WAWILI WA KUMFUATA COASTAL UNION WATAJULIKANA JUMAPILI IJAYO
| COASTAL UNION |
Wakati
Coastal Union ya Tanga ikiwa imeaga rasmi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
2015/16, swali linabaki kwa wadau wa soka nchini kwamba ni timu gani
itaungana na Wagosi wa Kaya kushuka daraja kutokana na timu tano kuwa
katika hatari?
Pazia
la msimu wa Ligi Kuu 2015/16 linatarajiwa kufungwa Jumapili ijayo Mei
22, mwaka huu na timu tano zinazoonekana kuwa katika hatari ya kuungana
na Coastal Union yenye pointi 22 (nafasi ya 16) kushuka daraja. Kati ya
timu hizo tamo, mbili ndizo zitaungana na Coastal kushuka daraja hivyo
kuwa na jumla ya timu tatu.
Timu
zote za Ligi Kuu tayari zimecheza mechi 29 na ambazo ziko kwenye hatari
ya kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15);
Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera
Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani
iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye
pointi 30 (nafasi ya 11).
Kwa
hali ya mambo ilivyo, licha ya kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu
ikilinganishwa na timu nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye
pointi 27 hadi 29 zinaweza kuishusha kama Wanakishamapanda hao
watapoteza mchezo wa mwisho au kupata sare huku wapinzani wao
wakishinda.
![]() |
| MGAMBO SHOOTING |
Kwa
mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Toto Africans
itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha
Stand United, wakati JKT Ruvu mgeni wa Simba ya Dar es Salaam kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wenyewe
Kagera Sugar watamaliza na Mwadui FC watakuwa kwenye Uwanja wa
Kambarage Shinyanga wakati Mgambo wataalikwa Azam FC kwenye Uwanja wa
Azam Complex ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam
ilihali African Sports ‘Wanakimanumanu’ wataifuata Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa Manungu, Mvomero mkoani Morogoro.
Mechi
nyingine ya kukunja jamvi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom zitakuwa kati ya
Mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Yanga itakayokuwa mgeni wa Majimaji ya
Songea kwenye Uwanja wa Majimaji wakati Mbeya City itakuwa mwenyeji wa
Ndanda FC ya Mtwara.
Mchezo
mwingine wenye presha utakuwa ni kwa Tanzania Prisons yenye pointi 48
ambayo licha ya kucheza na Coastal Union ambayo imeshuka daraja kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, itakuwa inafukuziwa na Mtibwa Sugar kuwa na nafasi
ya nne. Mtibwa Sugar ina pointi 47.
Hakuna
ubishi kwamba Tanzania Prisons itajizatiti licha ya kucheza na timu
ambayo haina nafasi katika Ligi Kuu msimu huu. Presha kubwa ni kwa Simba
na Azam ambazo zina tofauti ya pointi moja katika msimamo wa ligi hiyo
iliyoshirikisha timu 16.
Azam
FC ina pointi 63 ikishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga huku
Simba inayoshika nafasi ya tatu ina pointi 62. Mvutano wa Tanzania
Prisons, Mtibwa ni wa nafasi ya tatu na nne hasa ukirejea kwenye zawadi
za Vodacom ka timu vinara kama ilivyo kwa Azam na Simba.
Yanga
ambayo imetwaa ubingwa, tayari imepewa taji na medali kwa wachezaji 24,
viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya
Utendaji Jumamosi iliyopita na inachusubiri ni fedha Sh 81,345,723
wakati Azam na Simba zinawania zawadi ya mshindi wa Pili Sh 40,672,861
na Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 huku Prisons na Mtibwa Sugar zikichuana
kupata zawadi ya Mshindi wa Nne ambayo ni Sh 23,241,635.
Pia
timu zote zinawania zawadi ya Mchezaji Bora ambayo ni Sh 5,742,940
kiwango kinachofanana na atakachopewa Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa Bora
wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom wakati Mwamuzi Bora
atazawadiwa Sh 8,614,610 kiwango kinachofanana atakachopewa Kocha Bora
wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni