Waziri Mkuu awataka wabunge wa upinzani kurejea Bungeni
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
leo, Bungeni Mjini Dodoma amewataka wabunge wa upinzani ambao wamesusia
vikao vya Bunge tangu Mei 30 kuingia Bungeni na kuacha kususia vikao vya
Bunge kwani hakuna tija kwa Taifa.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akitoa hutuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la kumi na moja.
“kitendo cha baadhi ya
waheshimiwa wabunge kususia vikao vya Bunge hakitoi picha nzuri kwa
wananchi waliotuchagua kuwasilisha matatizo yao katika Bunge hili, hivyo
natoa rai kwa waheshimiwa wabunge hao kutafakari upya uamuzi wao na
niwasihi kwa busara zao waingie ili kwa pamoja na kwa ushirikiano tuweze
kutoa ushauri kwa Serikali,” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha Mhe. Majaliwa alitoa
ufafanuzi juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977
ambayo imetoa haki na kinga kwa waheshimiwa wabunge ili kujadili na
kuhoji utendaji wa Serikali kwa uhuru bila mashaka yoyote ya kuweza
kushitakiwa wanapotimiza wajibu wao wakiwa Bungeni.
Aliendelea kwa kusema kuwa kinga
ya aina hiyo haijatolewa kwa mwananchi yeyote yule Nchini ila kwa
Wabunge, hivyo basi hakuna mbunge aliyefungwa mdomo labda aamue
kujifunga mdomo yeye mwenyewe.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa Bunge
linaongozwa na Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge, hivyo ni
vyema zikafuatwa kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima na endapo kuna
utata katika jambo lolote ndani ya Bunge zipo taratibu zilizowekwa na
kanuni za kufuata ili kupata ufumbuzi na si kwa kususa kuingia Bungeni
kwani hakuna tija kwa Taifa.
Wabunge wa upinzani wamesusia
vikao vya Bunge tangu Mei 30, 2016 mpaka leo Juni 30 ambapo Bunge
limehitimishwa. Aidha wabunge hao wamekuwa wakiingia Bungeni kila
asubuhi na jioni kisha kutoka mara tu Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson
anapomaliza kusoma Dua maalum la kuliombea Bunge na Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni