SERIKALI YAANZISHA MPANGO MAALUM WA UPIMAJI WA ARDHI MAENEO YASIYOPIMWA JIJINI DAR ES SALAAM.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes
Kusiluka akiwaeleza waandishi wa Habari kuhusu mpango wa Serikali wa
kupima na kurasimisha maeneo yasiyopimwa katika jiji la Dar es salaam
leo.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
……………………………………………………………………………………………….
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Serikali
kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa mpango
maalumu wa upimaji wa Ardhi na Urasimishaji wa maeneo yote yasiyopimwa
katika jiji la Dar es salaam ambapo viwanja zaidi ya laki tatu
(300,000) vitapimwa na wamiliki wake kupewa Hati.
Akizungumza
leo jijini Dar es salaam kuhusu zoezi hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka amesema kuwa
Serikali imeamua kuja na mpango huo kwa sababu ya ukubwa wa jiji hilo na
wingi wa watu ulioambatana na ujenzi wa makazi holela.
“Katika
mwaka wa fedha 2016/2017 tumepanga kuwa na mpango maalum wa jiji la Dar
es salaam ambapo wataalam wetu watakwenda, kuhakiki mipaka na kupima
maeneo yote ambayo hayajapimwa na kutengeneza ramani zitakazoonyesha
maeneo ya barabara na maeneo ya huduma nyingine kwa kushirikiana na
wananchi husika.
Amesema
kuwa baada ya zoezi la uhakiki Serikali itatoa hati za maeneo hayo na
kusisitiza kuwa zoezi hilo litafanyika pia katika maeneo mengine ya miji
mikubwa nchini yenye watu wengi ikiwemo jiji la Mwanza.
Dkt.
Kusiluka amesisitiza kuwa urasimishaji utakuwa shirikishi kwa
kuwahusisha watu wote wa maeneo yatakayopimwa na Serikali ambapo
wananchi wenye nyumba watashirikiana na viongozi wa Serikali katika
mitaa kupanga na kuimarisha mindombinu ya maeneo yao pamoja na
kukubaliana maeneo ambayo barabara za mitaa zitapita, mitaro ya maji
machafu, magari ya kupitishia huduma za dharula kama Zimamoto nay ale ya
kubebea wagonjwa.
“Mpango
wa urasimishaji ni Shirikishi, wataalam wa ardhi watakwenda kwenye
maeneo yote yatakayopimwa hususan katika jiji la Dar es salaam na kukaa
na wananchi wote,kupitia mipaka wakishirikiana na wananchi wote kwa
uwazi ili zoezi hilo liwe na manufaa na tija kwa wananchi wote”
Amesisitiza Dkt. Kusiluka.
Amesema
kuwa licha ya kuwepo kwa sheria zinazoisimamia sekta ya Ardhi nchini
Tanzania bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
migogoro ya Wakulima na wafugaji, migogoro ya kijinai ya mtu mm kuvunja
nyumba au kuvamia eneo la mtu bila idhini, migogoro ya mipaka kati ya
majirani na ile inayosababishwa na wananchi kutokujua sheria.
Mbali
na sababu hizo amebainisha kuwa idadi ya watu na matumizi ya ardhi kwa
shughuli mbalimbali imekuwa ikiongezeka wakati ardhi ikibakia ileile
jambo linaloifanya sekta hiyo kuja na mikakati mbalimbali ya kukabiliana
na changamoto hizo kupitia watalaam waliopo.
Amesema
kuwa serikali imefanya mambo mbalimbali kuhakikisha kuwa inatatua kero
za wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali kwa kuwatumia wataalam
wake kupima na kupanga maeneo ya vijiji mbalimbali, kutoa elimu pia
kuajiri wataalam wa masuala ya Ardhi katika Halmashauri zote nchini.
Aidha amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kupima maeneo yote ya ardhi nchini ambayo hayajapimwa kupitia mpango wa miaka 10.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni