RAIS DK. SHEIN AZUNGUMZA NA BALOZI MTEULE NCHINI JAPAN
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akizungumza na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini
Japan Mhe,Mathias M.Chikawe alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kuonana na Rais,leo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akiagana na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini
Japan Mhe,Mathias M.Chikawe alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao,[Picha na ikulu.]
………………………………………………………………………………………………….
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya
kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na
Japan hasa kwa kutambua hatua za nchi hiyo za kuendelea kuiiunga mkono
Tanzania katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko
Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe. Mathias Meinrad
Chikawe
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inajivunia
uhusiano na ushirikiano mzuri pamoja na hatua za Japan za kuendelea
kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miradi kadhaa hapa nchini.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali
ya Japan imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa upande wa Zanzibar na
Tanzania Bara kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika
kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya maji,
umeme, kilimo, afya na miradi mengineyo.
Alisema kuwa Serikali ya Japan
pamoja na Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa muda mrefu zimekuwa
zikiunga mkono uimarishaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini ambapo kwa
upande wa Zanzibar nchi hiyo imeweza kusaidia mradi mkubwa wa maji
katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao hivi sasa upo katika awamu ya tatu.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema
kuwa Serikali Japan imeweza kusaidia miradi kadhaa ukiwemo ule wa
kusambaza umeme vijijini hasa katika Mkoa wa Kusini Unguja huku akieleza
mpango wa nchi hiyo wa kusaida ujenzi wa soko la kisasa la samaki huko
Malindi mjini Unguja sambamba na usambazaji wa huduma za umeme ukiwemo
ule wa vijijini na miradi mengineyo ya maendeleo.
Dk. Shein, pia, alimueleza Balozi
huyo umuhimu wa kuimarisha sekta ya uwekezaji hasa katika viwanda kwa
kutumia uvuvi wa bahari kuu kwa kuzingatia kuwa ukanda wa bahari
unaoizunguka Zanzibar una samaki wengi wa aina ya jodari ambao ni wazuri
na wanapendwa sana duniani.
Aidha, Dk. Shein alieleza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo
hasa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji ambapo lengo la Serikali kati
ya mwaka 2018-2019 ni kuzalisha nusu ya mahitaji ya mchele unaotumika
hapa nchini ambao hivi sasa unaagizwa nje ya nchi.
Dk. Shein pia, alitumia fursa
hiyo kumueleza Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuitangaza zaidi Tanzania
kiutalii hasa kwa kuweko vivutio kadhaa kama fukwe nzuri za bahari kwa
Zanzibar na mbuga za wanyama kwa Tanzania Bara.
Nae Balozi mpya wa Tanzania
nchini Japan Mhe. Mathias Meinrad Chikawe alitoa pongezi kwa Dk. Shein
pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe
Magufuli kwa kupata uteuzi wake huo.
Balozi Chikawe alimuhakikikishia
Dk. Shein kuwa katika wadhifa wake huo mpya juhudi za makusudi
atazichukua katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya
Japan na Tanzania unaimarishwa zaidi sambamba na kuyafanyia kazi
maelekezo yote aliopewa na Rais Dk. Shein.
Kabla ya kupangiwa kituo hicho cha kazi Balozi Chikawe aliteuliwa kuwa Balozi mnazo tarehe 14 Februari mwaka huu.
Balozi Chikawe aliwahi kuwa
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea kati ya mwaka 2005 na 2015, na kwa vipindi
tofauti katika Serikali ya Awamu ya nne alikuwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora ambapo pia aliwahi
kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni