Juhudi za Serikali katika kupunguza umasikini nchini
…………………………………….
Pamoja na uchumi wa Tanzania
kuelezwa kukua kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka katika miaka ya
hivi karibuni, hali ya uchumi kwa wananchi nchini imekuwa si ya
kuridhisha hasa kutoka na wengi kukabiliwa na umasikini wa kipato
uliochangiwa na sababu mbalimbali.
Kihistoria wakati wa ukoloni
wananchi waliwekewa vikwazo kushiriki katika uchumi ili watawalike
kirahisi wakilazimika kujishughulisha na uchumi wa sekta isiyo rasmi
wakati sehemu kubwa ya sekta rasmi ilishikwa na watawala.
Wakoloni walitumia mbinu mahsusi
kuwaendeleza wazungu na wananchi wachache ikiwa ni pamoja na utoaji
wa mikopo, utoaji wa elimu, ugawaji wa ardhi na utoaji wa leseni za
biashara.
Kutokana na hali hiyo Serikali
ya Tanzania pamoja na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakipambana kila
kukicha ili kijikwamua kutoka katika umasikini wa kukosa hata milo
mitatu kwa siku na mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwemo afya, maji,
malazi, mavazi na elimu.
Juhudi za kuongeza kasi ya
ukuaji wa uchumi na kupambana na umasikini zimekuwa zikitekelezwa kwa
mikakati na mipango mbalimbali kuanzia mikakati ya kisekta na mikakati
ya mwananchi mmoja mmoja.
Katika kushiriki kikamilifu
kwenye shughuli za uchumi, wananchi wanakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa ujuzi na uzoefu
vikichochewa na upungufu wa elimu, mafunzo, mila na desturi potofu na
mtazamo wa
kimaendeleo.
Pia ukosefu wa masoko ya uhakika
au uwezo wa kuingia katika masoko yenye ushindani, ukosefu wa
ushirikiano, ushiriki hafifu na ukosefu wa sauti ya pamoja ya makundi
mbalimbali ya wananchi katika kusimamia maslahi yao ya kukubaliana na
matatizo yanayowakwaza wasishiriki kikamilifu katika shughuli za
kiuchumi katika sekta zao.
Awali Tanzania iliamua kupitisha
na kutumia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA)
wenye misingi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia inayozingatia matokeo
ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na kukabiliana na changamoto za
kukuza uchumi na kupambana na umaskini nchini.
Mkakati huo unaonesha kuwa
kiwango cha umaskini wa kipato kwa wananchi hakikubadilika kwa kiwango
cha kuridhisha ambapo kila Watanzania 100, ni Watanzania 36 walikuwa na
umasikini wa kipato kwa mwaka 2000/1 wakati Watanzania 34 walikuwa
masikini katika kipindi cha mwaka 2007.
Kiwango hiki cha umasikini wa
kipato kimetofautiana kutoka eneo moja hadi lingine, maeneo ya vijijini
yakiwa na asilimia 38 ya umasikini wa vipato katika mwaka 2007
ikilinganishwa na asilimia 39 ya mwaka 2000/1.
Baadae Serikali ya awamu ya nne
ikiongozwa na Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ilipambana vilivyo
kuhakikisha inasaidia watanzania hasa walioko katika kaya masikini
nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujikwamua katika
hilo.
TASAF inausimamiwa na kuutengewa
fedha na Serikali pamoja na kupata ufadhili kutoka kwa wadau wa
maendeleo, wakiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza
(DFID), Shirika la Maendeleo la Serikali ya Marekani (USAID) na Serikali
ya Uhispania (Spain).
Lengo kuu la mfuko huu ni
kuziwezesha jamii zenye kipato cha chini kuinua hali zao za kimaisha kwa
kuanzisha shughuli zitakazoinua uchumi wao kupitia taasisi kuanzia
ngazi ya kikundi na hatimae vikundi vitaunda jumuiya na hata kuunda
shirikisho la kuwakomboa.
Mfuko huo umekuwa na awamu kuu
tatu mpaka sasa za kuwezesha kaya masikini Tanzania kujikwamua kiuchumi.
Baada ya kukamilika kwa Awamu ya I na ya II, TASAF imeleta mafanikio
makubwa kwa pande wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
Kwa kuwa jamii masikini
zimewezeshwa kutekeleza miradi zaidi ya13,954 ( kwa awamu ya Kwanza
miradi iliyotekelezwa na kukamilika ni 1,704 na Awamu ya Pili jumla ya
miradi 12,250 ilikamilika).
Serikali imeendelea na jitihada
za kupunguza umaskini kwa kusimamia utekelezaji wa Awamu ya II na III ya
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kuhamasisha jamii
yenye kipato cha chini kujiwekea akiba na kuwekeza.
Kupitia Mpango huo, jumla ya
vikundi 1,620 vyenye wanachama 20,869 kwa upande wa Tanzania Bara na
vikundi 158 vyenye wanachama 1,843 kwa upande wa Zanzibar viliundwa na
kupewa mafunzo na hivyo kuwekeza.
Mbali na Taasisi mbalimbali
zilizokuwa zikiwafikia na kuwasaidia wananchi katika hili ukiwemo Mfuko
wa TASAF na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge
Tanzania (Mkurabita) lakini bado kuna kazi kubwa ya kuwafikia wananchi
masikini.
Kama hiyo haitoshi, hivi
karibuni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango aliwasilisha
mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2016/2017 hadi
2020/2021, ambao utajielekeza katika dira ya Taifa ya uchumi wa kati
ifikapo 2025.
Alisema mpango huo wa maendeleo
wa miaka mitano unalenga katika ukuaji wa viwanda vitakavyo chochea
mabadiliko ya uchumi na maendeleo ya watu kufikia uchumi wa kati wa
viwanda na kuwa na watu wenye ujuzi watakao chochea ukuaji wa uchumi
huo.
Aidha, alisema Serikali
itajikita katika kupunguza umasikini, kutengeneza nafasi za kazi
zitakazotokana na uboreshaji wa kilimo, mifugo na viwanda huku
akisisitiza nidhamu, kufanya kazi kwa bidii na kuachana na mazoea.
Alifafanua kuwa Serikali
itahakikisha kuna elimu bure, huduma bora za afya na upatikanaji wa maji
safi na salama, mambo yatakayo imarisha nguvu kazi ya Taifa na kufikia
lengo lililo kusudiwa.
Waziri Dkt. Mpango aliwataka
washirika wa maendeleo kusaidia juhudi hizo za Serikali katika mpango wa
miaka mitano na zaidi kwa kuwa anaamini kwa upande wa Serikali
imejidhatiti kupambana na vikwazo vinavyokwamisha kufikia lengo hilo
kama rushwa, kukosa uwajibikaji na suala la utawala bora.
Mbali na hayo, Serikali
imejiandaa kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli wakati cha kampeni ya uchaguzi mkuu
uliofanyika Octoba 2015 kwa kukipa kila kijiji nchini Sh milioni
50 katika mwaka wa fedha wa 2016-2017.
Akizungumza hivi karibuni Waziri
Mkuu Kassimu Majaliwa alisema kuwa Serikali imetenga kiasi cha
shiliingi 59 bilioni za Kitanzania kwa lengo la utekelezaji wa ugawaji
wa shilingi 50 milioni kila kijiji nchini.
Waziri Mkuu alisema mradi huo
unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutenga fedha hizo kwa kila
kijiji kuwa na mfuko wa uwekezaji kwa ajili uya kukopesha vikundi vya
wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa.
Wakati akijibu swali la Mbunge
wa Viti Maalumu, Halima Bulembo mjini Dodoma,Naibu Waziri Ofisi ya Rais
Sera, Uratibu, Bunge la Walemavu, Antony Mavunde alisema kuwa ahadi ya
Rais Magufuli ya kila kijiji kupewa Sh milioni 50 itaanza kutekelezwa
katika mwaka wa fedha wa 2016-2017.
Alisema kuwa utaratibu wa kugawa
fedha hizo unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi kwa
kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI).
“Pamoja na mikakati yote hiyo
vigezo ambavyo vimekuwa vikitumika katika kutoa mikopo na mitaji kwa
vijana ni umri usiozidi miaka 35 ambavyo ni kujiunga na Saccos za
vijana za wilaya na kuunda vikundi na kuvisajili kisheria,” alifafanua
Naibu Waziri huyo.
Aidha, alisema ili kuhakikisha
vijana wanakuwa wajasiriamali na wanaweza kupatiwa mikopo na mitaji,
serikali imejiwekea mikakati ya kutambua vijana na mahitaji yao katika
ngazi mbalimbali na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali
ya vijana.
Wito kwa wananchi wote kwa
ujumla kushirikiana kujitoa kwa dhati na kuzisimamia rasilimali fedha
zitolewazo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa ya kupambana na
umaskini nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni