RC MKOANI PWANI HANA GARI ALAZIMIKA KUTUMIA LA DC KISARAWE
MKUU wa mkoa wa Pwani pamoja na
katibu tawala wa mkoa huo hawana usafiri wa uhakika katika kutekeleza
majukumu yao ya kazi hali ambayo inasababisha mkuu wa mkoa huo kutumia
gari la mkuu wa wilaya ya Kisarawe ambae bado hajaripoti kazini.
Aidha baadhi ya wakuu wa wilaya
magari yao ni mabovu ikiwemo gari la mkuu wa wilaya ya Kibaha huku
maafisa tarafa 26 kati ya 27 waliopo mkoani hapo wanakabiliwa na tatizo
la kukosa pikipiki wanazotumia kwenye kazi zao.
Akizungumzia changamoto
zinazoikabili sekretarieti ya mkoa huo,mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi
Evarist Ndikilo alisema analazimika kutumia gari la mkuu wa wilaya ya
Kisarawe kwasasa.
Alielezea kuwa anatumia gari hiyo
kutokana na mkuu huyo wa wilaya bado hajamwapisha kutokana na kutoa
udhuru maalum na endapo mkuu huyo wa wilaya ataanza kazi yeye atakuwa
hana gari la kutumia.
Mbali na hayo ,mhandisi Ndikilo
alisema wanakabiliwa na changamoto nyingine ya uhaba wa fedha za
matumizi ya kawaida (OC)ambapo uhaba huo unatokana na kushuka kwa ukomo
wa bajeti mwaka hadi mwaka hususan katika mwaka wa fedha 2015/2016
ulishuka kwa asilimia 40 ikilinganisha na ukomo wa fedha katika kipindi
cha nyuma.
Alisema fedha pia za matumizi ya
kawaida zinazopokelewa kila mwezi ni pungufu tofauti na kiasi cha fedha
iliyopangwa hivyo kuathiri sekretarieti ya mkoa katika kutekeleza
majukumu yake.
“Changamoto hii ni kubwa ambayo
inasababisha kuzalisha changamoto nyingine ikiwemo madeni ya watumishi
ambayo hadi sasa yamefikia mil.152”
“Watumishi hawapati stahiki zao
kwa wakati na mazingira ya kazi yakikabiliwa na changamoto mbalimbali
hivyo watumishi wengine wanaamua kuhama na kwenda kufanya kazi kwingine
ambapo wanafikiri wataweza kutumiwa vizuri na kupata maslahi
mazuri”alisema mhandisi Ndikilo.
Akizungumzia juu ya upungufu wa
vitendea kazi alisema pikipiki kwa maafisa tarafa ni tatizo jingine
ambalo linahitaji kushughulikiwa.
Mhandisi Ndikilo alieleza ni tarafa moja ya Kaskazini Mafia iliyo nzima kati ya maafisa tarafa 27 waliopo mkoani Pwani.
Alisema kuwa maafisa tarafa hao
ni mkono wa kulia wa wakurugenzi na wakuu wa wilaya ndio wanaochapa kazi
katika pande hizo lakini hawana usafiri wa uhakika.
Alisema sekretarieti ya mkoa
,wataalamu na maafisa tarafa hushindwa kutembelea mamlaka za serikali za
mtaa na maeneo mbalimbali kwa lengo la kufuatilia miradi na shughuli
zinazopaswa kufuatilia na hata wakitembelea inakuwa sio kwa kiwango
kinachotakiwa .
Mhandisi Ndikilo alisema zipo
hatua wanazozichukua ikiwa ni sanjali na kufikisha changamoto hizo
katika wizara na idara husika ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Hatua nyingine ni madeni ya
watumishi kufikishwa hazina ili yaweze kulipwa licha pamoja na
kuwasilisha taarifa hizo lakini hazina bado haijalipa kwa wakati.
Hata hivyo Mhandisi Ndikilo
alielezea kwamba baadhi ya maafisa tarafa hawana ofisi za kudumu
wanalazimika kutumia ofisi ambazo hazina hadhi huku kukiwa hakuna huduma
muhimu za maji na umeme.
Mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi ya mkoa imeshajenga ofisi 6 kati ya 27 zinazohitaji kwa maafisa tarafa hao.
Mhandisi Ndikilo aliiomba ofisi
ya rais ,utumishi wa umma kuangalia kwa ukaribu matatizo hayo ili
kuyatafutia ufumbuzi kwani ni moja ya sababu zinazokwamisha utekelezaji
wa ufuatiliaji na jitihada za kuinua maendeleo ya mkoa kwa haraka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni