesha kujadiliwa 
katika Bodi za Parole;  Taarifa hizo ni maoni kutoka kwa wazazi/ndugu 
zake, maoni ya mwathirika wa uhalifu, nakala ya hukumu, hati ya kifungo,
 maoni kutoka uongozi wa kijiji anachotarajia kwenda kuishi na 
maoni/taarifa kutoka Kituo cha Polisi kilichomkamata na pia matokeo ya 
uchunguzi wa alama zake za vidole kuhusu kumbukumbu zake za uhalifu.  
Taarifa hizi zote huwa ni kwa ajili ya kudumisha usalama wa jamii na wa 
mfungwa mwenyewe anufaikapo kwa Parole.
Baada ya Taarifa hizi zote 
kukamilika kila mfungwa anayependekezwa kunufaika na Parole hufunguliwa 
jalada (Prison Form. 64) kwa ajili ya kutunza kumbukumbu zake pamoja na 
taarifa za tabia na mwenendo wa mfungwa. Mchakato wa kumjadili mfungwa 
huanzia katika Kamati za Urekebishaji ya Gereza. Kamati hiyo hupitia 
taarifa hizo na kutoa maoni na mapendekezo kwenda Bodi ya Parole ya 
Mkoa.  Bodi ya Parole ya Mkoa hupitia maoni na mapendekezo hayo na baada
 ya uchambuzi wa kina, hutoa mapendekezo yake kwa Bodi ya Taifa ya 
Parole kupitia kwa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole.
Sekretarieti ya Taifa ya Parole 
ina jukumu la kuratibu shughuli zote za Bodi. Hivyo hupokea taarifa za 
wafungwa waliopendekezwa au kutopendekezwa kunufaika na Parole kutoka 
katika Bodi za mikoa. Huchambua taarifa hizo na kuandaa taarifa ya kila 
mfungwa kwa ajili kujadiliwa na Bodi ya Taifa ya Parole.
Bodi hiyo kwa kutumia taaluma 
mbalimbali walizonazo wajumbe wake na nyadhifa zao hufanya uchambuzi wa 
kina wa mawasilisho hayo na kutoa uamuzi wa mfungwa anufaike au 
asinufaike na Parole. Uamuzi wa Bodi ya Taifa ya Parole huwasilishwa kwa
 Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa uamuzi wa mwisho kwa 
mujibu wa Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Bodi za Parole Na. 25 ya mwaka 
1994 (Sura ya 400 R. E 2002). 
Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya 
Ndani ya Nchi hupitia taarifa za kila mfungwa na kutoa uamuzi wa mwisho 
wa kukubaliwa au kukataliwa kunufaika kwa mpango wa parole. Uamuzi huo 
huwasilishwa kwa Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole ambaye ni Kamishna 
Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania. Itaendelea…… !.
MWANDISHI WA MAKALA HII NI AFISA NGAZI YA JUU WA JESHI LA MAGEREZA, KWA MAONI NA USHAURI – 0754 871084, lucasmboje@yahoo.co.uk or mbojelucus@gmail.com
 
 
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni