Watu wenye ulemavu wajengewe miundombinu rafiki kupunguza changamoto za kimaisha.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu
Mhe. Dkt Abdallah Possi akizungumza watu wenye ulemavu na wadau wa
maendeleo nchini mara baada ya uzinduzi wa kanzidata kwa ajili ya watu
wenye ulemavu nchini.
Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Uratibu,Bunge,Kazi,Ajira na Walemavu
Mhe. Dkt Abdallah Possi akifatilia uwasilishwaji wa kanzidata ya watu
wenyes ulemavu nchini iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Bwana Joachim Marege ni mtu mwenye ulemavu
asiyeweza kutembea. Baba huyu anakofanyia kazi inabidi apande lifti hadi
ghorofa ya kumi. Siku moja nikiwa nimeongozana naye kwenye lifti mara
ghafla umeme ukakatika. Baada ya lift kufunguliwa nikamsaidia kutoka
kwenye lift na kuendelea na safari yangu lakini kwa ndugu huyu
haikuwezekana kuendelea na safari yake kwa kupanda ngazi ilibidi asubiri
kwa muda hadi umeme utakaporudi ndo akapanda lift na kwenda ofisini
kwake. Hii ni changamoto sana kwa watu wenye ulemavu katika kupata
miundombinu rafiki ya kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku na
ambao idadi yao inaongezeka kila kukicha.
Mnamo Aprili 11 2016 Ofisi ya Taifa ya
Takwimu wakishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu walizindua kanzi data
maalum kwa ajili ya kupata takwimu za watu wenye ulemavu nchini.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya
Duniani, zaidi ya watu bilioni moja dunia sawa na asilimia 15 ya watu
wote duniani wanakadiriwa kuwa na aina fulani ya ulemavu. Idadi ya watu
wenye ulemavu inaongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ajali,
majanga ya asili na ya kusababishwa na binadamu, ongezeko la watu hasa
wenye umri mkubwa, magonjwa ya kuambukiza, magonjwa ya akili na matatizo
sugu ya kiafya.
Kuongezeka huku kwa idadi ya watu wenye
ulemavu, kunasababisha mahitaji makubwa ya huduma muhimu za kijamii.
Aidha, maisha ya watu wenye ulemavu yanakuwa magumu zaidi kutokana na
unanyanyapaa kutoka kwa jamii kwa ujumla, hali ambayo inahitaji
mabadiliko ya kimtazamo. Ni ukweli ulio wazi kwamba watu wenye ulemavu
hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania wana matatizo ya
upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya ikilinganishwa
na watu ambao hawana ulemavu.
Kulingana na takwimu za Shirika la Afya
Duniani (WHO), karibu asilimia 80 ya watu wenye ulemavu wanaishi katika
nchi zinazoendelea. Umaskini hupunguza uwezekano wa watu wenye ulemavu
kupata huduma za kijamii na haki nyingine za kimsingi. Kwa bahati mbaya
programu nyingi za maendeleo zimeshindwa kuzingatia mahitaji maalum ya
watu wenye ulemavu kinyume na makubaliano ya kimataifa yanayosisitiza
uzingatiaji huo kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Tumeshuhudia majengo yaliyojengwa muda mrefu
hata yanayojengwa sasa mengi hayazingatii mahitaji maalum kwa watu
wenye ulemavu. Inabidi katika ujenzi miundombinu rafiki kwa wenye
ulemevu iwekwe ili kuwapunguzia adha katika maisha watu wenye ulemavu.
Pamoja na umuhimu na uelewa uliopo bado
upatikanaji wa takwimu sahihi ni tatizo hasa katika nchi zinazoendelea
kama Tanzania. Kwenye ngazi ya kimataifa, bado kuna tofauti kuhusu nini
hasa maana ya ulemavu, suala ambalo husababisha ulinganifu wa takwimu
kuwa mgumu. Katika ngazi ya kitaifa, taarifa za watu wenye ulemavu
hazitoshelezi mahitaji ya kuweka misingi madhubuti ya kupanga na
kutekeleza programu za maendeleo zinazolenga kuboresha maisha ya watu
wenye ulemavu.
Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita
Serikali ya Tanzania kwa kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imefanya
juhudi kubwa za kukusanya na kuchambua takwimu za watu wenye ulemavu
kupitia tafiti mbalimbali na Sensa za Watu na Makazi za miaka ya 2002 na
2012. Pamoja na juhudi hizi bado ukusanyaji wa takwimu hizi mara zote
hukabiliwa na changamoto kadhaa. Changamoto kubwa ni ile inayohusiana na
mtazamo wa jamii kuhusu ulemavu na watu wenye ulemavu kwa ujumla. Tabia
ya kuwaficha watu wenye ulemavu kwa visingizio mbalimbali hukwamisha
upatikanaji sahihi wa idadi au taarifa ambazo zinahusiana na watu wenye
ulemavu.
Changamoto nyingine ni watu kutojua maana
halisi ya ulemavu. Watu wengi huchukulia ulemavu kuwa ni hali ya mtu
kutoweza kabisa kufanya jambo fulani. Mfano kutosikia au kuona kabisa na
kadhalika. Tafsiri ya ulemavu sio sahihi na huwaacha watu wengi wenye
ulemavu katika tafiti na sensa zetu. Maana halisi ya ulemavu ni ile
ambayo ilitolewa kwenye Tamko namba 61/106 la Umoja wa Mataifa kuhusu
Haki za Watu wenye Ulemavu. Kulingana na Tamko hili, watu wenye ulemavu “ni
watu wote wale ambao wana matatizo ya muda mrefu ya viungo , akili ,
uelewa , au hisia ambavyo kwa pamoja na vikwazo vingine vinaweza
kusababisha ushiriki wa mtu kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za
kijamii kama watu wengine”.
Utafiti kuhusu watu wenye Ulemavu nchini
uliofanyika Mwaka 2008, ulionyesha kuwa asilimia 8 ya watu wote nchini
wenye umri wa miaka 7 na kuendela walikuwa na ulemavu wa aina moja au
nyingine. Taarifa za watu wenye ulemavu pia zilikusanywa kwenye Sensa ya
Watu na Makazi ya Mwaka 2012 na kuonyesha kuwa asilimia 9 ya watu wote
nchini walikuwa na ulemavu. Matokeo ya tafiti hizo na Sensa
yanadhihirisha kwamba kiwango cha ulemavu ni kikubwa katika maeneo ya
vijijiji kuliko mijini. Kulingana na matokeo ya Sensa ya Mwaka 2012,
kiwango cha ulemavu vijijini kilikuwa ni asilimia 9.4 sawa na watu
milioni 2.9 ikilinganisha na asilimia 7.3 sawa na watu 560,000 kwa
maeneo ya mijini huku kiwango cha ulemavu ni kikubwa kwa Tanzania bara
kwa asilimia 9 sawa na watu milioni 4.4 kuliko Tanzania Zanzibar
asilimia 7 sawa na watu 55,355.17. Pamoja na juhudi hizo Ofisi ya Taifa
ya Takwimu imekuwa ikikusanya pia taarifa za watu wenye ulemavu katika
tafiti nyingine. Tafiti hizo ni pamoja Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa
Kufanya Kazi na Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi.
Kulingana na Utafiti wa Watu Wenye Uwezo
Kufanya Kazi wa Mwaka 2014, mikoa yenye watu wengi wenye ulemavu ni
Tanga (asilimia 7.2), Mara (asilimia 6.3) na Dar es Salaam (asilimia
5.8).Pia inaonyesha mikoa yenye watu wengi wenye ulemavu wanaojua kusoma
na kuandika ni Dar es Salaam (asilimia 89.5), Kilimanjaro (asilimia
84.7) na Mjini Magharibi (asilimia 83.7).Hali
ya ajira kwa watu wenye ulemavu inaonyesha kuwa wengi wameajiriwa
kwenye sekta ya kilimo. Hali ya kipato kwa watu wenye ulemavu
walioajiriwa kwa mwezi ni kati ya Tshs. 65,000 na Tshs. 500,000, na kwa
wale ambao wamejiajiri kipato chao ni kati ya Tshs. 65,000 na
Tshs.300,000.
Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2012 yanaonesha kuwa kiwango cha kujua kusoma na kuandika ni asilimia
70.1 ya watu wote wenye ulemavu wanaojua kusoma na kuandika
ikilinganishwa na asilimia 78.9 ya watu ambao hawana ulemavu. Vile vile
matokeo hayo yanaonesha kuwa kiwango cha kuandikishwa shuleni kwa watoto
wenye ulemavu ni kidogo pia ukilinganisha na watoto ambao hawana
ulemavu kwani kulingana na matokeo hayo ni asilimia 75 ya watoto wenye
ulemavu wenye umri wa miaka 7 – 13 waliokuwa wameandikishwa shule
ukilinganisha na asilimia 77 ya watoto ambao hawana ulemavu.
Tofauti zote hizi ni matokeo ya mtazamo
walio nao baadhi ya watu hapa nchini kwamba hakuna sababu ya kumpeleka
mtoto mwenye ulemavu shule. Lakini, hata pale ambapo mzazi anakuwa
tayari kumpeleka mtoto mwenye ulemavu shuleni miuondombinu isiyozingatia
mahitaji ya watu wenye ulemavu inaweza kumzuia asifanye hivyo. Umbali
wa kwenda shule ni chanzo cha watoto wa aina hii kutopelekwa shule.
Pamoja na kuwepo kwa taarifa hizi
zinazotokana na Sensa na tafiti, lakini vile vile kuna takwimu ambazo
hukusanywa na taasisi mbalimbali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao
za kikazi. Hata hivyo, takwimu hizi hazijawekwa pamoja na katika hali
rafiki ili kumsaidia mtu au taasisi inayozihitaji. Aidha, inawezekana
pia kuwa ukusanyaji wa takwimu hauzingatii vigezo vinavyokubalika na
Serikali na taasisi za watu wenye ulemavu. kwa kutambua hali hiyo na
Wizara inayoshughulikia watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu na Vyama vya Watu wenye ulemavu iliandaa kanzidata (database)
ambayo ina takwimu muhimu kuhusu taarifa za watu wenye ulemavu nchini.
Kwa kuanzia, kanzidata hii ina takwimu zinazotokana na Sensa na baadhi
ya taifiti ambazo zimefanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Kanzidata hii itakuwa ikiboreshwa mara kwa
mara kwa kuingiza vyanzo vipya vya takwimu hasa vile vitokanavyo na
taarifa za kiutawala kila zinapopatikana na inategemea kuwa msaada kwa
watu wenye ulemavu kupata fursa mbalimbali za kujikwamua kichumi kwa
sababu takwimu sasa zitakuwepo ambazo zitasaidia Serikali pamoja na
asasi mbalimbali kuwawezesha watu wenye ulemavu nchini kujikwamua
kiuchumi kwa kuwawezesha mikopo ya kufanya shughuliza za ujasiriamali,
kuwawezesha kupata elimu na huduma bora za afya na huduma nyingine za
kijamii.
Kanzidata hii itasaidia mambo kadhaa muhimu.
Lakini kubwa zaidi ni upatikanaji wa taarifa hizi katika mfumo rafiki
utakaosaidia watumiaji kufanya uchambuzi wa kina zaidi kulingana na
mahitaji yao. Aidha, kanzidata hii itasaidia uelewa wa watu kuhusu
ulemavu kwa ujumla na umuhimu wa kuhusisha mahitaji ya watu wenye
ulemavu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Mwaka huu wa 2016 dunia kwa ujumla itaanza kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo (Sustainable Development Goals).Utekelezaji
huu ni wa miaka 15 ijayo baada ya kukamilika Malengo ya Millenia ya
Mwaka 2015. Moja ya mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa
Malengo ya Milenia ni ukosefu wa takwimu za kutosha kwa ajili ya
kufuatilia na kutathmini utekelezaji na kuachwa kwa baadhi ya sehemu ya
jamii. Ndio maana, kauli mbiu kuu ya Malengo Endelevu ya Maendeleo ni
“Hakuna atakayeachwa Nyuma” (Leaving no One Behind) na hivyo ni
muhimu kuhakikisha kuwa kuna taarifa za kutosha kwa ajili ya kufuatilia
na kutathmini Malengo mara utekelezaji utakapoanza baadaye mwaka huu.
Suala la watu wenye ulemavu ni mtambuka na
hivyo linajitokeza katika Malengo yote yanayozungumzia maendeleo
endelevu ya binadamu. Lengo Namba 1, kwa mfano, linazungumzia kumaliza
umaskini wa aina zote kwa watu wote. Lengo Namba 4, linazungumzia
kumaliza tofauti za aina yoyote kwenye suala elimu n.k. Kwa kutambua
ukweli huo, Wizara husika kwa kushirikiana na wadau wengine inaandaa
Andiko la Mradi ili kuweza kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za
watu wenye ulemavuni wakati muafaka kwa wadau wote wa ndani na nje kuwa
tayari kuunga mkono juhudi hizi za Serikali mtakapoombwa kufanya hivyo.
Juhudi hizi ni pamoja na kujenga mfumo ambao utaiwezesha Serikali
kupata takwimu za watu wenye ulemavu kwa haraka na usahihi zaidi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera,Bunge,kazi,Ajira na watu wenye Ulemavu Dkt Abdallah Possi ametoa
wito kwa Wananchi na wadau wa maendeleo hasa asasi za kiraia kusoma
taarifa hizi na kuzitumia vizuri taarifa zilizopo kwenye kanzadata hii
kwa kuwa zimezingatia vigezo vyote vya takwimu bora na zimetolewa na
taasisi zenye mamlaka ya Kisheria kufanya hivyo. Zitumieni kwa lengo
moja kuu ambalo ni kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu nchini kwa
kuondoa unyanyapaa katika jamii yetu na kushinikiza mabadiliko katika
sera na programu za maendeleo. Wananchi mnaombwa kutoa ushirikiano wa
kutosha wakati wa tafiti zinazolenga kupata taarifa za watu wenye
ulemavu. Toeni taarifa zao kamili ili Serikali iweze kupata takwimu
sahihi na hivyo kurekebisha sera na programu zake za maendeleo.
Mafaniko ya uazishwaji na utekelezaji wa
matumizi ya kanzi data hii imetokana na washirika wetu wa maendeleo
ambao wamesaidia juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya watu
wenye ulemavu na Watanzania kwa ujumla. Taarifa nyingi ambazo zipo
kwenye kanzidata hii zimepatikana kwa ushirikiano na Serikali na wadau
mbalimbali wa maendeleo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni