WANANCHI WA MWERA KIKOKANI HATARINI KUANGAMIA NA KIPINDUPINDU.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
BAADHI ya Wananchi wa Shehia ya
Mwera Kikokani Wilaya ya Magharibi “A” Unguja wameiomba serikali
kuwatembelea wahanga wa mafuriko wa maeneo hayo ili kufahamu changamoto
zinazowakabili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu, kabla hawajapata maafa
makubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wananchi hao wamedai kuwa toka wamepata mafuriko takriban wiki mbili
zilizopita hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyeweza kufika katika
eneo hilo kwa kuwafariji ama kutoa msaada wowote wa kibinadamu.
Akizungumza mmoja wa wakaazi wa
eneo hilo, Kadika Khamis alisema kuwa yeye ni miongoni mwa wananchi
waliokumbwa na mafuriko hayo na kuhama nyumba yake baada ya kujaa maji
ambapo kwa sasa ameomba hifadhi kwa jamaa zake.
Khamis alisema chanzo cha Mafuriko
hayo ni kutokana na mvua kubwa zilizonyesha na kujaza maji katika bonde
la Mtofaani ambayo njia yake imezibwa na ujenzi wa barabara pamoja
ujenzi holela na kusababisha maji hayo kuingia katika makaazi ya watu.
“Maeneo haya siyo sehemu ya
mabonde na hayajawahi kujaa maji wala kutokea mafuriko wakati wa msimu
wa mvua, hivyo hii ni mara ya mwanzo lakini imesababisha hasara kubwa
kwani mpaka sasa tumehama makaazi yetu na hatujui matatizpo haya
yataisha lini kwani mpasa sasda babo maji yapo katika majumba yetu kama
mnavyoyaona.”, alisema Khamis.
Kwa
upande wake, Rajab Simai alisikitishwa na kitendo cha viongozi wa
serikali hasa viongozi wa jimbo kushindwa kuwatembelea wananchi hao
ambao kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu.
Alisema kwamba kutokana na
mafuriko hayo kwa sasa wananchi hawana huduma muhimu za kibinadamu
zikiwemo malazi, chakula na maji safi kwani vyote vimeangamizwa na maafa
hayo.
“ Tunawaomba serikali kuu waje
wafanye japo ziara huku na kutuona maisha tunayoishi kwani watu wamehama
katika nyumba zao wengine zimeanguka, na tunaishi maisha magumu
tunahitaji msaada.”alisisitiza Simai.
Simai alieleza kwamba kutokana na
maji yaliyotwaama katika maeneo hayo ambayo ni makaazi ya watu na
kusababisha uharibifu wa miundombinu ya maji safi kuna hatari ya
wananchi kupata maradhi ya kipindupindu kwani maji wanayotumia kwa sasa
siyo salama na hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumzia hali hiyo Balozi wa
nyumba kumi, Sharifa Hassan Ali alikiri kuwepo kwa uharibifu wa makaazi
ya wananchi uliosababishwa na mvua za mafuriko zilizonyesha siku kadhaa
zilizopita.
Alisema kwamba baada ya kutokea hali hiyo alipeleka taarifa
kwa Sheha wa Shehia ya Mwera ili aweze kukagua na kuhesabu nyumba
zilizoathirika na kupeleka taarifa hiyo kwa ngazi za juu serikali lakini
hawakupata mrejesho wowote mpaka sasa.
Sharifa alisema kwamba kutokana na
hali iliyopo katika eneo hilo kuna baadhi ya wananchi wanatumia muda
mwingi kuwachunga watoto wao wasiende kuchezea maji machafu yaliyotwaama
katika eneo hilo ili wasipate maradhi ya kipindupindu.
Kwa
upande wake Sheha wa Shehia hiyo, Khamis Bilal Risasi alikiri kuwepo
kwa tatizo hilo na kufafanua kwamba yeye baada ya kupata taarifa za
maafa hayo alienda kukagua na kuwafariji wananchi waliopata maafa hayo.
Alipoulizwa suala la kutotoa
ushirikiano kwa wahanga wa mafuriko hayo, alikanusha na kueleza kwamba
yeye ni miongoni mwa viongozi wa serikali walioenda kukagua sehemu ya
tukio hilo.
“ Hao wananchi wanaosema kwamba
eti hakuna kiongozi yeyote aliyefika katika eneo hilo kuwafariji sio
kweli mimi pamoja na mwakilishi wa jimbo letu tulienda kuwakagua na
tukawataka waliokuwa hawana sehemu za kuishi tuwatengenezee kambi huko
Beit-el-sie wakakataa”. Alieleza Sheha huyo licha ya kutoweka wazi kama
taarifa hizo alizifikisha Idara ya Maafa Zanzibar au la.
Alisema kuwa robo tatu ya eneo la
shehia ya Mwera limezungukwa na mito ya maji pia kuna baadhi ya wananchi
wanaoishi maeneo ya juu wamejenga katika miundombinu ya kusafirisha
maji ya mvua hivyo mvua zikinyesha nyingi maji hayo yanakosa njia za
kupita na kupelekea kuvamia makaazi ya wananchi wasiokuwa na hatia.
Aidha alipoulizwa suala la kuwepo
kwa huduma za dawa za kutibu maji(water gurd) na vyandarua vya kuwagawia
wananchi, alisema kuwa aliwahi kupewa vidonge 300 ambavyo havikukidhi
mahitaji kwani aliwagawia baadhi ya wananchi waliopo katika mazingira
hatari ya kupata kipindupindi na mgao wa vyandarua alisema shehia hiyo
haijapata.
Akizungumzia maradhi ya
kipindupindu Sheha Risasi aliwasihi wananchi wa maeneo hayo kuweka
mazingira yao katika hali ya usafi kwa kutumia vyoo vilivyokuwa katika
sehemu salama pamoja na kuchemsha maji kabla ya kuyatumia ama kunywa ili
kujikinga na maradhi ya miripuko hasa kipindupindu.
Zaidi ya Nyumba zinazokadiliwa
kufikia 70 zimekubwa na mafuriko hayo na kati ya hizo nyumba 40 wakaazi
wake wamehama kutokana na maji kuingia ndani ya nyumba hizo na kuharibu
mali na miundombinu mbali mbali zilizokuwemo katika nyumba hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni