PROF. MBARAWA AFUNGUA MKUTANO WA NNE WA WADAU WA SIMU
………………………………………………………………………………………….
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezungumzia
umuhimu wa wananchi wa mjini na vijijini kutumia simu ili waweze
kunufaika na huduma mbalimbali za kimtandao zinazotumika hapa nchini.
Akizungumza
mara baada ya kufungua mkutano wa nne wa kimataifa wa chama cha kampuni
za simu duniani GSMA mobile 360, Prof . Mbarawa amesema Serikali
imejipanga kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano ya simu inawafikia
wananchi wote ili kuwezesha kunufaika na huduma za simu za kisasa.
‘Ili
wananchi waweze kupata maendeleo kwa haraka na kunufaika na fursa za
kimtandao katika masuala ya elimu, biashara, kilimo, afya na ustawi wa
jamii kwa ujumla kunahitajika uwepo wa simu za kisasa zinazoweza
kuruhusu mifumo ya kimawasiliano’, Amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameitaja
mifumo hiyo kuwa ni Elimu Mtandao, Afya Mtandao, Biashara Mtandao,
Kilimo Mtandao, Serikali Mtandao, Hali ya Hewa Mtandao ambavyo kwa
pamoja vitamhudumia mwananchi kwa ubora na wakati.
Amesisitiza
kuwa serikali inashirikiana kwa karibu na kampuni za mawasiliano ya
simu ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha huduma za simu zinakuwa za
uhakika na salama.
Serikali
inaendelea kuhakikisha kwamba mfuko wa Mawasiliano Vijijini unaendelea
kunufaisha watanzania na mkakati wa kuhakikisha umeme unafika vijijini
unaimarika sambamba na uwepo wa simu za kisasa za bei nafuu.
Takribani laini za simu milioni 39.9 nchini zinatumika katika huduma mbalimbali na hivyo huchangia uchumi wa nchi.
Waziri
Prof. Mbarawa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira
mazuri ya uwekezaji ili kukuza sekta ya mawasiliano hapa nchini ambapo
hadi sasa tayari kilomita 18,000/- za mkongo wa taifa wa taifa wa
mawasiliano zimejengwa hapa nchini.
“Serikali
itaendelea kudhibiti vifaa vya mawasiliano visivyo na ubora ili
visiingie nchini na hivyo kuhakikisha watumiaji wa mitandao ya simu
wanakuwa salama na wanaitumia mitandao hiyo kwa wakati wote’.
Amesisitiza Prof. Mbarawa.
Mkutano
huo wa siku mbili ambao pia umehudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu wa Nchi
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Bw. Thomas Luhaka ambapo
pamoja na mambo mengine utajadili Changamoto mbalimbali na kuja na
suluhisho na namna bora ya kuendeleza Sekta ya Mawasiliano duniani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni