MAANA YA PAROLE, MADHUMUNI YAKE NA SHERIA ZA BODI YA PAROLE HAPA NCHINI
Mh Agustino Lyatonga Mrema Mwenyekiti wa Bodi ya Parole
……………………………………………………………………………………………………………..
Na; Lucas Mboje – Jeshi la Magereza,
Matokeo haya yalisababisha Bodi ya Taifa ya Parole kuishauri Serikali kupanua wigo wa sheria hii ili wafungwa wengi zaidi waweze kunufaika. Mapendekezo haya yalilenga kifungu cha nne cha sheria ya Bodi za Parole vifungu vidogo (a),(b) na (c) ambavyo vinataja kuwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya maisha, waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, madawa ya kulevya, kujamiiana na adhabu ya kifo iliyobadilishwa kuwa kifungo kwamba hawawezi kupata msamaha wa Parole. Ilipendekezwa kwamba kifungu hicho kirekebishwe ili wafungwa wote wa makosa hayo nao wafikiriwe kunufaika na utaratibu wa Parole bila kujali makosa waliyotenda.
PAROLE ni utaratibu wa kisheria unaompa fursa mfungwa
aliyehukumiwa kutumikia kifungo Gerezani cha miaka minne na kuendelea
kutumikia sehemu ya kifungo chake katika jamii kwa masharti maalum baada
ya kukidhi vigezo vifuatavyo:-
i). Awe ametumikia theluthi (1/3) ya kifungo chake na
kuonesha mwenendo wa kurekebika kurudi katika jamii kumalizia sehemu ya
kifungo chake kwa masharti maalum. Masharti hayo ni kuwa chini ya
uangalizi maalum kuhakikisha kuwa hatendi kosa lolote mpaka
atakapomaliza kifungo chake, kuzingatia masharti ya Parole anayopewa
kikamilifu pamoja na kuwa raia mwema na kuishi kwa kujipatia kipato
halali katika jamii;
ii). Awe ameonesha kujutia kosa, kurekebika tabia na kuonesha mwenendo mzuri gerezani na;
iii). Mamlaka husika kujiridhisha kuwa hatahatarisha usalama wa jamii.
Parole ni moja kati ya adhabu mbadala na imeonesha
mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani. Utaratibu huu ni wa
kipekee kwa kuwa unawagusa wafungwa wa vifungo virefu ambao ndio wengi
waliopo magerezani. Aidha, ni utaratibu unaoshirikisha jamii katika
urekebishaji kwa kuzingatia usalama wa jamii na dhana kwamba uhalifu ni
zao katika jamii.
Madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu wa Parole nchini
hayatofautiani na madhumuni ya kuanzishwa kwa utaratibu huu kwenye nchi
nyingine Duniani zikiwepo nchi za Afrika kama vile: Afrika kusini,
Zambia na Namibia. Mfumo wa Parole ulioainishwa hapa nchini unatokana
na uzoefu wa Parole unaotumika nchini Canada. Sababu zilizopelekea
kuanzishwa kwa Parole hapa Nchini ni:-
i. Kuhusisha jamii katika suala zima la urekebishaji wa
wafungwa badala ya kutegemea serikali peke yake kwani chanzo cha uhalifu
ni mazingira yanayotokana na jamii yenyewe.
ii. Kuwepo na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya wafungwa
wenye vifungo virefu magerezani ambao kutokana na urefu wa vifungo vyao
hawawezi kufaidika na programu zilizopo za urekebishaji kwa sababu ama
watatoka magerezani wakiwa wazee wasiojiweza, watakutana na mabadiliko
makubwa kijamii, kiuchumi na kisera wasiyoweza kuyamudu haraka/ipasavyo
kwenda na wakati au watafia gerezani.
Wafungwa wa aina hii hukata tamaa kwani hawaoni sababu ya
kuwa na nidhamu wawapo gerezani, hivyo kusababisha usalama magerezani
kuwa mashakani. Parole ilikusudiwa kuwarejeshea matumaini ya kurejea
katika jamii na kuishi maisha ya kawaida na kupunguza tishio la
kiusalama magerezani na katika jamii kwa ujumla.
Jeshi la Magereza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
liliwasilisha mapendekezo ya kutungwa Sheria ya Bodi za Parole nchini.
Mapendekezo hayo yalijenga hoja ambayo hatimaye iliwasilishwa katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba, 1994 na
kupitishwa rasmi kuwa Sheria ya Bodi za Parole Na. 25/1994.
Sambamba na kutungwa kwa Sheria hiyo, kanuni za Bodi za
Parole ziliandaliwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali tarehe 29
Agosti, 1997 (GN. 563/1997) hivyo kuwezesha Sheria hiyo kuanza kutumika
rasmi. Hata hivyo Sheria iliyopitishwa haikuzingatia mapendekezo
yaliyotolewa na Jeshi la Magereza ambayo yaliwalenga wafungwa wote
kunufaika na Parole bila kujali aina na uzito wa makosa. Aidha, Sheria
husika haikuanza kutumika mara moja kutokana na sababu zifuatazo:-
i. Bodi ya Taifa ya Parole na Bodi za Parole za Mikoa
zilizokuwa zimeundwa kwa mara ya kwanza zilivunjwa na kuundwa upya na
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kulalamikiwa kuwa
uteuzi wa Wajumbe wake haukuzingatia uwiano wa jinsia na dini.
ii. Kutokamilika kwa maandalizi ya nyaraka mbalimbali
muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Parole ikiwa ni pamoja na
uendeshaji wa semina kwa wajumbe wa Bodi za Parole za Mikoa yote nchini
ili kufanikisha uanzishwaji na utekelezaji wa Sheria hiyo.
Baada ya matukio hayo, kikao cha kwanza cha Bodi ya Taifa ya
Parole kilifanyika tarehe 19 Agosti, 1999 ambacho kiliwajadili wafungwa
watano (5) na kupitisha watatu(3) walioonekana kutimiza masharti ya
kuachiliwa kwa Parole nchi nzima. Idadi hiyo ni ndogo hasa ikizingatiwa
kwamba wakati huo magereza yote nchini yalikadiriwa kuwa na wafungwa
27,000. Kutokana na Wafungwa hao watano waliojadiliwa, ilidhihirisha
kuwa Sheria yenyewe ilikuwa haitekelezeki kama ilivyokusudiwa katika
mapendekezo yaliyowasilishwa na Jeshi la Magereza hapo awali.Matokeo haya yalisababisha Bodi ya Taifa ya Parole kuishauri Serikali kupanua wigo wa sheria hii ili wafungwa wengi zaidi waweze kunufaika. Mapendekezo haya yalilenga kifungu cha nne cha sheria ya Bodi za Parole vifungu vidogo (a),(b) na (c) ambavyo vinataja kuwa wafungwa wanaotumikia vifungo vya maisha, waliofungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, madawa ya kulevya, kujamiiana na adhabu ya kifo iliyobadilishwa kuwa kifungo kwamba hawawezi kupata msamaha wa Parole. Ilipendekezwa kwamba kifungu hicho kirekebishwe ili wafungwa wote wa makosa hayo nao wafikiriwe kunufaika na utaratibu wa Parole bila kujali makosa waliyotenda.
Kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Bodi ya Taifa ya
Parole, Sheria Na. 25/1994 ilifanyiwa marekebisho kwa Sheria Na. 5/2002
ambayo ilijihusisha na eneo dogo tu kwamba badala ya mfungwa
anayestahili Parole kuwa amehukumiwa kifungo cha miaka nane (8) na
kuendelea, ilirekebishwa na kuwa awe amehukumiwa kifungo cha miaka minne
(4) na kuendelea.
Chini ya marekebisho hayo Wakili wa Serikali Mfawidhi wa
kanda aliongezezwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Parole ya Mkoa. Hata hivyo
suala la aina ya makosa na urefu wa kifungo katika kufikiriwa kunufaika
kwa mpango wa Parole lilibaki kama lilivyokuwa hapo awali. Baada ya
marekebisho hayo ya Sheria ya Bodi za Parole, Bodi za Parole za Taifa
na Bodi za Mikoa zilizinduliwa upya mwaka 2003, na Bodi ya Taifa ya
Parole ilifanya kikao chake cha kwanza mwezi Agosti, 2003 ambacho
kilikuwa cha pili tangu Sheria hii ilipoanza kutumika rasmi nchini mwaka
1999.
Kwa mujibu wa Sheria na Sera za kitaifa kuhusu uboreshaji
wa Magereza zinazotolewa kufuatia kuridhiwa kwa maazimio mbalimbali ya
Kimataifa katika kuboresha hali za wafungwa magerezani, imeonekana kuwa
vifungo siyo njia pekee ya kumrekebisha mhalifu. Adhabu mbadala
zimeonekana ni bora zaidi kuliko kifungo kwa vile jamii huhusishwa
katika suala zima la kumrekebisha mhalifu.
Adhabu mbadala zinazotumika hapa nchini ni pamoja na
kulipishwa faini, Kuachiliwa kwa masharti, Probation, Kuachiliwa kwa
matazamio, Kifungo cha Nje (EML), Parole, Huduma kwa Jamii n.k. Aidha,
katika adhabu mbadala zilizoainishwa, Utaratibu wa Parole umeonekana
unafaa zaidi kwa kuwa ndugu, uongozi wa mtaa/kijiji na mwathirika wa
uhalifu hushirikishwa kutoa maoni kabla ya mfungwa husika kunufaika na
mpango huu. Aidha, ni adhabu mbadala pekee inayohusika na wafungwa
wanaotumikia vifungo virefu magerezani. Itaendelea …………wiki ijayo……!.
MWANDISHI WA MAKALA HII NI AFISA NGAZI YA JUU WA JESHI LA MAGEREZA, KWA MAONI NA USHAURI – 0754 871084, lucasmboje@yahoo.co.uk or mbojelucus@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni